Social Icons

Pages

Monday, November 24, 2014

IPTL KUTAWALA WIKI YA MWISHO YA BUNGE

Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)Zitto Kabwe.
Bunge leo linaingia katika wiki yake ya nne na ya mwisho, huku mjadala kuhusu ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ya uchotwaji wa Sh. bilioni 306 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ukitarajiwa kuliteka Bunge.
Ratiba ya Bunge inaonyesha kuwa taarifa maalumu kuhusu ripoti hiyo, itawasilishwa bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) inayoongozwa na Zitto Kabwe  (pichani), pamoja na mapendekezo ya kamati hiyo keshokutwa.
Ripoti hiyo inahusu ukaguzi wa hesabu za fedha hizo uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) kuhusiana na kashfa hiyo.
Mjadala kuhusu ripoti hiyo uliibuliwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, na kusababisha kuzua mvutano mkubwa kati yake na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema.
Zinadaiwa kuchotwa kutoka kwenye akaunti hiyo na vigogo mbalimbali, wakiwamo mawaziri, wabunge, majaji wa Mahakama Kuu na viongozi wa dini.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema wameongeza muda wa wabunge kuijadili taarifa hiyo ya PAC pamoja na mapendekezo yatakayotolewa na kamati hiyo kuhusiana na ripoti hiyo.
Alisema sasa taarifa hiyo ya PAC itajadiliwa kwa siku mbili; Jumatano na Alhamisi, badala ya siku moja iliyokuwa imepangwa awali.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa leo baada ya kipindi cha maswali na majibu, pamoja na mambo mengine, wabunge wataendelea kujadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2014.
Muswada huo uliwasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, na ulianza kujadiliwa na wabunge, Ijumaa wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Azimio la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Ushirikiano katika masuala ya kiulinzi, litawasilishwa bungeni kesho.
Lingine ni Azimio la Kuridhia Itifaki ya Uzuiaji wa Vitendo Haramu dhidi ya Usalama wa Miundombinu ya Kudumu iliyojengwa chini ya Bahari katika Mwambao wa Bara ya Mwaka 1988, ambalo linatarajia kuamualiwa na wabunge wiki hii ama kulipitisha au la.
Azimio hilo liliwasilishwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, na kujadiliwa Ijumaa wiki iliyopita, lakini ikashindikana kupitishwa kutokana na akidi ya wabunge kutotimia.
Mbali na taarifa maalumu ya PAC, ratiba ya Bunge inaonyesha kuwa Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza na kuchambua sera mbalimbali zinazohusu masuala ya ardhi, kilimo, mifugo, maji na uwekezaji ili kubaini kasoro zilizomo katika matumizi ya ardhi, itawasilisha taarifa yake keshokutwa bungeni.
Alhamisi, baada ya kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa waziri mkuu na maswali ya kawaida, wabunge wataendelea kujadili taarifa ya Kamati hiyo teule ya Bunge.
Ijumaa, baada ya kipindi cha maswali na majibu, waziri mkuu anatarajiwa kuwasilisha hoja ya kuahirisha Bunge.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: