Social Icons

Pages

Monday, October 20, 2014

LIONS INTERNATIONAL YATOA BILIONI 20/- KUOKOA WATOTO

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid (kulia), akifurahia jambo na Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Surua na Rubella Tanzania kutoka Klabu ya Lions International, Abdul Majeed Khan, baada ya kuzindua kampeni ya chanjo dhidi ya surua na rubella mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.
Klabu ya Lions Internation, imechangia takribani Sh. billioni 20 (sawa na Dola milioni 12 za Marekani) katika kampeni shirikishi ya chanjo ya surua-rubella.Chanjo hiyo imelenga kufikia watoto zaidi ya milioni 20 nchini kote.
Katika kampeni hiyo ya siku saba iliyoanza Oktoba 18, mwezi huu, watoto wenye umri kati ya miezi tisa na miaka kumi na mitano watapata chanjo hiyo ikiambatana na matone ya vitamin A na dawa za minyoo tumbo huku watu wazima wakipata kinga tiba dhidi ya matende, mabusha, ngiri maji pamoja na minyoo.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Mratibu wa surua-rubella wa klabu ya Lions nchini, Abdul Majeed Khan, alisema ushiriki wa klabu yake ni ishara kuwa taasisi za huduma nchini zina wajibu wa kuchangia katika kuboresha afya za Watanzania.
“Ni matumaini yetu kuwa kwa mchango wetu huu na michango ya wadau wengine wa masuala ya afya kwa ajili ya kampeni hii, itawezesha kufikia angalau watoto milioni 21 na kuwakinga na magonjwa haya hatarishi," alisema.
Naye Gavana mstaafu mwenzake, Wilson Ndesanjo, alisema kuwa kupitia wanachama wake waliotapakaa duniani kote, Lions ilikusanya Dola milioni 7.5 za Marekani (sawa na Sh. bilioni 12.37) huku kiasi kingine kikichangiwa na umoja wa Global Alliance for Vaccines and Immunizations (Gavi).
Pamoja na shughuli nyingine, klabu ya Lions Tanzania imekuwa ikichangia katika kuboresha sekta ya maji nchini kwa kuchimba visima shuleni na vijijini.
Katika sekta ya afya, Klabu ya Lions hutoa huduma ya upimaji wa afya ya macho na utoaji wa miwani bure kwa wagonjwa.
Hata hivyo, watu wenye ulemavu wa kutokusikia na walemavu wa kutokuongea, pia hupatiwa huduma mbali na kuwezesha watoto wenye matatizo ya moyo kupelekwa nchini India kwa upasuaji.
Hadi sasa watoto 3,000 tayari wamenufaika na huduma hiyo.
Hata hivyo, kampeni hiyo ya chanjo ya surua-rubela, inalenga watoto wote hata ambao walikwisha chanjwa huko nyuma.
Hii inatokana na Tanzania imekuwa mara kwa mara ikishuhudia milipuko ya magonjwa hayo na mlipuko mkubwa wa hivi karibuni ulitokea mwaka jana wilayani Kwimba, Mwanza ambako watu zaidi ya 200 waliathiriwa.
Hata hivyo, ni mara ya kwanza kwa Tanzania kutoa chanjo ya rubella na ni nchi ya kwanza Afrika kutoa chanjo moja kwa ajili ya surua na rubella yenye mchanganyiko ya dawa mbili.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Neema Rusibamayila, alisema kwa sababu magonjwa ya surua na rubella yana dalili zinazofanana, ni muhimu kuchanja yote kwa pamoja ili kuendelea kulinda afya za watoto na kupunguza vifo vya utotoni.
Aliongeza kuwa kati ya mwaka 2010 na 2012, asilimia tisa ya watoto wote waliodhaniwa kuwa na surua waligundulika kuugua rubellla.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: