
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum
Muswada huo wa Sheria ya Takwimu wa Mwaka 2013, uliwasilishwa na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, bungeni mjini hapa jana.
Moja ya kifungu cha muswada huo kilicholalamikiwa na wabunge wa upinzani ni Ibara ya 37 (4), ambacho kinaeleza wadau na vyombo vya habari watakaotoa takwimu bila kibali cha Ofisi ya Takwimu watafungwa jela miaka mitatu pamoja na faini ya Sh. milioni 10 au vyote kwa pamoja.
Adhabu hiyo iliungwa mkono na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, inayoongozwa na Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, kupitia maoni ya kamati hiyo yaliyowasilishwa bungeni jana.
Awali, akiwasilisha muswada huo bungeni jana asubuhi kabla ya baadaye jioni kuuondoa, Waziri Saada alisema lengo lake ni kuipa mamlaka zaidi Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya kutekeleza majukumu yake ya kitakwimu kwa uhuru na ufanisi.
Alisema lengo lingine ni kuanzisha mfumo wa utoaji wa takwimu ujulikanao kama "National Statistical System" unaokusudia kuboresha na kuimarisha takwimu rasmi nchini.
Alitaja madhumuni ya kuwapo mfumo huo kuwa ni kuwezesha nchi kupata takwimu sahihi kwa watumiaji na kupunguza migongano, hasa pale takwimu hizo zinapozalishwa na taasisi zaidi ya moja.
Alitaja mambo muhimu yaliyozingatiwa katika muswada huo kuwa ni pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa taasisi, chombo cha habari au mtu yeyote anayechapisha au kutoa taarifa zenye kuhamasisha wananchi wasishiriki au kutoa ushirikiano katika zoezi lolote la ukusanyaji wa takwimu rasmi nchini.
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilihoji adhabu hiyo ikisema uthibitisho wa kosa lake bado ni kitendawili.
Akiwasilisha maoni ya msemaji mkuu wa kambi hiyo wa wizara hiyo, kuhusu muswada huo, bungeni jana, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Christina Lissu, alisema licha ya adhabu hiyo kuwa ni jambo jema katika kujenga nidhamu ya utoaji taarifa kitakwimu, haijulikani atakayethibitisha kosa hilo kutendwa na vyombo vya habari.
“Je, haitakuwa kwamba, taarifa zisizoipendeza serikali ndiyo zitaonekana za upotoshaji hata kama zina ukweli?” alihoji Lissu.Alisema taaluma ya habari inazingatia utafiti na siyo rejea pekee ya taarifa rasmi zilizotolewa na serikali.
Alisema kuvibana vyombo vya habari kutumia taarifa za serikali na wakala wake ni kutotambua kazi ya wanahabari ya kufanya tafiti na kuitaarifu jamii juu ya mambo yanayoihusu.
Alisema pia ni kuendeleza kuvinyima uhuru vyombo vya habari na kuwanyima wananchi haki ya kupata habari kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 18 (d) juu ya kupata taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi.
“Pamoja na kuminya uhuru wa vyombo vya habari bado haielezwi ni kwa vipi chombo cha habari kitapelekwa jela. Kwa tafsiri ndogo ni kwamba bado hakuna uzoefu wa utekelezaji wa kutoa adhabu ya aina hiyo kwa chombo cha habari,” alisema Lissu.
Aliongeza: “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kurejea upya muswada huu kwa kutokuwa na hila na vyombo vya habari na kuangalia mbali zaidi kwa manufaa ya taifa letu.”
“Pia inaitaka serikali kuweka sheria ya kutambua takwimu hizi, ambazo zitajenga serikali yenye nidhamu ya uwajibikaji kwa wananchi na siyo kuficha uovu kwa kutunga sheria kandamizi kwa taasisi za kuwasaidia wanyonge.”
KAMATI YA BUNGE
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Luhaga Mpina, alishauri adhabu ya mwaka mmoja kwa kosa hilo iongezwe.
“Kamati inashauri kuwa kifungu kiongezeke na kuwa miaka mitatu badala ya miezi kumi na mbili ili kuzuia tabia ya baadhi ya watu kutoa takwimu za uongo na kwa makusudi kabisa kwa lengo la kupotosha jamii,” alisema Mpina.
Pia alisema takwimu na tafiti mbalimbali zinazofanywa, ripoti zake zipelekwe katika maktaba za serikali kwa ajili ya kutumiwa na wadau wa takwimu.
Akichangia mjadala kuhusu muswada huo bungeni jana, Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa, alisema iwapo serikali itakuwa na takwimu sahihi, hakutakuwa na tatizo la mishahara hewa.
WAZIRI AONDOA MUSWADA BUNGENI
Hata hivyo, baadaye jana jioni serikali ililazimika kuundoa muswada huo bungeni kwa maelezo kwamba, ili kujipanga zaidi.
Dalili za kuondolewa kwa muswada huo zilianza mapema baada ya wabunge wa upinzani kuweka azimio la kutangaza mgogoro wa kikatiba kuhusu adhabu kwa wadau.
Akitangaza uamuzi wa kuondolewa muswada huo bungeni jioni ya jana, Waziri Saada, alisema lengo ni kujipanga zaidi na kuingiza maoni muhimu ya wadau.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapenda kuliarifu Bunge lako tukufu tunaomba kuundoa muswada huu ili twende kukajipange ikiwemo kuingiza maoni ya wadau muhimu na utakapokuwa tayari tutauleta tena hapa,” alisema Waziri Mkuya.
Baada ya kutolewa kwa tamko hilo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, alitangaza kuahirisha Bunge hadi leo asubuhi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment