Rais wa Baraza la Wawekezaji wa Kifaransa barani Afrika, Etienne GIROS
akizungumza na waandishi wa habari wa Tanzania walipotembelea ofisini
kwake jijini Paris, Ufaransa. Kushoto ni mtaalamu wa baraza hilo kwa
ukanda wa kusini mwa Afrika, Laurent Padoux.
Ufaransa imekanusha taarifa za kuyumba kwa uchumi wao na kusisitiza kuwa bado uko imara katika maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari kutoka Tanzania
waliotembelea Paris, mkurugenzi wa Idara ya Habari wa Wizara ya Mambo
ya Nje, Gael Veyssiere alisema taarifa hizo ni propaganda za
kiushindani.
Alisema ufaransa haiendeshwi kwa kuangalia takwimu
za dunia na tafiti za nje kwani, licha ya takwimu zilizotolewa hakuna
lililobadilika ndani ya nchi na hata kwa wananchi wake.
Veyssiere, ambaye idara yake iliratibu ziara hiyo,
alisema wataendelea kuyasaidia mataifa mengine katika shughuli za
kijamii na uchumi kwa ajili ya kuifanya dunia kuwa sehemu bora na salama
ya kuishi binadamu wote.
Alisema Ufaransa imewekeza vya kutosha kuhakikisha
uchumi wake hauathiri maisha ya wananchi na kusisitiza kuwa propaganda
za washindani wao, zina nia ya kuwavunja moyo.
Alisema Ufaransa imeendelea kuzalisha na kuuza nje
bidhaa zake kwa kiwango cha kuridhisha, na endapo kutatokea tatizo la
uchumi, inaweza kujikwamua bila kuathiri wengine.
Uchumi wa Ufaransa unategemea zaidi viwanda, ikiwa
inatengeneza ndege, magari, treni za kasi, pamoja na uuzaji wa nishati
kwa baadhi ya nchi za Ulaya.
Utalii wake huchangia kiasi kidogo licha ya kuwapo kwa idadi kubwa ya watalii ambao hutembelea jiji la Paris.
Ufaransa ni ya tano kwa utajiri duniani na ya pili kwa nchi za Ulaya ikiongozwa na Ujerumani.

No comments:
Post a Comment