Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda amesema Serikali imeamua kutafuta soko la utalii kutoka
nchi za Ghuba na Mashariki ya Kati ili kuongeza idadi ya watalii nchini
na kukuza pato la Taifa kupitia sekta hiyo.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo
inasema Pinda ametoa rasi hiyo alipofungua Kongamano la siku mbili la
Utalii na Uwekezaji lilionza leo kwenye Hoteli ya Le Meridien, jijini
Dubai, Falme za Kiarabu.
“Tunao mkakati wa kukuza utalii nchini lakini
wengi wamekuwa wakitoka Ulaya na Marekani. Eneo ambalo tumeona tuwekeze
kwa nguvu kwa maana ya kuongeza idadi ya watalii ni hili la nchi za
Ghuba na Mashariki ya Kati,” alisema.
Waziri Mkuu alisema kimahusiano Tanzania iko
karibu na nchi hizo za ghuba lakini pia wanao uwezo wa kifedha wa
kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ya utalii.
Alitoa wito kwa makampuni yanayotaka kuwekeza
nchini yaangalie fursa zilizopo kwenye ujenzi wa hoteli za kawaida,
hoteli za mahema (tented camps) na hoteli zenye kutoa huduma za vyakula
(special cuisine restaurant).
Hata hivyo, Pinda aliwataka wawekezaji watakaokuja
wafanye juhudi ya kushirikiana na Watanzania wazawa ili nao wajione ni
sehemu ya uwekezaji huo.
Mapema, akifungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema
katika kipindi cha miaka mitano, Tanzania imeweza kuongeza idadi ya
watalii kutoka 714,367 mwaka 2009 hadi kufikia watalii 1,095,884 kwa
mwaka 2013.
“Kiwango cha mapato ya watalii hao kiliongezeka
kutoka dola za Marekani bilioni 1.2 hadi kufikia dola za Marekani
bilioni 1.8 katika kipindi hicho hicho cha miaka mitano,” alisema na
kuongeza kuwa sekta hiyo inaajiri watu zaidi ya 400,000 kuchangia
asilimia 17 kwenye pato la Taifa.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu akizungumza na washiriki wa kongamano hilo alisema Tanzania ni
nchi ya pili duniani kwa kuhifadhi rasilmali zake na kuzitumia kwa
utalii.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment