Muziki wa Bongo Fleva unazidi kubadilika kila
kukicha, zile zama za kufanya muziki wa ‘play back’ unaanza kupotea
taratibu na sasa imefika wakati wa kupiga laivu ambapo kwa staa wa
muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ atalifanya hilo
Sikukuu ya Krismasi mwaka huu ndani ya Dar Live, Mbagala-Zakhem jijini
Dar.
Katika mahojiano yake na gazeti hili Diamond
alizungumza mengi kuhusiana na muziki wake ambapo hakusita kueleza
dhamira yake ya kuubadilisha muziki wake na kuwa ‘live’. Katika makala haya Diamond anafunguka nyuma ya pazia kuhusiana na maisha ya muziki wake wa sasa.
Changamoto
Miongoni mwa changamoto alizowahi kukutana nazo Diamond tangu afanikiwe kufanya muziki na wanamuziki wa kimataifa ni lugha. Diamond anakiri kuwa Kiingereza ilikuwa changamoto
kubwa sana kwake na amewasihi sana wanamuziki kutoka Bongo hasa
wanaojitanua kimataifa kulifanyia kazi suala la lugha kwani ni muhimu
sana. Changamoto nyingine ambayo amekumbana nayo ni
kutokana na suala zima la kutengeneza video. Alikuwa akihitaji kampuni
kubwa ya kutengeneza video ya ‘Mdogomdogo’ lakini kila kampuni aliyokuwa
akikutana nayo walikuwa wakimpigia hesabu kubwa huku wengine
wakimwambia inahitaji kutafuta hekalu kubwa, kijiji kizima jambo ambalo
kwake lilikuwa si rahisi.
“Kwa mara ya kwanza nilikutana na Kampuni ya The
God Father nchini Afrika Kusini ambapo tulikuwa wasanii kama 19 katika
kutengeneza video ya Wimbo wa Cocoa na Chocolate ambao ulikuwa
ukihamasisha kilimo kwa vijana na kuwa kilimo kinalipa.
Tukiwa katika kuchukua vipande vya video sikuwa na
wazo kufanya kazi na kampuni hiyo lakini mmoja wa waandaaji wa kampuni
hiyo alinitaka kubaki baada ya kutengeneza wimbo huo. Kweli niliongea
naye na kusema wananikubali kwa jinsi ninavyoweza kujituma katika
utengenezaji wa video ndipo tukaanza rasmi kufahamiana nao kwa
kutengeneza nao video kama ‘Mdogomdogo’ na ‘Nitampata Wapi’ na
nyinginezo.
Usiku wa Historia
Katika usiku unaotambulika kama Usiku wa Wafalme
ambao unatarajiwa kufanyika ndani ya uwanja wa taifa wa Burudani, Dar
Live, Desemba 25, wiki ijayo. Diamond atapanda na kufanya bonge moja la
shoo la kihistoria. “Nahitaji kuonyesha Watanzania kwamba tunaweza
kufanya shoo kubwa hata kama tukiwa nyumbani kwetu. Mara nyingi shoo
zangu kubwa huwa zinatoka Dar Live na siku hiyo niwahakikishie kwamba
nitapiga live band nyimbo zote na pili nitakuwepo na wasanii wote
nilioshirikiana nao katika nyimbo zangu huku nikipiga nao hizo nyimbo
jukwaani. Mashabiki pia wategemee kuona madansa wangu wapya na niwaambie
pia nitapiga nyimbo zaidi ya 20 bila kupumzika.” Usiku huo pia utafunikwa na mkali wa muziki wa Pwani, Mfalme
Mzee Yusuf ambapo usiku huo atapanda jukwaani na kundi lake la Jahazi
Modern Taarab na kuimba nyimbo zao zote kali.
Kolabo na Wanigeria
Kuhusiana na Kolabo, hadi sasa Diamond anakiri
kufanya kolabo nyingi na Wanigeria wengi kuliko msanii yeyote nchini.
Miongoni mwa kolabo alizozifanya ni pamoja na wakali kama Tiwa Savage,
Yemi Alade, Waje, Bracket, KCEE, Davido na wengine wengi. “Niseme kuwa kwa sasa naangalia kolabo za nje ya
Nigeria baada ya kufanya nao nyingi. Nimeshapata ombi la kufanya kolabo
na msanii kutoka Cash Money Brothers, Mohombi Nzasi Moupondo ‘Mohombi’
ambaye amekuwa akivuma na ngoma zake za Bumpy Ride na Coconut Tree.”
Tuzo 3 za Channel O
Diamond amewapongeza mashabiki wake wote kwa kumpa
sapoti ya kupata tuzo tatu kwa mpigo kutoka kituo cha Channel O Afrika,
tuzo zijulikanazo kama Channel O Music Video Awards (Choamva). Kwa mara ya kwanza ndani ya Dar Live, Diamond
atatimba na tuzo hizo ikiwa ni kutoa shukrani kwa mashabiki wote
watakaofika usiku huo na wengi wakipata nafasi ya kupiga naye picha na
kuongea mawili-matatu.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment