Sakata la uchotwaji wa
fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow linaendelea kuchukua sura mpya
baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Prof Sospeter Muhongo kutoa
ufafanuzi wa Serikali bungeni mjini Dodoma kuwa fedha hizo si za umma na
kwamba bado Serikali ina mzigo wa madeni katika sakata hilo.
Kauli ya Prof Muhongo inakuja siku moja baada ya
Kamati ya PAC kuwasilisha ripoti yake jana juu ya suala hilo ambapo
pamoja na mambo mengine, Kamati ya PAC ilijiridhisha kuwa sehemu ya
fedha hizo ni za Serikali.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe akisoma taarifa ya
kamati hiyo jana alisema Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), Francis Mwakapalila, Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade
wakithibitisha kuwa sehemu ya fedha zilizokuwamo kwenye Akaunti ya
Tegeta Escrow zilikuwa za Serikali.
Akiwasilisha maelezo ya Serikali leo, Prof Muhongo
alipangua hoja moja baada ya nyingine zilizotolewa na Kamati ya PAC
jana na kusisitiza kuwa fedha hizo si mali ya umma.
Prof Muhongo pia alitumia muda mwingi kueleza
jinsi Kampuni ya uwakili ya Mkono and Advocates iliyokuwa ikiitetea
Serikali pamoja na Tanesco, ilivyochota kiasi kikubwa cha pesa kama
malipo ya kazi hiyo tangu kuanza kwa mgogoro huo.
“Gharama za mawakili; Kampuni ya Mkono &
Advocates waliokuwa wakiitetea Tanesco na Serikali katika suala la IPTL
tangu mwaka 1998 hadi 2013 ni Sh62.90 bilioni na bado wanaidai Serikali $
milioni nne,” alismea Prof Muhongo.
Aliongeza kuwa Kampuni hiyo ya Mkono &
Advocates iliishauri Serikali kuwapa kazi nyingine ya kwenda kuitetea
Serikali juu ya mgogoro huo, lakini Serikali ilikataa na kuongeza kuwa
waliokoa Sh95 bilioni kwa uamuzi huo kwani uwezekano wa kushinda ulikuwa
mdogo.
Nchi yatikiswa
Dodoma. Hatimaye mtikisiko wa tano umetimia na
nchi kutikiswa; ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC)
imependekeza kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu, Waziri wa
Nishati na Madini, naibu wake na katibu mkuu wa wizara hiyo
wawajibishwe kutokana na kuhusika kwao kwenye sakata la uchotwaji wa
Sh306 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa ajili ya kutunza
fedha za gharama za uwekezaji (capacity charge) baada ya kuibuka mzozo
wa kimkataba baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni
binafsi ya IPTL ambayo iliingia mkataba wa kufua umeme na kuliuzia
nishati hiyo shirika hilo la umma.
Ripoti hiyo ilisomwa jana bungeni kwa kupokezana
kati ya Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe na Makamu mwenyekiti, Deo
Filikunjombe baada ya majadiliano marefu kwenye vikao vya ndani vya CCM
na Kamati ya Uongozi wa Bunge na jitihada kubwa za kutaka isisomwe na
kujadiliwa.
Ripoti hiyo ilitokana na ukaguzi uliofanywa na
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo ilianika
ukiukwaji mkubwa wa taratibu wakati wa uchotaji wa fedha hizo pia
mahojiano na mkurugenzi mkuu wa Takukuru na Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA).
Waziri Pinda ametiwa hatiani na kamati hiyo kutokana na kujua
kuwapo kwa ufisadi huo na kauli zake kuwa fedha hizo hazikuwa mali ya
umma, wakati Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Werema ameonekana
kutoishauri vizuri Serikali na pia kuagiza fedha hizo zitolewe kwenye
akaunti hiyo, wakati Waziri Sospeter Muhongo hakuchukua hatua wakati
akijua kuwapo kwa sakata hilo, huku naibu wake, Stephen Masele akitiwa
hatiani kwa kulidanganya Bunge.
Kamati pia imependekeza uteuzi wa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi utenguliwe kutokana na
kuingia makubaliano ya kutoa fedha bila ya kujiridhisha kikamilifu
kuhusu uamuzi wa hukumu ya mahakama ya Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi
wa Migogoro ya Kiuwekezaji (ICSID).
Iwapo mjadala huo, unaotazamiwa kuendelea leo,
utaafiki hatua hizo zichukuliwe, Rais atalazimika kuunda Serikali upya
kwa mara ya pili tangu alipofanya hivyo mwaka 2008 wakati wa sakata la
Richmond, ambalo lilihusu umeme. Pia atakuwa akifanya mabadiliko ya
mawaziri kwa mara ya tano kutokana na wasaidizi hao kujikuta kwenye
kashfa.
Kuhusu Pinda
Akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo, Makamu
Mwenyekiti wa PAC, Filikunjombe alisema katika suala hilo, Pinda
anahusika kwa kuwa katika Katiba Ibara ya 52(1) inaeleza kuwa waziri
mkuu atakuwa na madaraka ya juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa
siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Pia ibara ya 52(2) inasema waziri mkuu atakuwa
kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni. Kutokana na ibara hizo,
Filikunjombe alisema baada ya kupitia vielelezo vilivyomo kwenye ripoti
ya CAG, kamati imejiridhisha pasipo shaka kwamba Waziri Mkuu alikuwa ana
taarifa zote kuhusiana na mchakato mzima wa kuchotwa fedha katika
Akaunti ya Escrow.
“Ushahidi uliotolewa na CAG kwenye kamati
unaonyesha kuwa waziri mkuu alikuwa akipata taarifa za jambo hili na
kamati imesikitishwa kuona kuwa Waziri Mkuu hakuchukua hatua zozote
kuzuia muamala huu usifanyike,” alisema Filikunjombe.
Alisema: “Kamati inathibitisha bila shaka kwamba
waziri mkuu alikuwa analijua jambo hilo vizuri na kwamba aliridhia
muamala huo ufanyike na ndiyo maana kauli zake bungeni mara kadhaa
alithibitisha kuwa fedha za escrow si mali ya umma.
“Kwa uzito na unyeti wa jambo hili, kwa vyovyote
vile Waziri Mkuu anapaswa kuwajibika kwa kauli zake na kwa
kutokutekeleza wajibu wake wa kikatiba ipasavyo, ili kurejesha imani ya
wananchi kwa Serikali yao na viongozi wao kisiasa,” alisema mbunge huyo
wa Ludewa.
Maswi kikaangoni
Kuhusu Maswi, kamati ya PAC imethibitisha kuwa
katibu mkuu huyo aliingia makubaliano ya kutoa fedha katika Akaunti ya
Tegeta Escrow bila kijiridhisha kikamilifu kuwa maamuzi ya hukumu ya
ICSID yalikuwa bado kutolewa na hivyo kusababisha fedha kutolewa bila
kukokotoa upya gharama za ‘capacity charges’ jambo ambalo limesababisha
kupotea kwa fedha za umma.
“Pia kamati imethibitisha uzembe wa hali ya juu uliofanywa na
katibu mkuu huyo, kushindwa kujiridhisha kama masharti ya sheria ya kodi
ya mapato sura ya 333 kifungu cha 90(2) yalitekelezwa. Kifungu hicho
kimsingi kinaitaka mamlaka ya ‘approval’ ya uhamishaji wa kampuni
kutotambua kampuni mpaka kwanza kodi za uhamishaji ziwe zimelipwa na
hati za malipo ya kodi zimetolewa na mamlaka ya kodi,” alisema
Filikunjombe.
Alisema kutokana na hilo kamati inapendekeza kuwa
uteuzi wa katibu mkuu huyo utenguliwe na Takukuru wamfikishe mahakamani
mara moja, kwa kukosesha serikali mapato, matumizi mabaya ya ofisi na
kusaidia utakatishaji wa fedha haramu.
Kauli zamponza Masele
Kwa upande wa Masele, Filikunjombe alisema kuwa
kamati imethibitisha kuwa naibu waziri huyo alisema uongo bungeni kwa
kutamka kauli ambazo zilikuwa na lengo la kupotosha umma kuhusu akaunti
hiyo ikiwamo kutoa kauli ambazo zingeweza kusababisha nchi kuingia
kwenye mgogoro wa kidiplomasia na nchi ya Uingereza.
“Kamati inapendekeza naibu waziri huyo achukuliwe
hatua kali za kinidhamu ikiwemo kutenguliwa uteuzi wake. Pia
inapendekeza kuwa naibu waziri huyo afikishwe mbele ya kamati ya Bunge
ya Maadili ili aadhibiwe kama mbunge kwa kusema uongo bungeni ili iwe
fundisho kwa wabunge wengine kuhusiana na kauli wanazotoa ndani ya
Bunge,” alisema Filikunjombe.
Muhongo matatani
Akizungumzia kuhusu Muhongo, alisema kamati
imethibitisha kuwa waziri huyo amekuwa mara kwa mara akipotosha Bunge na
Taifa kwa ujumla kuhusu fedha za akaunti hiyo kwamba ndani ya fedha
hizo hakukuwa na fedha za umma.
Alisema kuwa kamati imebaini kuwa waziri huyo,
ambaye wakati wote alikuwa akitingisha kichwa kuonyesha kutokubaliana na
taarifa ya kamati, ndiye alikuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Harbinder
Singh Sethi na James Rugemalira tena katika ofisi ya umma na pengine
hilo ndilo lilikuwa sababu ya upotoshaji huo.
“Iwapo waziri huyo angetimiza wajibu wake
ipasavyo, fedha za Tegeta Escrow zisingelipwa kwa kwa watu wasiohusika
na nchi ingeweza kuokoa mabilioni yaliyopotea kama kodi za VAT, Capital
Gain Tax na ushuru wa stempu ambazo ni sawa na takribani Sh30 bilioni,”
alisema Filikunjombe.
Kutokana na hilo, Filikunjombe alisema kamati
inapendekeza kuwa mamlaka yake ya uteuzi itengue uteuzi wake kutokana na
sababu hizo.
Werema naye yumo
Kuhusu AG, Filikunjombe alisema kuwa kamati
imethibitisha kuwa Jaji Werema alitoa ushauri ulioipotosha Benki Kuu ya
Tanzania kuhusu hukumu ya Jaji Utamwa kwa kutumia madaraka yake vibaya,
AG aliagiza kodi ya serikali yenye thamani ya Sh21 bilioni isilipwe na
hivyo kuikosesha serikali mapato adhimu.
“Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kujua au kwa makusudi
alipotosha Bunge na Taifa kwamba mgogoro uliopelekea kufunguliwa kwa
Akaunti ya Escrow ulikuwa ni mgogoro wa wanahisa wa IPTL badala ya
mgogoro kati ya Tanesco na IPTL,” alisema Filikunjombe.
Alisema kutokana na hilo kamati inapendekeza kuwa
uteuzi wa manasheria mkuu wa serikali utenguliwe mara moja na kisha
afikishwe mahakamani kwa maumizi mabaya ya ofisi yaliyopelekea serikali
kupoteza mabilioni ya fedha.
Baada ya kumaliza kusoma mapendekezo hayo, Spika
wa Bunge, Anne Makinda alisema Serikali itatoa majibu leo kabla ya
mjadala kuendelea.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment