Social Icons

Pages

Wednesday, December 31, 2014

WAFANYABIASHARA YA MAGAZETI WALALAMIKIA RISITI WANAZOPEWA DAR

Afisa Uhusiano wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera.
Wafanyabiashara wa magazeti katika Stendi daladala ya Mawasiliamo jijini Dar es Salaam wameulalamikia uongozi wa kituo hicho kuwatoza ushuru mkubwa ambao haulingani na kipato wanachokiingiza kwa siku.
Walisema pamoja na kutozwa ushuru huo mkubwa pia wanapewa risiti za mabasi ambazo hazihusiani na biashara yao. Walisema kuwa walianza kutozwa ushuru wa Sh. 2,000 kwa siku tangu Novemba 3, mwaka huu na kupewa risiti hizo pasipo maelezo yoyote.
“Sisi tunauza magazeti, kwa nini tupewe risiti za mabasi na sio za biashara husika na kwa muda sahihi?” alihoji Abdulmalik Siraji. Alisema pia risiti hizo wakati mwingine zinakuwa  za tarehe iliyopita huku mabavu na lugha mbaya vikitumika watoza ushuru hao wanapokwenda kuchukua fedha hizo.
“Mbona daladala zinatozwa Shilingi 500 kwa ruti za ndani ya Jiji na Shilingi 1,000 kwa ruti za nje? Kwa nini nao wasipandishiwe?” alihoji Johari Twaha.
Meneja wa kituo hicho, Michael Simkanga, alisema inawalazimu kutumia risiti za mabasi tokana na mashine wanazotumia kuandaliwa kwa ajili ya ushuru wa mabasi kwa kuwa Manispaa haikuandaa mashine za kutoa risiti maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara wa magazeti. “Mashine hizi zimetolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni maalum kwa ajili ya ushuru wa mabasi, hivyo inatulazimu kuzitumia pia kwa wafanyabiashara hao mpaka pale itakapoletwa mashine nyingine maana hatuna namna kwa sasa, tunafanya hivi ili kukabiliana na gharama za uendeshaji,” alisema Simkanga.
Alisema kiwango hicho kimewekwa na Manispaa, hivyo wao wametekeleza agizo na walikubaliana na makampuni yanayotoa magazeti. Aliongeza kuwa risiti hizo hutolewa asubuhi kwa kuzingatia idadi ya wafanyabiashara waliopo, hivyo kwa wale ambao tarehe husika wanakuwa hawajafungua ofisi wanazitunza na kuzitumia kwa kubadili tarehe iliyopita na kuweka ya siku husika kwa kuwa zinakuwa tayari zimeshaingia katika mahesabu yao. Afisa uhusiano wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera, alisema Manispaa haijawi kutoa kibali kwa mfanyabiashara yeyote katika stendi hiyo.

CHANZO: NIPASHE

No comments: