Social Icons

Pages

Wednesday, December 24, 2014

UKAWA: SABABU 10 ZILIZOTUPANDISHA CHATI

Wenyekiti wa UKAWA Freeman Mbowe (CHADEMA), Profesa Ibahimu Lipumba (CUF) na James Mbati (NCCR-Mageuzi). Hakuna ambaye alitarajia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na vijiji mwaka huu kama ungekuwa na upinzani mkubwa kama uliotokea.
Tumeshuhudia katika uchaguzi huu, watu wakipigana hadi damu kumwagika, nyumba kuchomwa moto, masanduku ya kura kuibwa na kura kuchomwa moto na hata kukamatwa kwa baadhi ya wabunge na wanasiasa. Uchaguzi huo uliofanyika kuanzia Desemba 14, mwaka huu, licha ya kuwa na upungufu mkubwa uliosababisha kurejewa katika maeneo kadhaa, lakini umetoa funzo kubwa kwa Watanzania na hasa vyama vya kisiasa.
Uchaguzi wa mwaka huu, tofauti na chaguzi zilizopita, umewaweka matatani wakurugenzi wa halmashauri 17, sita kati yao wakifukuzwa kazi, watano wakipewa onyo na wengine sita wakisimamishwa. Jingine kubwa, katika uchaguzi huu, ulikuwa ni muungano wa vyama vya upinzani, kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuamua kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi mbali mbali.
Katika chaguzi zote zilizopita tangu kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, hakukuwahi kuwa na muungano kama huu. Ingawa mara kadhaa, viongozi wa upinzani walikuwa wakikutana na kukubaliana kuungana na kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi mbali mbali, lakini wamekuwa wakivurugana.
Safari hii, Katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, walau baadhi ya vyama vinavyounda Ukawa walikubaliana kusimamisha mgombea mmoja katika maeneo kadhaa nchini. Licha ya mpango huu, pia kukabiliwa na vikwazo kidogo, lakini kwa kiasi kikubwa umeweza kuvinufaisha vyama vya upinzani kwa kuwaunganisha wanachama wao kupambana na wana CCM katika kura.
Vyama ambavyo viliungana kupitia ukawa ni Chadema, CUF, NLD na NCCR- Mageuzi. Muungano huu umesababisha matokeo tofauti kubwa ya matokeo ikilinganishwa na ule wa mwaka 2009. Takwimu zinasoma wakati mwaka 2009 CCM ilishinda vijiji 9,800, mwaka huu imeshinda vijiji 7,290 licha ya vijiji kadhaa kuongezwa katika maeneo mengi nchini.
Kwa upande wa Serikali za mitaa, CCM mwaka 2009 ilishinda vitongoji 2,242 lakini safari hii, imeanguka kwa kushinda vitongoji 2,116 tu licha ya vitongoji vipya vingi kuongezwa.
Upinzani kwa ujumla imefanya vizuri kwa kuongeza viti, kwa vyama vya Chadema na CUF, wakati chadema mwaka 2009 walikuwa na uongozi wa vijiji 289 mwaka huu, wameshinda na kupata viti 1,248. upande wa vitongiji walikuwa na 124 na sasa wameshinda 753.
Chama cha Wananchi CUF walikuwa na viti 407 vya vijiji, mwaka 2009 lakini sasa wanaviti 945 wakati walikuwa na vitongoji 133 lakini sasa wanavitongoji 235 .
Matokeo haya ni kabla ya marejeo ya uchaguzi uliofanyika Desemba 21, katika maeneo mbali mbali nchini.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika na Naibu Mkurugenzi wa habari na Uenezi-CUF, Abdul Kambaya, wajumbe wa sekretarieti ya Ukawa, wamezungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti na kueleza siri ya mafanikio yao katika uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa. Wote kwa pamoja wanatoa sababu zinazofikia 10 ambazo wanaamini ndizo zimechangia ushindi wao kama Ukawa katika uchaguzi huo na kuzitaja.

Ziara za mikoa na operesheni mbali mbali.
Mnyika anasema tofauti na miaka ya nyuma, vyama vya upinzani vilikuwa vikitupiwa lawama kuwa ni vyama vya uchaguzi kwani baada ya chaguzi kwisha hupotea lakini tangu uchaguzi wa mwaka 2010 hali imebadilika.
Anasema safari hii baada ya uchaguzi wa mwaka 2010, vyama vya upinzani hasa Chadema, hawakulala waliendelea na mikutano mikoani na operesheni mbali mbali ambazo zilikwenda sambamba na kutolewa elimu ya uraia, “tulikuwa na operesheni Sangara, tukaja vuguvugu la mabadiliko, Delete CCM kabisa na nyingine nyingi ambazo zimesaidia kufikisha ujumbe hadi vijijini,” anasema

Chadema ni msingi.
Mnyika anasema katika maeneo mengi nchini, kupitia mikutano ya chini kwenye matawi waliibua kampeni ya Chadema ndio msingi, kutokana na mikutano iliyofanyika vijijini. Anasema mpango huu ulisaidia sana kukijenga chama hicho vijijini tofauti na miaka ya nyuma kwani vikao vilifanyika kutathimini mabadiliko.
Anasema katika mpango huo, walikubaliana kuwa na mtandao wa upinzani vijiji hadi kuwa na mabalozi jambo ambalo limefanikiwa sana.

Muungano wa UKAWA.
Abdul Kambaya na Mnyika wanasema muungano wa Ukawa umekuwa na mafanikio makubwa, kwani awali walikuwa na migongano wakati wa kupitisha wagombea lakini safari hii wamekubaliana.
Kambaya anasema ingawa baadhi ya maeneo viongozi wa ngazi za chini walishindwa kufikia maridhiano ya kusimamisha mgombea mmoja, lakini kwa maeneo mengi wagombea wamesimamishwa na hivyo wananchi kuwa na imani na Ukawa na kuwapa ushindi.

Mchakato wa katiba mpya.
Viongozi hawa wa Chadema na CUF, kila mmoja anasema mchakato wa Katiba Mpya na msimamo wa Ukawa kutetea maoni ya wananchi umekuwa na manufaa makubwa kwao.
Kambaya anasema wananchi wameelewa dhamira ya dhati ya Ukawa kuhakikisha taifa linakuwa na Katiba ambayo inatokana na maoni yao na siyo maoni ya CCM. Kwa upande wake Mnyika anasema, suala la katiba limewanufaisha kwani wananchi wameamini kuwa Ukawa ndiyo tegemeo lao kwa sasa baada ya kutoa maoni yao lakini CCM wamepinga.
Vita dhidi ya ufisadi na utetezi wa rasilimali.
Mnyika anasema, vita dhidi ya ufisadi iliyoanza mwaka 2005 pale Dk Wilbroad Slaa alipotangaza orodha ya mafisadi imeendelea hadi sasa “kuanzia bungeni hadi kwenye mikutano yetu tumekuwa tukiibua ufisadi na kusimamia wachukuliwe hatua wahusika jambo ambalo limesaidia sana kuwaonyesha wananchi nini malengo yetu,” anasema, “michango yetu kutaka rasilimali za nchi kunufaisha Watanzania kama madini, mafuta, ardhi, gesi na mengine mengi imekuwa siri kubwa ya ushindi wetu.”

Sakata la Escrow.
Kambaya anasema sakata la wizi wa zaidi ya Sh306 bilioni katika akauti ya Tegeta Escrow, limeongeza mori ya wananchi kuwaunga mkono Ukawa. Kambaya anasema suala hili ingawa Serikali ya CCM inalipuuza lakini limeibua dhana kubwa ya kutaka uwajibikaji kwa wahusika kama Ukawa unavyotaka. “suala hili limetunufaisha sana Ukawa kwani wananchi sasa wamechoshwa na ufisadi unaofanywa na watendaji wa Serikali ya CCM,” anasema.

Kero za wananchi
Mnyika anasema kukithiri kwa Kero za wananchi vijijini kama uhaba wa maji, huduma za afya, umasikini, matatizo ya elimu yamewafanya kuichoka CCM. Anasema viongozi wa CCM wamekuwa wakiahidi mambo mengi lakini wameshindwa kuyatekeleza hasa yale ambayo yanagusa wananchi masikini. Mnyika anasema CCM kutotimiza ahadi zao, kumewafanya wananchi kutowaamini wagombea wao hadi ngazi za chini na hivyo, kuwapigia kura Ukawa.

Wagombea wanaokubalika.
Mnyika anasema katika maeneo mengi wagombea waliotokana na Ukawa walikuwa wanakubalika baada ya kupitia michujo mingi. “Kwa mfano sisi Chadema tulikuwa na wagombea, CUF walikuwepo na NCCR- Mageuzi lakini kutokana na kukubaliana kuwa na mgombea mmoja, walichujwa hadi kupatikana mmoja anayekubalika,” anasema. Anasema mchujo huo, ulisababisha maeneo mengi Ukawa kuwa na wagombea ambao ni chaguo la wananchi, ingawa wengi waliwekewa mapingamizi na kuondolewa.

Vyombo vya habari.
Kambaya anasema ushindi wa Ukawa hauwezi kuvitenga vyombo vya habari kutokana na kuibua kwa kutangaza mambo mengi ambayo ni kero katika jamii bila woga yaliyokuwa yakiibuliwa na viongozi wa vyama vinavyotokana na Ukawa. Anasema pia vyombo vya habari tangu kutangazwa muungano wa Ukawa, vimeonyesha kuwaunga mkono kwa kutetea umoja na kupingana kutengana. “kwa niaba ya Ukawa tunavishukuru sana vyombo vya habari kwa kuwa mstari wa mbele kwanza kufichua maovu katika jamii na pia kukemea kutengana Ukawa wakati wote,” anasema Kambaya. Anasema kufafanuliwa kwa kashfa nyingi ambazo zinatafuna fedha za umma kama sakata la wizi wa fedha za Escrow kumefanya wananchi kuwa na imani na upinzani kama watetezi wao. Hata hivyo, viongozi hawa kwa pamoja wanakiri kuwa ushindi wa Ukawa haukuwa rahisi katika uchaguzi huu.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: