Rais Jakaya
Kikwete jana alikagua gwaride la Uhuru la vikosi vya ulinzi na usalama
ambavyo baadaye vilipita mbele yake kutoa heshima ikiwa ni maadhimisho
ya miaka 53 ya Uhuru wa Tanganyika.
Ikiwa hakutakuwa na mabadiliko yoyote, kiongozi
huyo wa awamu ya nne wa Tanzania, anatazamiwa kustaafu kikatiba mwakani
kabla ya sherehe nyingine za Uhuru Desemba 9, 2015.
Kwa kawaida uchaguzi mkuu hufanyika wikiendi ya
mwisho ya Oktoba na matokeo hutangazwa siku chache baadaye. Kwa maana
hiyo, hilo lilikuwa gwaride la mwisho la sherehe za Uhuru kwake akiwa
mkuu wa nchi.
Mbali na hilo, wakati Rais Kikwete akifanya
shughuli hiyo, macho ya Watanzania yalikuwa yameelekezwa kwake kuona
jinsi anavyotekeleza jukumu hilo siku ya pili tu baada ya kutoka katika
mapumziko ya upasuaji wa saratani ya tezi dume huko Marekani Novemba 8.
Kabla ya tukio hilo lililofanyika Uwanja wa Uhuru,
juzi Rais Kikwete alionekana katika picha akifanya mazoezi mepesi siku
10 tu baada kurejea nchini akitokea Hospitali ya Johns Hopkins,
Baltimore alikotibiwa.
Jana, Rais Kikwete alidhihirisha kuimarika kiafya
baada ya kumudu kukagua gwaride hilo na baadaye mchana akasimama kwa
muda mrefu akitoa nishani za heshima kwa watu mbalimbali waliolitumikia
Taifa.Rais, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu alitembea kwa mwendo wa
ukakamavu akiwa ameongozana na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis
Mwamunyange kukagua gwaride hilo.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi walisikika wakimshukuru Mungu kwa jinsi alivyosaidia afya ya Rais kuimarika.
“Jamani kweli Rais Kikwete sasa yupo poa anatembea kwa mwendo wa ushupavu haswaa,” alisema mkazi wa Kinondoni Juma Ramadhani.
Rais Kikwete pia alisimama kwa muda mrefu kupokea salamu za kijeshi kutoka kwa gwaride hilo.
Sherehe zafana
Rais Kikwete aliingia kwenye Uwanja wa Uhuru saa
5.08 asubuhi akiwa katika gari la wazi huku akiwa ameambatana na
Jenerali Mwamunyange.
Wakati akiingia, Kikwete alikuwa akitabasamu na
kuwapungia mikono wananchi waliofika kwenye uwanja huo ambao walijibu
kwa kumshangilia.
Akiwa amevalia suti nyeusi, shati jeupe na tai nyekundu, Rais
Kikwete alikagua gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama ambavyo ni,
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Magereza, Polisi, Wanamaji, FFU na
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Baada ya ukaguzi huo, vikosi hivyo vilipita kwa
mwendo wa pole na wa haraka kutoa heshima kwake. Kivutio kikubwa
kilikuwa kwa kikosi cha FFU ambacho askari wake walionyesha ukakamavu wa
hali ya juu walipokuwa wakipita kutoa heshima zao kwa Rais na kuibua
shangwe na hoihoi kutoka wa wananchi waliokuwa wamefurika uwanjani hapo.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na Rais wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk Ali Mohamed Shein, makamu wake wa
Kwanza, Maalim Seif Shariff Hamad, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Makamu
wa Pili wa SMZ, Balozi Seif Ali Idd.
Wengine waliohudhuria ni Rais Mstaafu wa Awamu ya
Pili, Ali Hassan Mwinyi na mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa,
Cleopa Msuya na Frederick Sumaye.
Sherehe hizo zenye kaulimbiu; “Miaka 53 ya Uhuru;
ingia katika historia ya nchi yetu jitokeze kuipigia kura Katiba
Inayopendekezwa,” ilitumbuizwa na halaiki ya watoto 1,500 wa shule za
msingi ambao walionyesha maumbo mbalimbali, kucheza sarakasi na kuimba.
Mbali na maonyesho mengine, watoto hao
walipeperusha njiwa 25 angani ikiwa ni ishara ya kuonyesha kuwa Tanzania
ni nchi ya amani.
Pia vikundi vya ngoma za asili kutoka Kasulu, Kigoma na Kyela, Mbeya vilitumbuza.
Viongozi wakosekana
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal alikuwa
miongoni mwa baadhi ya viongozi walikosekana katika sherehe hizo,
wengine wakiwa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa na mawaziri wakuu wastaafu,
Jaji Joseph Warioba, Salim Ahmed Salim na John Malecela.
Pia viongozi wa vyama vya siasa akiwamo Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba,
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa TLP, Augustine
Mrema hawakuhudhuria.
Alipoulizwa, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi
ya Upinzani Bungeni alijibu kwa kifupi kwamba yuko Ujerumani na
angetaka apigiwe simu baadaye. Simu za Mbatia na Lipumba ziliita bila
kupokewa huku Mrema akiwa hapatikani kwenye simu yake.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment