
Utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Twaweza Septemba mwaka huu matokeo yake yalitangazwa jijini Dar es Salaam jana, na Mtafiti wake, Elvis Mushi, ambaye alisema wananchi 1,445 waliohojiwa kwa njia ya simu.
Mushi alisema asilimia 13 walisema wangemchagua Lowassa, huku asilimia 12 wakisema wangemchagua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kama uchaguzi huo ungefanyika Septemba mwaka huu.
Utafiti huo ni wa tatu kufanywa na Twaweza. Mwaka 2012 Lowassa alikuwa anakubalika kwa asilimia sita, mwaka jana asilimia 13 sawa ya mwaka huu.
Pinda mwaka 2012 alikuwa anakubalika kwa asilimia 16, mwaka jana asilimia 11 na mwaka huu asilimia 12. Aidha, katika uwezekano wa kupitishwa na chama kuwania nafasi ya urais, mwaka 2012 Lowassa alipata asilimia nane, mwaka jana asilimia 20 na mwaka huu asilimia 17.
Pinda mwaka 2012 alikuwa na asilimia 23 ya kuweza kuteuliwa, mwaka jana asilimia 14 sawa na mwaka huu.
Katika utafiti huo, makada wengine wa CCM walipigiwa kura ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye kwa mwaka huu ana asilimia tano ikilinganishwa na mwaka jana alipokuwa na asilimia mbili na 2012 alikuwa na asilimia nne ya uwezano wa kuchaguliwa.
Aidha, Membe angeliweza kupitishwa na chama chake kwa asilimia saba mwaka huu, huku mwaka 2012 akiwa na asilimia tano na mwaka jana asilimia nne.
Katika uwezekano wa kuchaguliwa Dk. Slaa anashikilia nafasi ya tatu nyuma ya Lowassa na Pinda, akiwa na uwezekano wa wananchi kumchagua kwa asilimia 11, tofauti na mwaka 2012 alipokuwa na asilimia 19 sawa na mwaka jana.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba anashikilia nafasi ya nne kwa uwezekano wa wananchi kumchagua akiwa na asilimia sita, tofauti na mwaka juzi alipokuwa na asilimia tatu na mwaka jana asilimia tano. Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambaye hivi karibuni amelalamikiwa sana na wananchi katika suala la mchakato wa katiba, akiwa anajipambanua kuwa ni mtaji wa urais, ameshika nafasi ya sita akiwa na asilimia nne mwaka huu, mwaka juzi asilimia mbili na mwaka jana asilimia tatu. Sitta ameshikilia nafasi ya sita katika orodha ya wagombea tisa.
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ameshikilia nafasi ya saba akiwa na asilimia tatu mwaka huu, mwaka juzi asilimia sita na mwaka jana asilimia tano za uwezekano wa kuchaguliwa.
Mwenyekiti wa Chadema, Freema Mbowe, amefungana na Dk. Magufuli katika nafasi ya saba, huku mwaka juzi akiwa na asilimia moja na mwaka jana asilimia tatu.
Mbunge wa kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ameshika nafasi ya nane akiwa asilimia moja ikilinganishwa na mwaka jana na mwaka juzi alipopata asilimia tatu.
“Utafiti huo umebaini kwamba uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani utakuwa ‘mgumu zaidi’ katika historia ya Tanzania kuanzia ngazi ya ubunge hadi urais,” alisema Mushi.
Kulingana na utafiti huo, Lowassa amepanda kwa asilimia 7 zaidi mwaka huu ukilinganisha na mwaka 2012 alipokuwa na asilimia 6 na mwaka 2013 alikuwa na asilimia 13 kama ilivyo mwaka huu.
Mwaka 2012 Pinda alikuwa na asilimia 16 na kushuka hadi asilimia 11 mwaka 2013 na amepanda kwa asilimia 1 mwaka huu baada ya kuwa na asilimia 12.
Matokeo yanaonyesha kuwa Dk. Slaa ameshuka kwa asilimia nane tangu mwaka 2012 na mwaka jana alipokuwa asilimia 19 kuwashinda Lowassa na Pinda kwa miaka miwili mfululizo.
Mushi alisema katika utafiti huo wafuasi wa CCM waliohojiwa kuhusu nani anafaa kuwa rais, mbunge au diwani, asilimia 24 walisema watampigia kura mwanachama yeyote atakayeteuliwa na chama hicho.
Mushi alisema utafiti huo umeonyesha kuwa mgombea kutoka CCM kama uchaguzi ungefanyika leo angeongoza kwa asilimia 47, mgombea kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) asilimia 28, mgombea binafsi asilimia 19 na asilimia 6 waliohojiwa walisema hawajui.
NANI ANAFAA KUPEPERUSHA BENDERA YA CCM
Watu waliohojiwa ambao ni wanachama wa CCM walioulizwa ni nani anapaswa kupeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi ujao, mwaka 2012 asilimia 42 walisema hawana uhakika, lakini idadi hiyo imepungua mwaka 2014 na kufikia asilimia 18 huku asilimia 24 hawakutaja jina lolote walisema watampigia mtu yeyote.
Alisema kwa wale waliotaja majina ya watu wanaowataka, asilimia 17 walimtaja Waziri Mkuu mstaafu, Lowassa, akifuatiwa na Waziri Mkuu wa sasa, Pinda asilimia 14.
Kuhusu umoja wa vyama vya siasa una nafasi katika uchaguzi ujao, wananchi walioulizwa asilimia 47 walisema wangeichagua CCM na theluthi moja wangempigia kura mgombea kutoka Ukawa.
NANI ANAFAA KUPEPERUSHA BENDERA YA UKAWA
Watu wanne kati ya 10 ambao sawa na asilimia 41 walioulizwa walimtaka Dk. Slaa, kwamba anafaa kupeperusha bendera ya Ukawa. Wengine waliopata zaidi ya asilimia 10 ni Prof. Lipumba asilimia 14, Mbowe asilimia 11 na Zitto aliyepata asilimia 6.
Viongozi wengine waliopata asilimia moja kila mmoja ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa TLP, Agustino Mrema.
NAFASI YA CCM 2015
Utafiti huo unaonyesha kuwa kwa mwaka 2014 CCM inaendelea kuongoza dhidi ya upinzani kwenye uchaguzi wa ngazi zote tatu, yaani ngazi ya udiwani, ubunge na urais.
Takwimu zinaonyesha kuwa kama uchaguzi ungefanyika Sepemba mwaka huu CCM ingeshinda uchaguzi hata kama vyama vyote vya upinzani vingeungana na kuweka mgombea mmoja wa urais.
Katika mgombea urais, CCM angepata asilimia 51, Chadema asilimia 23, CUF ailismia 4 na NCCR-Mageuzi asilimia moja.
ASILIMIA 47 YA WABUNGE KUNG’OKA
Mushi alisema wananchi walioulizwa kama watampigia tena mbunge wao wa sasa, asilimia 47 walisema hapana kwa sababu hajatekeleza ahadi walizoziahidi mwaka 2010.
Kwa upande wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wananchi wengi waliohojiwa nani anaweza kupeperusha bendera ya Ukawa, walimtaja Dk. Slaa.
“Dk. Slaa alitajwa na watu wanne kati ya 10 waliohojiwa (41), wakati viongozi wengine wa Ukawa waliopata zaidi ya asilimia 10 ni Prof. Ibrahim Lipumba (14) na Freeman Mbowe (11).
“Wagombea watalazimika kufanyakazi ya ziada kupata wapiga kura hasa kwa kuwa kuna kundi kubwa yaani asilimia 19 ya wananchi waliosema watapima uwezo wa mgombea,” alisema.
Ripoti ya utafiti huo imeandikwa na Youdi Schipper na Elvis Mushi na kuhaririwa na Risha Chande na Rakesh Rajani.
Matokeo ya utafiti huo yamebainisha pia kuwa pamoja na kwamba umaarufu wa CCM umeporomoka, bado kina wafuasi wengi Tanzania Bara. Kuhusu makada wanaotajwa kusaka urais ndani ya CCM, utafiti umebaini kwamba hakuna hata mmoja mwenye uhakika wa kufanya vizuri.
KATIBA MPYA SULUHiSHO LA MATATIZO
Akichangia katika mjadala huo, Jenerali Ulimwengu, alisema changamoto za umaskini, ujinga na maradhi suluhisho lake ni kuwa na katiba iliyo bora.
“Umuhimu wa katiba ni kila kitu namna gani mnataka kutawaliwa, ukidharau katiba unapata matatizo yote hayo, tujenge utamaduni wa kuheshimu katiba,”alisema.
Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema vyama vya siasa vitafakari kutokana na kasi ya wananchi kuendelea kukosa imani na vyama.
“Taasisi za kisiasa zimepoteza mvuto kwa wananchi, mfano hivi sasa vimeelekeza nguvu kuzungumzia suala la Katiba badala ya kuzungumzia kero zinazowakabili Watanzania kama elimu, afya na umaskini,”alisema.
Kwa uapnde wake Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM. Nape Nnauye, alisema suala la utekelezaji wa ahadi zinazotolewa na wagombea linapaswa kuangaliwa mfano wakati takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya wananchi wanajihusisha na kilimo, lakini utafiti huo unaonyesha ahadi zilikuwa ni asilimia 2 tu.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment