Social Icons

Pages

Friday, November 21, 2014

PINDA: MA-RC TAFUTENI NJIA ZA AJIRA KWA VIJANA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amewaagiza wakuu wa mikoa nchini kufanya uchambuzi wa kujua mahitaji ya ajira za vijana na kutafuta njia ya kuanzisha ajira mpya hasa katika maeneo ya vijijini.
Alitoa agizo hilo mjini hapa juzi wakati akifungua kongamano la siku mbili la wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa yote nchini lililolenga kujadili changamoto ya ajira kwa vijana.
Alisema ni lazima kukaa chini na kufanya ubunifu wa ajira mpya kwa vijana nchini kama vile ufugaji, uvuvi, useremala, uashi na biashara ya usafirishaji ambayo iko vijijini. Aliongeza kuwa katika kutekeleza kazi hizo, ni lazima kuchukua hatua madhubuti za kuendelea kuboresha mazingira ya vijijini ili kuepusha vijana kukimbilia mijini kutafuta kazi.
“Hatua hizo ni pamoja na kuainisha na kuimarisha fursa zilizoko mijini na vijijini hususan kuweka sera nzuri za kuvutia wawekezaji katika sekta ya viwanda hasa vya usindikaji wa bidhaa zinazotokana na bidhaa zinazozalishwa ndani na wananchi, kutafuta namna ya kusaidia vijana kupata mikopo, kuboresha mazingira ya vijijini na kuwezesha kupata huduma muhimu za kijamii kama vile umeme, maji, shule na kuwafundisha vijana elimu ya ujasiriamali na ufundi stadi,” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, ukosefu wa ajira umekuwa changamoto kubwa kwa sasa duniani kwani ripoti ya mwaka 2014 ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuhusu hali ya ajira imeonesha kuwa takribani zaidi ya watu milioni 202 sawa na asilimia sita ya watu wanaostahili kufanya kazi, hawana kazi ambapo kati yao vijana ni milioni 74.5 sawa na asilimia 13.1.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: