Bendera ya Palestina
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshindwa kupitisha azimio la
kuitaka Israel kuacha kulikalia kwa mabavu eneo la Ukingo wa Magharibi
ifikapo Disemba 31, mwaka 2017 pamoja na kuruhusu Palestina kuwa taifa
huru.
Ufaransa, Urusi na China ni miongoni mwa nchi nane zilizopiga kura
kuliunga mkono azimio hilo, lakini Marekani na Australia wamepiga kura
ya kulipinga. Nchi nyingine tano ikiwemo Uingereza, hazikupiga kura.
Balozi wa Jordan kwenye Umoja wa Mataifa, Dina Kawar, amesema hiyo ni
haki halali ya watu wa Palestina ambayo wameichagua katika juhudi za
kutafuta amani ya Mashariki ya Kati. Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Samantha Power, amesema
wamepiga kura kulipinga azimio hilo siyo kwa sababu wanaridhishwa na
hali iliyopo, bali kwa sababu amani inapaswa kupatikana kwa njia ya
mazungumzo ya maafikiano.
Siku ya Jumatatu mataifa 22 ya Kiarabu yakiwakilishwa na Jordan
kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, yalikubali kuliunga mkono
pendekezo la Palestina kuhusu marekebisho ya azimio la Umoja wa Mataifa
la kutaka Israel kuacha kuikalia kimabavu Palestina katika kipindi cha
miaka mitatu ijayo.
Power ameukosoa uamuzi wa kupelekwa kwa muswada wa azimio hilo kwa
ajili ya kupigiwa kura na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa
kuwa halitazikutanisha pamoja kwa karibu pande zinazohasimiana.
Palestina yasema ujumbe wao umekataliwa
Balozi wa Palestina kwenye umoja huo, Riyad Mansour amesema ujumbe
wao ulikuwa ni juhudi kubwa na zenye uhalisia kwa ajili ya kufungua
mlango wa amani, lakini kwa bahati mbaya Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa haliko tayari kuusikiliza ujumbe huo. Muda mfupi kabla ya kura hiyo, wanadiplomasia wa baraza hilo
walitarajia azimio hilo litapata kura tisa za ''ndiyo'', lakini Nigeria
ambayo inaaminika kuliunga mkono azimio hilo, haikupiga kura. Balozi wa
Nigeria kwenye Umoja wa Mataifa, Joy Ogwu, ameunga mkono msimamo wa
Marekani akisema kuwa njia ya mwisho ya amani inaegemea katika suluhisho
la mazungumzo.
Marekani, ambayo ni mwanachama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa na mshirika wa karibu wa Israel, imesema pendekezo hilo
la Palestina halina manufaa. Siku ya Jumatatu, msemaji wa Wizara ya
Mambo ya Nje ya Marekani, Jeff Rathke aliwaambia waandishi wa habari
kwamba azimio hilo jipya siyo jambo ambalo wanaweza wakaliunga mkono na
kwamba nchi nyingine zina mtazamo sawa na Marekani.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema
iwapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa haitolikataa azimio hilo,
wao watalipinga. Amesema mamlaka ya Palestina inajaribu kuweka amri kwa
Israel ambayo itadhoofisha usalama wa Israel na kuuweka mustakabali wake
wa baadaye katika hatari. Amesema Israel itayapinga mazingira yoyote
yatakayohatarisha maisha yake ya baadaye.
Wasiwasi kuhusu kuzuka mvutano kati ya Israel na Palestina
umeongezeka baada ya mazungumzo ya amani kushindikana mwezi Aprili mwaka
huu, hali iliyosababisha kuanza kwa mashambulizi wakati wa majira ya
joto yaliyowaua maelfu ya Wapalestina.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment