
Dk. Makongoro Mahanga
1. Shomari Kitogo, mkazi wa Segerea
Barabara hasa kutoka Segerea Mwisho hadi
Makaburini ambako ni nyumbani kwako ni mbovu, nataka unipe maelezo ya
kina na yenye matumaini ya utekelezaji ili unishawishi kukupa kura yangu
katika uchaguzi ujao.
Jibu: Kuna miradi mingi ya barabara na madaraja
iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na Wakala wa Barabara
Tanzania (Tanroads) katika Kata ya Kinyerezi, barabara ya kutoka
Segerea-Kinyerezi hadi Majumba Sita imekamilika kuboreshwa kwa lami na
wakala huyo katika kipindi hiki.
Pia, Tanroads imekamilisha daraja kubwa la
Segerea/Kinyerezi na imeanza ujenzi wa daraja jingine kubwa la
Kinyerezi/Sitakishari. Tanroads pia imekuwa ikikarabati Barabara ya
Kinyerezi-Kifuru-Malambamawili kwa changarawe huku mipango ya kuanza
kujenga barabara hiyo kwa lami ikiwa imekamilika na ujenzi utaanza
wakati wowote kwa kipande cha Kinyerezi hadi Kifuru. Barabara nyingine
inayosimamiwa na wakala ni ya Kimara - Bonyokwa hadi Kinyerezi Shule.
Nimeshaiagiza Tanroads ikarabati barabara hiyo kwani iko katika hali
mbaya.
2. Stella David, mkazi wa Tabata
Sijawahi kukuona hata siku moja. Ningekuwa
nimekuona ningetaka unieleweshe sababu za kutokuwa na maji kwa miaka
yote hii. Sidhani kama mimi nitakuwa mpigakura wako labda nitakapopata
jibu la uhakika ni lini tutapata maji?
Jibu: Natembelea jimboni mara kwa mara na kipindi
hiki kuanzia Julai 5 hadi 26, nilitembelea Kata zote nane za jimbo langu
na kufanya mikutano ya hadhara. Ninachoweza kusema ni kwamba wapigakura
wangu wasidhaharau matangazo wanaposikia wajongee na waniulize maswali
nitawajibu na yakibaki nitapanga siku ya kukutana nao na kuwaelewesha.
3. Salmini Myemba, makazi Kinyerezi
Kuna baadhi ya maeneo yamejengwa kiholela, hakuna
kinachofanyika kuhakikisha kunakuwa na mitaa inayopitika, nahitaji
ufafanuzi suala hilo utalifanyia kazi lini na mchakato wake ukoje?
Vilevile, suala la michango shuleni limekuwa tatizo nataka anipe
ufafanuzi litakwisha lini kwa sababu Serikali imetangaza kuwa elimu ni
bure.
Jibu: Mitaa mingi imejengwa siku nyingi,
ninachoweza kusema watu wa Mipango Miji hawakuliona hilo tangu awali.
Mimi kama Mbunge inakuwa ngumu kutatua kero hiyo kwa kuwa sina fedha za
kuwalipa ili nipitishe bomoabomoa kunyoosha mitaa.
Kwa hiyo ninachofanya sasa ni kuhakikisha wanaojenga kipindi
hiki wanafuata utaratibu katika ujenzi wakizingatia barabara na
kutojenga kwenye mkondo wa maji kwani mara nyingi ujenzi huo ndiyo
unaosababisha mafuriko na wapo watu wameshapewa onyo mara kadhaa licha
ya kuwa viwanja ni vyao.
4. Asha Said, mkazi wa Tabata Bima
Katika jimbo letu vikoba ni mtihani, hakuna juhudi
unazofanya ukishirikiana na watendaji wako kuhakikisha tunapata mikopo
ya kujikomboa. Kama unataka kura yangu, nipe maelezo ya kina na
nikuelewe.
Jibu: Miongoni mwa mambo niliyowahi kuyatolea
ufafanuzi mara nyingi tena katika mikutano ya hadhara ni kuwataka kina
mama kuungana katika vikundi na kuwasilisha maombi yao.
Nitakuwa na nafasi nzuri ya kuwasaidia wakiwa
wameungana na ninakuruhusu uzunguke kwa kina mama walioungana na
kuhitaji mikopo ukimpata aliyenyimwa, njoo uniulize tena, kwani nina
uhakika hakuna na ninaweza kusem jimbo langu linaongoza kwa kina mama
kujishughulisha katika vikundi na kupatiwa mikopo.
5. Janeth Msami - Mkazi wa Gongolamboto
Kero ya michango shuleni, mtoto anasoma nusu mwezi
kila siku anarudishwa kibaya zaidi kila mwaka tunachangia madawati
lakini bado kuna watoto wanakaa chini. Mbunge ni kwa jinsi gani
unalifanyia kazi tatizo hili?
Jibu: Michango shuleni siyo ya ada ni ile ambayo
wanakubaliana kati ya wazazi na kamati za shule, hivyo lipo chini ya
makubaliano hayo. Hapa labda nitoe angalizo tu kuwa wazazi wanatakiwa
kuhudhuria mikutano ya shuleni ili vitu muhimu kuhusu elimu ya watoto
wao vinapojadiliwa wawepo. Hili limekuwa linaleta manung’uniko mengi kwa
wazazi kutokana na kuambiwa elimu ni bure na wanasahau kuwa kuna
masuala ambayo wazazi wanatakiwa kuchangia ikiwamo masomo ya ziada.
6. Maze Moshi, mkazi wa Tabata Kimanga
Utendaji wako wa kazi hauridhishi. Jipange
kulitembelea jimbo lako kama vipi uache kimoja kama unataka kuwa mbunge
uwe mbunge, ukitaka kuwa waziri uwe waziri kwa sababu huonekani jimboni.
Jibu: Kuwa waziri na mbunge hakunizuii kufanya
mambo yangu, ingawa kuna wakati nakiri ninakuwa na kazi nyingi kiasi
kwamba nalazimika kuacha majukumu kwa watendaji wengine.
Kutekeleza majukumu ni wajibu wangu bila kujali
nipo wapi, lakini kuhusu kufika jimboni kama nilivyokwishasema hapo
awali, siyo kweli kwamba sifiki, ninajitahidi kuzunguka katika kata zote
nane na kukutana na wananchi, kama ambavyo nimefanya mapema mwaka huu
na huo ni utaratibu wangu wa miaka yote.
7. Gidion Lameck, mkazi wa Tabata Shule
Uliahidi kuboresha ajira kwa vijana. Nataka kufahamu hali hii hadi lini?
Jibu: Tatizo la ajira ni kubwa na siyo Tanzania
pekee, bali duniani kote. Ndiyo maana tunajitahidi kuhakikisha vijana
wanapokuwa shuleni wanajifunza kujiajiri badala ya kuwekeza akili katika
kuajiriwa. Lakini ukija ofisini kwangu utakuta ushahidi wa mafaili ya
vijana wanaoomba niwasaidie kuwaunganisha katika kazi mbalimbali na mara
mojamoja ninapopata nafasi za kuwaweka ninafanya hivyo.
Ushauri wa bure, waungane katika vikundi ili
niangalie ni namna gani ninaweza kuwasaidia na wao wakajisaidia kwa
kuwapa semina na mitaji kwa wanatakaokuwa na nia ya kufanya biashara,
lakini kuwapa ajira mmojammoja ni ngumu kwani vijana wapo wengi na ofisi
zenye kazi au kampuni zenye nafasi zipo chache.
8. Emmanuel Sanga, mkazi wa Vingunguti
Umewasahau wapigakura wako, ukija huku unakutana na wanaCCM
wenzako unaondoka. Kwa nini tangu tumekuchagua huji kusikiliza
malalamiko yetu hadi waandishi wakuulizie?
Jibu: Siyo kweli kwamba nakutana na wanaCCM,
kinachotokea kama wanachama, mbunge wao anapokuwa kwenye mkutano na
wananchi lazima watafika kwa wingi wakiwa wamevaa sare, hivyo kuonekana
kama nimekwenda kuzungumza na wao.
Namshauri mwananchi wangu mpigakura wangu, afike
katika mikutano yangu bila kujali wamejaa watu wa aina gani na kama ana
swali lolote aniulize, nitampa majibu palepale.
9. Jonas Mahimbo, mkazi wa Vingunguti
Huku maeneo ya Vingunguti miundombinu ni mibovu. Barabara nyingi zipo katika hali mbaya. Je, una sifa ya kuendelea kuwa mbunge?
Jibu: Sifa ninayo kutokana na juhudi ninazofanya
kutatua tatizo hilo ikiwamo miradi ya miundombinu iliyotekelezwa katika
Kata ya Vingunguti. Ujenzi wa daraja kubwa la Vingunguti/Segerea
limekamilika kwa gharama ya zaidi ya Sh2 bilioni. Miradi ya miundombinu
chini ya mradi wa CIUP ikiwamo ujenzi wa barabara ya lami kutoka
Barabara Kuu ya Nyerere hadi Vingunguti Darajani na ile ya Mtaa wa
Miembeni ilikamilika pia katika kipindi hiki. Barabara nyingine za
changarawe katika Kata ya Vingunguti chini ya mradi huu pia zilikamilika
ikiwamo ya kuelekea Majengo na Mji Mpya. Tumemteua I.K. Andersen
Contractors kukarabati barabara ya Vingunguti Relini – Karakata (Ng’ombe
Road) kwa gharama ya Sh43,108,590 na kazi hiyo itaanza hivi karibuni.
10. Mage Sheki, mkazi wa Ukonga
Maji ni tatizo sugu katika jimbo hili hakuna mkazi
asiyelalamikia maji. Je, ni lini tutapata maji kama wenzetu wa majimbo
mengine?
Jibu: Tatizo la maji bado ni kubwa Kata ya
Kinyerezi. Hata hivyo, kuna miradi inayoendelea ya kuchimba visima,
ukiwamo mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Ubelgiji na Umoja wa Ulaya
(EU/BTC) katika eneo la Kanga. Mradi huu umekamilika isipokuwa tatizo ni
umeme mdogo. Tayari Tanesco wameombwa kurekebisha hali hiyo. Pia katika
mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) wa miradi ya visima katika vijiji
10 kila wilaya, Kata ya Kinyerezi itachimbiwa visima viwili maeneo ya
Bonyokwa na Kifuru. Pia kuna Sh30 milioni ambazo zitatumika kutafutia
chanzo kingine cha maji mazuri. Tatizo la Kata ya Kinyerezi ni
kukosekana kwa maeneo mengi yenye maji mazuri na ya kutosha. Mbali na
mradi mkubwa wa maji wa Dawasa kutoka Ruvu Juu kukamilika Septemba, 2015
tatizo la maji katika Jimbo la Segerea ikiwamo Kata ya Kinyerezi
litakwisha.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment