Afisa mmoja katika tumu ya uokozi inayoendelea kuitafuta ndege ya Air Asia. Ndege iliotoweka ya shirika la ndege ya Air Asia iliokuwa na abiria 162
huenda ikawa chini ya bahari huku nchi za Asia zikituma ndege na meli
katika juhudi za kuendelea kuitafuta ndege hiyo.
Ndege hiyo ya Airbus chapa A320-200 inayomilikiwa na shirika la Air Asia
la Indonesia ilitoweka baada ya rubani wake kushindwa kupata ruhusa ya
kupaa juu zaidi kutokana na hali mbaya ya hewa, wakati ilipokuwa angani
ikitokea mji wa Surabaya nchini Indonesia na kuelekea Singapore siku ya
jumapili.
Maafisa wanasema Ndege hiyo yenye nambari ya usajili QZ8501 haikutuma
mawasiliano yoyote ya kuwa na matatizo, ilitoweka tu katika eneo la
bahari ya Java dakika tano baada ya kuomba kubadili njia ili kukwepa
hali mbaya ya hewa, lakini ombi hilo lilikataliwa kutokana na msongamano
wa ndege angani.
Hata hivyo timu ya uokozi inaendelea kuitafuta ndege hiyo
katika kisiwa cha Belitung mahali ambapo ndege hiyo inaaminika kuanguka.
Mkuu wa oparesheni hiyo Joni Superiadi amesema kwa sasa hawajafanikiwa
kupata mabaki ya ndege hiyo lakini bado oparesheni zinaendelea.
"Hadi wakati huu bado tunaendelea na shughuli za kuitafuta ndege hiyo
iliopoteza mawasiliano, kwa sasa tunaelekea katika kisiwa cha Nangka.
Boti nyengine za uokozi pia zinaendelea na shughuli hii ya kutafuta
ndege hiyo katika maeneo mengine yalioko karibu, lakini mpaka sasa bado
hatujapata mabaki yoyote ya ndege hiyo," alisema Mkuu wa oparesheni hiyo
Joni Superiadi.
Raia wengi waliokuwa katika ndege iliotoweka wanatokea Indonesia
Ndege hiyo iliotoweka siku ya Jumapili ilikuwa na abiria 155 kutoka
Indonesia, Raia watatu wa Korea Kusini, raia mmoja kutoka Singapore,
Mmalasia mmoja na Muingereza mmoja, huku rubani msaidizi wa ndege hiyo
akitokea nchini Ufaransa. Kutoweka kwa ndege hii kunaufanya mwaka huu wa 2014 kuwa mwaka
mbaya uliokumbwa na majanga makubwa ya ndege kwa mashirika ya ndege
yaliona ushirika na mashirika ya ndege ya Malaysia.
Awali ndege ya Malasia MH370 ilitoweka tarehe 8 mwezi Machi ilipokuwa
inatokea Kuala Lumpur kuelekea mjini Beijing, ndege hiyo ilikuwa na
abiria 239 pamoja na wafanyakazi wa ndege, mpaka leo haijafanikiwa
kupatikana. Janga jengine lilitokea tarehe 17 mwezi wa Julai ndege ya shirika hilo
hilo la Malaysia ilipodunguliwa ikiwa angani nchini Ukraine na
kusababisha mauaji ya abiria wote 298 waliokuwa ndani.
Makundi ya ndege za Air Asia wakiwemo washirika wake kutoka Thailand,
Ufilipino na India, hawajakuwa na majanga yoyote tangu ndege shirika
hilo lilipoanzishwa mwaka wa 2002. Hata hivyo hisa za kundi hilo mjini
Kuala Lumpur zimeshuka kwa asilimia nane kuanzia mapema leo asubuhi.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment