Social Icons

Pages

Wednesday, December 17, 2014

SPIKA BUNGE LA EALA KIKAANGONI LEO ARUSHA

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Dk Margret Zziwa akisikiliza uamuzi wa jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) wakati wa kesi yake Arusha jana.

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Dk Margret Zziwa huenda akang’olewa kwenye nafasi yake katika kikao cha dharura cha Bunge hilo kinachofanyika jijini Arusha leo.
Bunge hilo linakutana leo baada ya Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), kutupilia mbali maombi ya Spika Zziwa ya zuio la muda dhidi ya kikao hicho kinachotarajiwa kupokea, kujadili na kuamua taarifa ya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Spika kutoka Kamati ya Sheria, Kanuni na Madaraka ya Bunge.
Jopo la majaji watano wa EACJ, chini ya Jaji Kiongozi, Jean Bosco-Butasi, lilitupa maombi hayo baada ya Spika Zziwa kupitia kwa wakili wake, Jet Tumwebaze kushindwa kuishawishi mahakama kuhusu madhara atakayopata iwapo kikao hicho kingefanyika.
Katika maombi yake, Spika Zziwa licha ya kudai hoja ya kumwondoa madarakani inakiuka Katiba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya Bunge kumteua Chris Okumu kuwa kaimu spika, cheo ambacho hakipo kwenye Katiba. Spika huyo pia anadai kikao cha leo hakiko kwenye kalenda ya vikao vya Eala na kwamba, amekuwa mtumishi wa umma kwa muda wa zaidi ya miaka 14, hivyo kitendo cha kumwondoa madarakani kitamshushia hadhi na kumletea madhara yasiyolipika.
Akisoma uamuzi wa Mahakama kwa niaba ya majaji wenzake, Jaji Isaac Lenaola kutoka Kenya alisema kifungu cha 53(3) cha Mkataba wa EAC, kimeweka utaratibu wa wabunge kumwondoa madarakani spika wao na mahakama kama moja ya mihimili, haiwezi kuingilia suala hilo.
“Ni jukumu la mlalamikaji kuthibitisha kuwa madhara atakayopata hayawezi kurekebishika katika shauri hili, lakini mlalamikaji ameshindwa kuishawishi mahakama. Mahakama inajielekeza kuwa madhara atakayopata mlalamikaji iwapo ataondolewa, yanaweza kulipika kwa fedha kutegemeana na shauri alilolifungua mahakamani,” alisema Jaji Lenaola. Majaji wengine waliosikiliza ombi hilo ni Fakihi Jundu (Tanzania), Monica Mugenyi (Uganda) na Faustin Ntezilyayo (Burundi). Jopo la majaji hao pia limepanga kusikiliza ombi la msingi kwenye keshi hiyo Februari 3, mwakani.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: