Wapiganaji wa Al-Shabaab nchini Somalia
Kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab nchini Somalia, Zakariyah
Ismail Ahmend Hersi, amekamatwa na polisi baada ya kujisalimisha jana
Jumamosi.
Afisa mmoja wa idara ya ujasusi amesema Hersi alijisalimisha kwa
polisi katika mkoa wa Gedo, baada ya kile kinachoonekana ni uwezekano wa
kuzuka mzozo ndani ya kundi hilo.
Huenda Hersi anatofautiana na wapiganaji watiifu kwa kiongozi wa
Al-Shabaab, hayati Abdi Godane, aliyeuawa katika shambulio la anga
lililofanywa na Marekani mwanzoni mwa mwaka huu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, afisa wa kijeshi wa ukanda
huo, Jama Muse, amesema Hersi alikuwa anasimamia masuala ya kijasusi na
fedha na pia alikuwa ni mmoja kati ya makamanda waandamizi wa
Al-Shabaab.
Ingawa jeshi la Somalia lilimuweka katika orodha ya mawakala wa
Al-Shabaab, haijafahamika wazi iwapo Hersi bado alikuwa ana nguvu ndani
ya kundi hilo la kigaidi katika miezi michache iliyopita. Inawezekana
kuwa Hersi alikuwa miongoni mwa kundi la makamanda waliotofautiana na
Godane kabla ya kifo chake.
Marekani iliahidi Dola milioni 3
Marekani iliahidi kutoa zawadi ya Dola milioni tatu ambazo ni sawa na
Euro milioni 2.14, kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kiongozi huyo.
Hata hivyo, wizara ya mambo ya nje haijazungumza chochote kuhusu taarifa
hizo. Kundi la Al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa
Al-Qaeda, limeendelea kuwa tishio nchini Somalia na Afrika Mashariki.
Kundi hilo limefanya mashambulizi kadhaa ya kigaidi nchini Somalia na
katika nchi jirani, ikiwemo Kenya, ambayo wanajeshi wake ni sehemu ya
kikosi cha Umoja wa Afrika kinachokisaidia kikosi cha Somalia
kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Siku ya Alhamisi ambayo ilikuwa ni sikukuu ya Krismasi, kundi
la Al-Shabaab lilifanya mashambulizi katika kambi ya kikosi cha Umoja wa
Afrika-AMISOM kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na kuwaua watu 14,
wakiwemo wapiganaji wote wanane wa kundi hilo.
Kundi hilo limekiri kuhusika na shambulio hilo ambalo lilikuwa la
kulipiza kisasi kutokana na mauaji ya Godane, na kuharibu pia nyumba za
maafisa wa Umoja wa Mataifa na balozi za mataifa ya Magharibi. Msemaji
wa Al-Shabaab, Sheikh Mohamud Rage, alikiambia kituo cha redio cha
Andalus, kinachowaunga mkono wapiganaji hao, kuwa hilo lilikuwa
shambulio la kulipiza kisasi.
Al-Shabaab ilikuwa ikiidhibiti sehemu kubwa ya mji wa Mogadishu
wakati wa miaka ya 2007 hadi 2011, lakini vikosi vya Umoja wa Afrika,
vililifurumusha kundi hilo nje ya mji mkuu huo na miji mingine mikubwa.
Marekani na Umoja wa Mataifa zimeonya kuwa mapigano ya kisiasa nchini
Somalia yanaiweka hatarini hali ya usalama nchini humo. Serikali ya shirikisho bado haina nguvu na ina uwezo mdogo sana nje ya mji mkuu, Mogadishu.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment