Kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na kampuni ya kufua
umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na wenzake wawili
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya Waziri Mkuu na wenzake
watatu, jana ilishindwa kuanza kusikilizwa kama ilivyokuwa imepangwa
awali na hivyo kuahirishwa hadi Desemba 31, mwaka huu.
Kushindikana kwa kesi hiyo kuanza kusikilizwa jana, kulitokana na upande
wa serikali kuiomba mahakama muda wa kutosha ili ipate fursa ya kupitia
nyaraka za kesi hiyo.
Wadai wengine katika kesi hiyo namba 59 ya mwaka 2014, ni kampuni ya Pan
Power Solution Tanzania (PAP) na mmiliki wake, Harbinder Singh Sethi,
huku wadaiwa wengine wakiwa ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
Tanzania (Takukuru), Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG).Uamuzi wa kuahirisha kesi hiyo ulitolewa na Jopo la majaji watatu; Augustine Mwarija, Gadi Mjemmas na Stella Mugasha, baada ya kusikiliza ombi la upande wa utetezi, wakiiomba mahakama iwape muda wa siku moja kupitia maelezo ya mashtaka hayo ili wawasilishe utetezi wake.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, akisaidiwa na Wakili wa Serikali Gabriel, aliiambia mahakama kuwa juzi (Jumatatu) saa 5:00 asubuhi, walipokea nyaraka za kesi hiyo, lakini hawakupata muda wa kuzisoma kwa sababu ya wingi wa majalada hayo. Jopo la mawakili wa upande wa mashitaka wakiongozwa na Wakili Joseph Makendege, Melchisedeck Lutema na Gabriel Munyele ulikubaliana na ombi hilo.
Wadai katika kesi hiyo wanaiomba mahakama itoe amri ya kuzuia utekelezaji wa maazimio nane ya Bunge kuhusu kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya shilingi, uliofanywa katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT). IPTL, PAP na Sethi, walifungua kesi hiyo Desemba 18, mwaka huu, chini ya hati ya dharura kupitia kampuni za mawakili ya Bulwark, Asyla na Marando and Mnyele.
Katika hati ya madai iliyowasilishwa katika mahakama hiyo, wadai wanapinga maazimio ya Bunge kutekelezwa wakidai kwamba kilichofanyika bungeni ni kinyume cha Katiba ya nchi. Wanadai maazimio hayo yanalenga kugombanisha mihimili mitatu ya dola na kwamba, yaliegemea upande mmoja. Pia wanadai kwamba kuna kesi mbalimbali zinazoendelea mahakamani zinazohusiana na sakata la fedha hizo. Vile vile, wanadai Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alifanya ukaguzi, pia Takukuru ilifanya uchunguzi, hatimaye taarifa ya CAG ikajadiliwa bungeni. Wanadai mjadala huo ulisababisha Bunge kufikia maazimio hayo.
Wadai hao wanadai kitendo hicho kilipuuza amri ya Mahakama Kuu kwa kufuata tafsiri potofu iliyotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria kuhusu amri iliyozuia mjadala wa akaunti hiyo kufanyika bungeni. Kutokana na sababu hizo, wanaiomba mahakama izuie utekelezwaji wa maazimio ya Bunge. Pia itangaze maazimio hayo yaliyofikiwa Novemba 29, mwaka huu na maamuzi ya Spika wa Bunge kuyakubali, kuwa ni kinyume cha Katiba ya nchi.
MAAZIMIO YA BUNGE
Azimio la kwanza lililofikiwa na Bunge linataka Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua stahiki za kisheria watu wote waliotajwa na taarifa maalumu ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (CAG) kuhusika na kashfa hiyo na watu wengine watakaogundulika kuhusika kufuatia uchunguzi mbali mbali unaoendelea.
La pili linataka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka; aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema; Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao. Wengine waliotajwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusika katika kashfa hiyo ni Sethi na mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira.
Azimio la tatu linataka kamati za kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka kabla ya mkutano wa 18 wa Bunge, kuwavua nyadhifa wenyeviti wa kamati za Bunge; Andrew Chenge (Bajeti), Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini) na William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala).
La nne linataka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Azimio la tano linataka mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi
kuitaja Benki ya Stanbic Bank (Tanzania) Ltd na benki nyingine yoyote
itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi,
kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti hiyo,
kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
La sita linataka serikali iandae na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyoiunda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Azimio la saba linataka serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo.
Na azimio la nane linataka serikali itekeleze azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti na serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme.
La sita linataka serikali iandae na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyoiunda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Azimio la saba linataka serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo.
Na azimio la nane linataka serikali itekeleze azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti na serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment