 
Rais Barack Obama leo anakutana na viongozi wa baraza la Congress, 
lakini anakabiliana na hadhara tofauti kabisa, licha ya kuwa orodha ya 
wageni wake hao haijabadilika.
Mkutano wa rais Obama na viongozi wa baraza la wawakilishji na seneti ni
 wa kwanza tangu pale baraza la Congress linalodhibitiwa na chama cha 
Republican kufanya kikao chake cha kwanza wiki iliyopita. Kiongozi wa maseneta wa chama cha Democratic Harry Reid , mshirika wa 
siku nyingi wa rais Obama katika baraza la seneti, alishushwa cheo 
katika uchaguzi wa Novemba mwaka jana na kuwa kiongozi wa wachache 
katika seneti. Kiongozi wa upinzani Mitch McConnel , ambaye ni mwiba 
katika upande wa Obama kama kiongozi wa wachache katika baraza la seneti
 , sasa amechukua wadhifa wa zamani wa Reid katika baraza hilo la juu.
Mazungumzo ya fursa za ushirikiano
Watu hao watatu watajiunga na spika wa bunge John Boehmer na kiongozi wa
 wabunge wa chama cha Democratic Nancy Pelosi katika ofisi ya rais 
kujadili fursa za uwezekano wa ushirikiano kati ya chama cha Democratic 
na Republican mwaka huu. Hata hivyo haifahamiki bado kwamba vyama hivyo viwili vitaweza kufumbia 
macho tofauti zao za wazi katika masuala kadhaa na kuangalia katika 
maeneo machache ya msimamo wa pamoja. Vyama vyote viwili vilimaliza uchaguzi wa muhula wa kati mwaka jana 
vikizungumzia kwa matarajio juu ya kufanyakazi kwa pamoja kuhusiana na 
mageuzi ya kodi, kukuza biashara na maendeleo ya miundo mbinu - maeneo 
ambayo Obama na Warepublican wanaweza kwa kiasi fulani kukubaliana. Lakini mwanzoni mwa mwaka huu umetamalaki kwa kiasi kikubwa na mapambano
 yale ambayo yanatambuliwa kuhusiana na bomba la Keystone XL, hatua za 
Obama kuhusu wahamiaji pamoja na sera zake za mambo ya kigeni.
Nafasi ya maafikiano
Katika muda wa wiki mbili zilizopita, Obama mara kwa mara ametishia 
kuchukua hatua ya kutumia kura yake ya turufu kuzuwia miswada ambayo 
Warepublican wameiwasilisha kama masuala yao ya umbele. Hata hivyo , msemaji wa Ikulu ya Marekani Josh Earnest amesema kuna " 
mambo chungu nzima" ambayo Obama anaweza kuyafanya mwaka huu pamoja na 
Warepublican. "Haina maana tutakubaliana na kila kitu - kwa hakika hilo haliwezekani,"
 amesema Earnest. " Lakini suala ni kwamba , tutaruhusu hali ya 
kutokubaliana kuhusu masuala machache na kuwa chachu cha kufikiwa 
makubaliano mengine yote. "Rais anahakika kwamba hilo halitatokea," ameongeza. Haijafahamika wazi iwapo Reid atahudhuria kikao hicho. Anapata nafuu 
kutokana na maumivu yanayohusiana na mazowezi na msemaji wake amekataa 
kusema iwapo atakuwapo katika mkutano huo.
CHANZO: DW KISWAHILI 
 

No comments:
Post a Comment