Wizara ya Afya, na
Ustawi wa Jamii, itaanza kutumia mfumo mpya wa utoaji wa taarifa za
magonjwa ya mlipuko kwa kutumia simu za mkononi kwa lengo la kuyadhibiti
mara yanapogundulika kabla ya kusababisha madhara makubwa.
Naibu katibu mkuu wa Tamisemi, Dk Deo Mtasiwa
alisema hayo jana katika mkutano ulioshirikisha wataalamu wa magonjwa ya
binadamu na wanyama pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(Tehama) ili kuangalia njia itakayotumika kurahisisha upatikanaji wa
taarifa hizo.
Alisema mfumo wa kushughulikia magonjwa ya mlipuko
ya kuambukiza kwa binadamu na wanyama katika nchi za Afrika bado ni
hafifu na kuwapo kwa mfumo huo wa kutumia mawasiliano ya simu kutoka kwa
wagonjwa kwenda kwa wataalamu kutarahisisha udhibiti wa magonjwa hayo
kwa haraka.
Alisema kitendo cha wataalamu wa Afrika kupitisha uamuzi wa kutumia teknolojia hiyo, kutasaidia kupiga hatua.
na kuwa mfano wa kuigwa.
“kwa kweli sisi kama Serikali kupitia Wizara ya
Afya, mfumo huu tunautumia katika kipengele cha matokeo makubwa sasa
(BRN) katika kuuboresha na kuufanyia kazi kwa ngazi ya kimataifa ili
Tanzania katika nchi za Afrika uwe ndiyo mfano wa kuigwa na nchi zingine
kwa kufanya vizuri kupitia mfumo huu,” alisema Dk Mtasiwa.
Mtafiti kutoka SACIDS, Profesa Esron Karimuribo
alisema kwa pamoja wameweza kukutana na wataalamu hao ili kuangalia njia
itakayotumika kurahisisha upatikanaji wa taarifa hizo zitakazosaidia
kuzuia vifo vinavyotokea pindi magonjwa hayo yanapozuka.
Alisema kupitia mfumo huo wa mawasiliano, taarifa
za magonjwa hayo zitaifikia Serikali na wataalamu wake kwa haraka ili
wachukue tahadhari kabla ya kuleta madhara kwa jamii.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine, Kadeghe
Fue alisema kabla ya kuwapo kwa mfumo huo, taarifa zilikuwa zikichelewa
kuwafikia wataalamu kwa kuwa walikuwa wakitumia makaratasi na sasa kwa
kutumia teknolojia ya mawasiliano ya simu za mkononi itaharakisha
upatikanaji wa taarifa hizo na zitasambaa kwa wakati.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment