
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas (pichani), jana
alisema kuwa mtuhumiwa huyo aliuawa juzi saa 5:30 usiku katika
barabara ya Arusha- Babati eneo la Kisongo, wilayani Monduli, wakati
wakimpeleka kijijini alikozaliwa Chemchem, wilaya ya Kondoa, mkoa
Dodoma, kuwaonyesha askari bomu jingine aliloficha.
Alidai kuwa, mtuhumiwa huyo ambaye inadaiwa wakati wa uhai wake
alikuwa mwalimu wa karate na judo ni mwasisi na kinara wa matukio ya
ugaidi yaliyotokea jijini Arusha, Zanzibar, Mwanza na Dar es Salaam.
“Huyu tulimpata kutokana na intelejensia imara ya polisi ya kisasa
na ya hali ya juu na tulimkamata mkoani Morogoro Oktoba 6, mwaka huu na
kusafirishwa Oktoba 11 mwaka huu kuletwa Arusha na alipohojiwa alikiri
kuhusika na kuratibu matukio ya ugaidi na alikuwa akijificha kwenye
nyumba tofauti na porini, ” alisema kamanda huyo.
Alidai mtuhumiwa huyo alipigwa risasi kwenye mguu wa kulia na kalio
la kulia alipojaribu kutumia uzoefu wake wa kuruka judo na kupiga
karate kutaka kuwazidi polisi ili atoroke na kwamba alifia njiani wakati
akipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwa matibabu.
Hata hivyo, hakueleza sababu za kumpiga risasi mtuhumiwa huyo
ambaye hakuwa na silaha yoyote na kama alijeruhi askari yeyote zaidi ya
kudai kuwa maiti yake imehifadhiwa hospitalini hapo kwa uchunguzi zaidi
na kusubiri ndugu kuichukua kwa maziko.
Vile vile Kamanda Sabas hakueleza kama hatua ya kuuawa kwa
mtuhumiwa huyo muhimu itawakosesha polisi taarifa muhimu katika mchakato
wa upelelezi wao.
Awali Kamanda huyo alitaja baadhi ya matukio ambayo mtuhumiwa huyo
inadaiwa alikiri kuhusika nayo kuwa ni la Oktoba 25 mwaka 2012
lililotokea saa 5:30 usiku katika mtaa wa Kanisani Paloti, kata ya
Sokoini One, jijini Arusha.
Katika tukio hilo, yeye na wenzake inadaiwa walitega bomu kwenye
chumba cha Sheikh Abdulkarim Idd Jonjo (52) nyumbani kwake na kumjeruhi
baada ya kulipuka.
Inadaiwa tukio la pili na wenzake ambao wamefikishwa mahakamani,
lilitokea Mei 5 mwaka jana saa 10:30 maeneo ya Kanisa la Katoliki la
Mtakatifu Joseph Mfanyakazi lililopo Olasiti jijini Arusha.
Katika tukio hilo inadaiwa kuwa aliratibu kurushwa kwa bomu na kusababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi 56.
Juni 15 mwaka 2013 saa 11:50 jioni katika viwanja vya Soweto, kata
ya Kaloleni, jijini Arusha na wenzake, wanadaiwa kurusha bomu na kuua
watu wanne, kujeruhi 60.
Julai 11 mwaka 2013 saa 5:00 eneo la Kwa Mrombo, jijini Arusha na
wenzake wanadaiwa walimwagia tindikali usoni Sheikh Said Juma Makamba.
Februari 12 mwaka 2014 saa 3:45 katika eneo la Tindigani, Unga
Ltd, jijini humo, kwenye msikiti wa Sawiyatu Qadiria, wanadaiwa
kumwagia tindikali usoni Sheikh Hassan Bashir.
Februari 28 mwaka 2014 saa 5:15 alfajiri katika msikiti wa
Bondeni, wanadaiwa kumwagia tindikali Mistapha Mohamed Kiago na
kumjeruhi usoni na shingoni.
Aprili 13 mwaka 2014 saa 1:30 usiku, eneo la Mianzini kwenye nyumba
ya wageni na Baa ya Niht Park, wanadaiwa walirusha bomu na kujeruhi
watu 11 na kusababisha kifo cha mmoja.
Aprili 13 mwaka 2014 la saa 5:00 katika eneo la Majengo, jijini
Arusha, anadaiwa alirusha bomu kwa kushirikiana na wenzake na kuwajeruhi
watu wawili Sudi Ali Sudi (37) ambaye ni Mkurugenzi wa Answar Muslim
Kanda ya Kaskazini na mwenzake Muhaji Hussein Kifea (38), mkazi wa Dar
es Salaam. Julai 7 mwaka huu, saa 4:15 usiku eneo la
Uzunguni, mgahawa wa Vama Traditional Indian, uliopo jirani na
Viwanja vya Gymkhana, wanadaiwa walirusha bomu na kujeruhi watu wanane.
Kamanda huyo polisi alisema wanaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine
wanaojihusisha na kikundi hicho ambacho mtuhumiwa huyo alikiri
kuendesha mafunzo ya karate na judo kwenye baadhi ya misikiti jijini
Arusha.
Hata hivyo, alisema vikundi hivyo vimesambaratishwa na polisi.
Alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa polisi ili kuendelea kudumisha amani jijini Arusha na maeneo mengine ya nchini.
“Hawa watu hawakuwa wanafadhiliwa nje ya nchi ila walikuwa
wanajifadhili wenyewe na kwa faida zao wenyewe” alisema Kamanda Sabas.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment