Vigezo 13 vilivyowekwa na CCM 
katika Uchaguzi Mkuu wa 2005 kumpima mwanachama anayefaa kugombea urais,
 ndivyo vitakavyotumika kuwaengua makada wanaoendelea kujitokeza kuwania
 nafasi hiyo mwakani, imefahamika.
Vigezo hivyo vinaonekana kuwa kizingiti kwa baadhi
 ya makada wa chama hicho ambao tayari wametangaza na wengine wanaotajwa
 kutaka nafasi hiyo ya juu nchini, ukiachilia mbali mnyukano 
unaotarajiwa kutoka vyama vya upinzani vinavyoonekana kupata nguvu.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula 
amelithibitishia gazeti hili kwamba, “Sifa hizo 13 zilizotumika mwaka 
2005 na 2010 ndizo zitakazotumika pia mwaka 2015 na wala hakutakuwa na 
maboresho wala nyongeza ya aina yoyote.” Vigezo hivyo viliwekwa ili kuhakikisha chama hicho
 kinampata mgombea asiyetiliwa shaka juu ya vitendo vya uadilifu, mwenye
 uzoefu wa uongozi serikalini, atakayedumisha muungano, mwenye upeo wa 
masuala ya kimataifa, mtetezi wa wanyonge, asiyejilimbikizia mali na 
mwajibikaji, mambo ambayo hata hivyo, bado yameibua mjadala iwapo 
yanazingatiwa au la. Pia anayetakiwa lazima awe mwenye kuzitetea sera 
za CCM, anayekubalika na wananchi, asiye na hulka ya udikteta au 
ufashisti, mwenye uwezo wa kufanya uamuzi wa busara na kiwango cha elimu
 ya chuo kikuu au inayolingana nayo.
Licha ya vigezo hivyo, baadhi ya makada 
waliokwishajitokeza na wengine wanaotajwa wanaonekana dhahiri kukosa 
baadhi sifa hizo na wengine wako ‘kifungoni’ kwa miezi 12 baada ya 
kupewa onyo kali kwa kufanya kampeni mapema na kujihusisha na vitendo 
vinavyokiuka maadili ndani ya chama na jamii.
Vigogo wa CCM ambao wanatajwa kutaka kupewa ridhaa
 ya kupeperusha bendera ya chama hicho ambao iwapo watachukua fomu, 
watatazamwa kwa vigezo hivyo ni Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla, 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri Mkuu, Mizengo 
Pinda, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January 
Makamba ambao wamekwishatangaza kuwania nafasi hiyo.
Wengine ambao wanatajwa ingawa hawajatangaza nia 
hadharani ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Waziri Mkuu mstaafu,
 Frederick Sumaye; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; 
Bernard Membe; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu); 
Stephen Wasira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William 
Ngeleja.
Wachambuzi wanavyosema
Akizungumzia vigezo hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu 
cha Tumaini, Danford Kitwana alisema CCM inajua kuwa hakuna mgombea 
anayeweza kuwa na sifa zote 13, kwa hiyo inapaswa iangalie ni nani 
anawazidi wengine. “Kigezo cha kuwa na sifa ya maadili ndicho 
kinachowakwamisha wengi, pia hakuna mgombea anayeweza kuwa na sifa zote 
zilizowekwa na chama, mwingine anaweza kuwa na sifa saba, nne au tano.
“Wakitumia mfumo wa kuwatazama wagombea wao kwa idadi ya sifa, mtu mwenye sifa nyingi ndiye asimamishwe kugombea.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Emmanuel Mallya 
alisema Tanzania inahitaji kuongozwa na rais mwenye historia ya uadilifu
 wa matumizi ya fedha za umma.
“Tunahitaji kiongozi anayeweza kusimamia fedha za 
umma, si mtu anayenunua vitu ovyo bila kujali Hazina kuna kiasi gani, 
hilo ni tatizo kubwa,” alisema Dk Mallya. Aliongeza kuwa, kiongozi huyo lazima awe 
mchapakazi anayeweza kuwaletea wananchi maendeleo, lakini watu wengi 
wamekuwa wakisema wanamtaka mtu mwadilifu bila kuzungumzia uwezo wake wa
 kufanya kazi.
Mwalimu mstaafu wa shule ya msingi, Rehema Mathayo
 alisema kutokana na baadhi ya viongozi ndani ya CCM kukumbwa na kashfa 
za ufisadi, anayetaka kugombea urais lazima awe ‘msafi’ ndani na nje ya 
chama.
“Mshindi ndani ya chama ni mtu atakayekuwa 
amewashinda wenzake kwa kuwa na maadili mazuri na asiwe na doa lolote la
 kujishughulisha na ‘dili’ za ajabu,” alisema Rehema.
Mwalimu huyo aliongeza kuwa mgombea huyo lazima 
awe na uzoefu mkubwa wa masuala la kimataifa kwa kuwa hata kama atakuwa 
na maadili, kama hafahamu namna ya kuwaunganisha wananchi na jumuiya za 
kimataifa, hatakuwa na manufaa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Ernest 
Mwasalwiba alisema kutokana na kuporomoka kwa maadili hususan kwa 
viongozi wa umma, vitendo vya rushwa na kadhia mbalimbali, rais ajaye 
anatakiwa kuhakikisha yale anayoyasema ndiyo anayatenda na Watanzania 
hawahitaji Rais dikteta.
“Masuala ya maadili, rushwa, yote haya yanazuiwa 
mpaka sasa lakini suala ni usimamizi tu... ni wakati sasa wa rais ajaye 
kuonyesha ajenda yake itakuwa ipi, anapokuwa amesema kitu kila mtu 
lazima afuate mfano akisema anachukia rushwa na maadili kwa yaheshimiwe 
isiwe ni mjadala kila mtu anafuata kuanzia chini hadi juu. “Dikteta siyo kiongozi tunayemtaka, bali tunataka 
kiongozi atakayesimamia sheria na mifumo iliyopo iweze kufanya kazi 
ipasavyo... mfano Rais Jakaya Kikwete kipindi anaingia aliingia na 
kaulimbiu ya ‘Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mpya’ ambayo ilifuatwa hadi 
na viongozi wa halmashauri.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Romanus 
Dimoso alisema: “Sifa za rais huwa zinajulikana. Tunahitaji rais ajaye 
anayejua hali ya kisiasa ilivyo kwa sasa, hatutaki rais ambaye hatambui 
mchango unaotolewa na vyama vingi vya siasa na jinsi atakavyoweza 
kufanya navyo kazi hususan kwa kuhakikisha demokrasia inazingatiwa.”
Aliongeza: “Je, malengo ya anayetaka urais yale ya
 kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 nchi hii inafikia uchumi wa kati. 
Amejipanga vipi kama mtumishi wa kwanza wa Taifa hili kutufikisha 
huko?... Hatutaki mtu awe rais tu kwa jina.”
Rais mstaafu wa Chama cha Madaktari Tanzania 
(MAT), Dk Primus Saidia alisema: “Tunahitaji rais anayeweza kufanya 
uamuzi mgumu kwa mustakabali wa Taifa, asiwe rais wa maneno maneno, bali
 wa vitendo. Anasema dawa hospitalini hakuna na kesho zinakuwapo.
“Tunataka mtu mwenye historia ya uongozi, ameshawahi kufanya nini katika kuboresha sekta ya afya, elimu, uchumi na kijamii? Alishafanya maamuzi magumu yapi ambayo kila mmoja aliyaona na aliyaheshimu?”
CHANZO: MWANANCHI
“Tunataka mtu mwenye historia ya uongozi, ameshawahi kufanya nini katika kuboresha sekta ya afya, elimu, uchumi na kijamii? Alishafanya maamuzi magumu yapi ambayo kila mmoja aliyaona na aliyaheshimu?”
CHANZO: MWANANCHI
 

No comments:
Post a Comment