Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry anaendelea na juhudi
zake za kuufufua utaratibu wa amani ya Mashariki ya kati. Baada ya
kuonana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini
Rome, amepangiwa kukutana na Saeb Erakat mjini
London.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani aliyewasili London jana usiku
ataonana pia na katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu Nabil El
Arabi. Waziri Kerry anaendeleza mazungumzo barani Ulaya kwa lengo la kujaribu
kufufua utaratibu wa amani kati ya Israel na Palestina.Baada ya
mazungumzo yake jumapili iliyopita pamoja na waziri mwenzake wa Urusi
Sergei Lavrov,alikutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa
muda wa masaa karibu matatu mjini Roma.
"Wanasiasa hao wawili walikuwa na mazungumzo ya muda mrefu na ya kina
kuhusu usalama wa Israel na matukio katika Umoja wa mataifa"duru ya
wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imesema.
Baadae jana usiku waziri Kerry akakutana na mawaziri wenzake wa Ufaransa
Laurent Fabius,wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na wa Uengereza
Philip Hammond katika uwanja wa ndege wa Orly mjini Paris.
"Tumesema wazi kabisa wakati wa mazungumzo pamoja na washirika wetu,kuna
baadhi ya mambo hatuwezi kamwe kuyatetea" amesema afisa mmoja wa wizara
ya mambo ya nchi za nje ya Marekani mwishoni mwa mazungumzo
hayo,akimaanisha Marekani haiko tayari kuridhia madai ya wapalastina.
Wapalastina wameelezea azma yao ya kuwasilisha hapo kesho kupitia
mwakilishi wa Jordan,mswaada wa azimio mbele ya baraza la usalama la
Umoja wa mataifa ili kudai Israel ikome kukalia ardhi zao mnamo muda wa
miaka miwili inayokuja.
Ufaransa inasaka Azimio la Maridhiano
Ufaransa pia tangu wiki kadhaa sasa imeanzisha mashauriano
pamoja na London na Berlin na baadae na Washington na Amman ili kuandaa
hati ya maridhiano ambayo hailingani na ile ya wapalastina na ambayo
ingeweza kuungwa mkono na wanachama wote 15 wa baraza la Usalama.
"Paris inasaka ufumbuzi wa pamoja katika juhudi za kidiplomasia
zlizoanzishwa na umoja wa Mataifa kuhusu mzozo kati ya Israel na
Palestina" amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent
Fabius,muda mfupi kabla ya kukutana na mawaziri wenzake. "Ikiwa wapalastina watawasilisha mswaada wao wa azimio,wamarekani
wameshasema watatumia kura yao ya turufu kuupinga.Kwa hivyo kwa upande
mmoja mswaada huo wa azimio hautaweza kukubaliwa na kwa upande wa pili
kuna jibu litakalofuatia kutoka upande wa wapalastina.Sisi
tunachotaka,ni kufikia ufumbuzi wa pamoja."ameeleza waziri wa mambo ya
nchi za nje wa Ufaransa. Pendekezo la Ufaransa linazungumzia juu ya kuanzishwa haraka mazungumzo
ya amani kati ya Israel na Palestina kwa misingi muhimu kama vile kuishi
pamoja kwa amani dola ya Israel na dola ya Palestina lakini bila ya
kuwekwa muda kwa Israel kuyahama maeneo inayoyakalia ya wapalastina.
Wamarekani wanaliangalia kwa jicho la tahadhari pendekezo hilo la Ufaransa.
Netanyahu azikosoa nchi za Ulaya kuelemea upande wa Wapalastina
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa amepangiwa pia
kukutana mjini Paris na katibu mkuu wa jumuia ya nchi za kiarabu Nabil
Al Arabi na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Palastina Riyad Al-Malki.
Waziri mkuu wa Israel anaepinga hatua yoyote ya kupewa muda wa kuyahama
maeneo ya wapalastina amezituhumu nchi za Ulaya kuwapendelea
wapalastina."Ninavutiwa sana na juhudi za waziri wa mambo ya nchi za nje
wa Marekani za kuepusha hali isizidi kuwa mbaya" amesema.Na kuongeza
tunanukuu:"juhudi za wapalestina na nchi kadhaa za Ulaya za kuilazimisha
Israel na kuipa masharti zitapelekea hali kuzidi kuwa mbaya na
kuitumbukiza Israel katika hali ya hatari."
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment