
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika mkutano wa wajasiriamali vijana, Lukuvi, alisema serikali inatambua changamoto zinazowakabili vijana katika kujikwamua kimaisha na kujikuta wakikwamishwa na mitaji, soko la uhakika, mazingira ya biashara na gharama za uzalishaji.
Alisema, serikali imechukua hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto hiyo kama kuanzisha mfuko wa vijana utakaotoa mikopo kwa masharti nafuu kwa vikundi vitakavyoundwa. Alisema itaishawishi Wizara ya Elimu kufundisha somo la ujasiriamali kuanzia shule za msingi na sekondari badala ya kubaki katika ngazi za vyuo vikuu.
“Katiba iliyopendekezwa baraza la vijana limewekwa, hivyo tumieni fursa hiyo kujadili masuala yenu muhimu ili yashughulikiwe bila kujali itikadi za siasa na dini, mwito wangu wekezeni katika somo la ujasiriamali ili mtumie ujuzi katika kujiajiri au kuajiri wengine,” alisema Lukuvi.
Aliwataka kujiepusha na matumizi ya madawa za kulevya kwa kuwa yanachochea upatikanaji wa magonjwa ya afya ya akili, kudhoofika afya, homa ya ini, kifua kikuu, na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Rais wa kampuni ya Gilgal ya Dar es Salaam, ambayo ndiyo iliyoandaa mkutano huo, Peter Christopher, aliwashauri vijana badala ya kuendelea kutegemea ajira kwa serikali waangalie njia ya kuzingatia somo la ujasiriamali linalofundishwa vyuoni kama ajira ya kwanza kwao.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment