Social Icons

Pages

Wednesday, August 13, 2014

MJUMBE ALIYEJERUHIWA APIGA KURA WODINI

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Kundi la 201, Thomas Mgoli akiwa amelazwa katika Hospital ya Mkoa wa Dodoma, jana. Picha na Emmanuel Herman

Kamati namba 12 inayoongozwa na mwanasiasa mkongwe, Paul Kimiti, imelazimika kuhamia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kumwezesha kupiga kura, Thomas Markus Mgoli, aliyelazwa hospitalini hapo akipatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kipigo na watu wasiojulikana juzi usiku.
Mgoli, ambaye ni Mjumbe wa Bunge hilo kutoka kundi la 201 akiwakilisha Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), alilazimika kuzipigia kura sura ya pili, ya tatu, ya nne na sura ya tano ya Rasimu ya Katiba akiwa hospitalini hapo jana ili kukamilisha zoezi zima la upigaji wa kura kwa wajumbe.
Hata hivyo, Mgoli alipiga kura ya kuikataa ibara ya 39 ya Rasimu ya Katiba inayozungumzia mlemavu kuruhusiwa kuingia gerezani akiwa na magongo ya kutembelea kwa kuwa yakitumika vibaya yanaweza kuleta madhara kwa wengine.
NIPASHE lilishuhudia kazi hiyo ya upigaji wa kura hospitalini hapo ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Thuwayba Kissasi, saa 8: 46 mchana, katika wodi namba 18 ya daraja la kwanza alikolazwa.
Mgoli alilazwa hospitalini hapo juzi baada ya kuvamiwa na watu wanne wasiojulikana wakati akitokea kununua vinywaji katika grosary moja (Jina Limehifadhiwa)  iliyopo eneo la Area A, karibu na Shule ya Msingi Chamwino, Manispaa ya Dodoma.
Mjumbe huyo alipata kipigo hicho baada ya watu hao kudaiwa kumhoji uhalali wake wa kuwapo Dodoma kuendelea na Bunge Maalum la Katiba, wakimweleza kwamba yeye (Mgoli) ni kibaraka wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kwamba hawatakubali aendelee na hayo wanayoyafanya.
Akizungumzia mkasa huo hospitalini, mjumbe huyo alisema hakuna haja ya kuuana wala kuumizana ila ni vyema ikafika mahali, Watanzania tukubali kutokubaliana na tujenge misingi ya maridhiano.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Mzee Nassor, aliiambia NIPASHE jana kwamba, afya ya mjumbe huyo kwa sasa imeanza kuimarika na anaendelea vizuri na matibabu.
“Afya yake inaimarika  na anaendelea vizuri, amefanyiwa vipimo, bado tunaendelea kumwangalia hali yake,”alisema.

JESHI LA MAGEREZA HALIJATAJWA
Wakati Bunge hilo likiendelea kuchambua Rasimu itakayopendekezwa kuwa Katiba mpya, imebainika Jeshi la Magereza halikutajwa katika vyombo vya ulinzi na usalama wa Jamhuri ya Muungano katika rasimu hiyo.
Vyombo vilivyoainishwa kwenye Sura ya 15, 236(1) ya Rasimu ya Pili, inayojadiliwa kwenye Kamati 10 za Bunge Maalum, ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano na Idara ya Usalama wa Taifa.
Hata wajumbe wa Baraza la Ulinzi na Usalama waliotajwa kwenye sura hiyo ya Rasimu, 237(1) ni pamoja na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, huku Kamishna wa Magereza akiwa hatajwi.
Kufuatia taarifa zilizolifikia NIPASHE kuwa Magereza inatakiwa kuingizwa kwenye Katiba ijayo, ililazimika kupata ufafanuzi kutoka kwa mmoja wa makamishna wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kuhusu Sura na vipengele hivyo.
Akizungumza kwa simu, Prof. Paramagamba Kabudi, alisema kutokuwapo jeshi wala kamishna wa Magereza katika Rasimu ya Pili ni sahihi kwasababu siyo suala la Muungano.
“Tanzania Bara kuna Magereza, Zanzibar kuna Kikosi Mafunzo, sasa kwanini watake Magereza iingizwe kwenye Katiba ilhali kwa upande wa Zanzibar hakijaingizwa?,”  alisema Prof. Kabudi
Prof. Kabudi alitahadharisha kuwa, ikitokea jeshi mambo mengine yasiyo ya muungano kama vile ardhi yakiingizwa kwenye Rasimu itakayopendekezwa kuwa Katiba ijayo ya Muungano, kitakachokuwa kimeandikwa siyo Katiba ya Muungano Tanganyika bali ya Tanganyika.
Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, hata Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hakuweka masuala ya Tanganyika kwenye Katibu ya Jamhuri ya Muungano bali yalitungiwa sheria, kuhusu namna yatakavyoshughulikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Aidha, alisema hoja kwamba umuhimu wa jeshi hilo kuingizwa kwenye Katiba inayoandikwa unakolezwa na mafunzo kuanzia ngazi ya ofisa kwa watumishi wa Magereza kutolewa kwa pamoja na Tanzania Bara, alisema haina msingi kwakuwa kuna watumishi wengi hata wa nchi za nje ambao hupata mafunzo nchini wakati hakuna uhusiano wa kimuungano na nchi wanazotokea.
Akizungumzia dhana ya uhitaji wa huduma za Jeshi la Magereza katika mahakama za Jamhuri ya Muungano, bila kufafanua alisema suala hilo linajibiwa katika Sura ya 10 ya Rasimu inayojadiliwa.

URAIA PACHA

Raia waishio nje ya nchi wametuma waraka maalumu unaohusu uraia pacha, wakiomba ujadiliwe ndani ya kamati za Bunge Maalumu la Katiba.Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad, alisema jana kuwa, raia hao walituma waraka huo kupitia kwa mtaalamu wao ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge hilo kupitia wateule wa Rais 201, Kadari Singo.  
“Juzi walimtuma mtaalamu wao Singo ili alete waraka huo na niliomba kibali kwa mwenyekiti ili waraka huo uruhusiwe kujadiliwa ndani ya kamati na alipata ruhusa hiyo,’’ alisema katibu.
Alisema hadi juzi mchana kamati tatu zilikuwa zikiendelea kujadili ibara inayohusu uraia pacha na kamati zingine zimekamilisha kujadili ibara hiyo.  
Alisema hivi sasa wajumbe hao wanaendelea kama kawaida kujadili sura mbalimbali ndani ya kamati ikiwamo kupitia ibara inayohusu masuala ya uraia wa nchi mbili.
Aidha, alisema baadhi ya wajumbe wa bunge hilo toka katika kundi la wajumbe 201 wamerejea bungeni na kuendelea na majadiliano ya kamati kama kawaida.  
Naye mwenyekiti wa kamati namba 12 Paul Kimiti alisema kamati yake imekuwa ikijadili suala hilo la uraia pacha kwa kina.
Alisema hata hivyo ibara hiyo imekuwa na mvutano hasa kwa upande wa Zanzibar ambapo baadhi ya wajumbe wamekuwa na hisia tofauti kuhusiana na kuruhusu uraia pacha kwa upande wa Zanzibar.  
Kimiti alisema baadhi ya wajumbe wameonyesha hofu kufuatia baadhi ya watu ambao walitoroka nje ya nchi wakati wa mapinduzi na hivyo kuruhusiwa kuwa na uraia pacha kunaweza kuleta matatizo.
Hata hivyo, alisema wajumbe hao walikubaliana kuwapo kwa uraia pacha kwa hao waliotoroka nje wakati wa mapinduzi na wanaweza kudhibitiwa katika sheria itakayotungwa.
Akizungumzia hali ya majadiliano ndani ya kamati, Kimiti alisema wajumbe wamekuwa wakijadili kwa amani na utulivu.
Alisema inaonyesha kuwa sura zilizokuwa zikileta mgogoro ni zile zilizokuwa zikihusu muundo wa serikali kwani kwa sasa wamekuwa wakiendelea bila tatizo.

Chanzo: NIPASHE

No comments: