Aina ya mbu anayesababisha malaria
Juhudi za kukabiliana na ugonjwa hatari wa Ebola kwenye eneo la Afrika
Magharibi, zimekwamisha kampeni dhidi ya Malaria ambao unazuilika na
kutibika, lakini umesababisha vifo vya maelfu ya watu kuliko hata Ebola.
Imeelezwa kuwa madaktari katika eneo la Gueckedou nchini Guinea
ambako ugonjwa wa Ebola ulianzia, waliacha kuchukua vipimo vya malaria.
Kiwango cha kuuripoti ugonjwa wa malaria kilishuka kwa asilimia 40
nchini Guinea, hatua ambayo Mkurugenzi Msaidizi wa mpango wa rais wa
Marekani wa kupambana na malaria, Dokta Bernard Nahlen, anasema siyo
nzuri.
Amesema kushuka kwa kiwango cha kuripoti visa vya malaria, kunatokana
na watu kuogopa kwenda kwenye vituo vya afya, hivyo hawapati matibabu
ya malaria. Takwimu zinaonyesha kuwa nchini Guinea, nusu ya watu milioni
12 hawana uwezo wa kupata huduma za afya na wanafariki bila ya
kuhesabiwa.
Kiasi Waguinea 15,000 walikufa kwa malaria mwaka uliopita, 14,000
wakiwa ni watoto wenye chini ya umri wa miaka mitano. Kwa mujibu wa
takwimu za Shirika la Afya Duniani-WHO, kiasi watu 1,600 wamekufa
kutokana na ugonjwa wa Ebola nchini Guinea.
Shirika la Nets for Life lenye makao yake mjini New York, ambalo
limekuwa likitoa msaada wa vyandarua vilivyowekewa dawa ya kuuwa mbu,
limesema malaria ni chanzo cha vifo vya watoto wenye chini ya umri wa
miaka mitano nchini Guinea na baada ya ugonjwa wa Ukimwi ambao ni chanzo
cha vifo vya watu wazima.
Dalili za Ebola na malaria zinafanana
Ebola na malaria zina dalili sawa ikiwemo homa, kizunguzungu
pamoja na maumivu ya kichwa na misuli. Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa
asilimia 24 ya watu wa Gueckedou waliopimwa homa mwezi Oktoba walikutwa
na Ebola pamoja na malaria na asilimia 33 kati yao ambao hawakuwa na
Ebola, walikuwa na malaria.
Ugonjwa wa malaria umewaua madaktari 38 wa Cuba waliopelekwa Guinea
kusaidia katika mapambano dhidi ya Ebola. Dokta Nahlen amesema shirika
lake linafanya utafiti wa kitaifa wa vituo vya afya na kwengineko ili
kubaini ni wapi watu wenye malaria wanakwenda kutibiwa.
Anasema kwenye nchi jirani ya Liberia, serikali ilisitisha mpango wa
kugawa vyandarua milioni 2. Nako Sierra Leone, nchi ambayo ilishika
nafasi ya tatu katika nchi zilizoathiriwa na Ebola, madaktari wasio na
mipaka, mwezi huu walichukua hatua isiyokuwa ya kawaida ya kugawa dawa
za kujikinga na kutibu malaria kwa watu milioni 1.5.
Patrick Robataille kutoka shirika la madaktari wasio na mipaka mjini
Freetown, anasema watu wamekuwa wakimiminika kwenye vituo vya kutibu
Ebola, wakidhani wameambukizwa ugonjwa huo, huku ukweli ikiwa ni kwamba
wameambukizwa malaria. Imeelezwa kuwa madaktari wamekuwa waoga wa
kuchukua sampuli ya damu kwa wagonjwa ili kuwapima malaria.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment