 
Rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud Abbas anakamilisha miaka
 10 madarakani Alhamisi akiipa changamoto kubwa Israel. 
Atakutana na viongozi wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu Cairo, Misri.
Baada ya muongo mmoja uongozini kiongozi huyo hana mengi ya kujivunia 
kwani bado angali mbali sana kuufikia mkataba wa kuundwa dola huru la 
Palestina. Abbas ameshindwa kuukomboa Ukanda wa Gaza kutoka kwa 
wapinzani wake kisiasa, chama cha Hamas, na anaonekana na wengi kama 
mlinzi wa masilahi ya kiusalama ya Israel katika Ukingo wa Magharibi. Abbas mwenye umri wa miaka 79 anayejulikana kwa jina la utani "Abu 
Mazen" alibadili mkondo siku chache kabla kuadhimisha miaka kumi 
madarakani Alhamisi wiki hii kwa kusaini mkataba wa kutaka kujiunga na 
mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC. Hatua hiyo yumkini ikaruhusu 
malalamiko na mashtaka ya uhalifu wa kivita dhidi ya Israel katika kile 
ambacho wengi wanaamini ni mkakati wa mwisho wa kiongozi huyo. Hatua ya kujiunga na mahakama ya ICC ni sehemu ya mkakati mpana ambao 
Wapalestina wanatumai utaleta shinikizo la kimataifa dhidi ya Israel na 
kuimarisha nafasi yao katika mazungumzo ya kudai taifa lao huru katika 
siku za usoni. Wapalestina wanasema hatua hiyo imetokana na hali ya 
kukata tamaa kufuatia miongo miwili ya kushindwa kwa mazungumzo ya 
kutafuta amani yaliyosimamiwa na mshirika mkubwa wa Israel, Marekani.
Abbas lawamani
Israel inamlaumu Abbas kwa kujaribu kutumia kampeni ya kulifanya taifa 
la Kiyahudi kuwa lisilo halali badala ya kuendelea na mazungumzo. Hatua 
hiyo ina athari zisizo mithili, lakini maafisa wa Palestina wanasema 
rais Abbas alilazimika kuchukua hatua. "Sisi tuwadhaifu na njia pekee tunayoweza kuitumia ni kurejesha harakati
 za kuitetea Palestina kwa jumuiya ya kimatiafa," alisema afisa mmoja wa
 ngazi ya juu aliyezungumza bila kutaka kutajwa jina akielezea maoni 
binafsi ya rais Abbas.
Wapalestina walio karibu na Abbas wanasema amekuwa chini ya shinikizo 
nchini kukabiliana na Israel tangu vita vya siku 50 vya msimu wa 
kiangazi mwaka uliopita katika Ukanda wa Gaza kati ya Israel na kundi la
 Hamas ambapo zaidi ya Wapalestina 2,200 waliuwawa, wengi wao raia, 
pamoja na watu 72 upande wa Israel. Alikuwa na chaguo ima awasikilize watu na uongozi na washauri wake, au 
ajitenge mwenyewe zaidi," amesema Hanas Ashrawi, afisa mwandamizi wa 
Chama cha Ukombozi wa Palestina, PLO, ambaye mara kwa mara hupewa 
taarifa na rais Abbas.
Abbas atakuwa Cairo
Katika siku ya maadhimisho ya miaka 10 madarakani, Abbas aliyeapishwa 
mnamo Januri 15 mwaka 2005, atakuwa mjini Cairo nchini Misri, kuwasihi 
viongozi wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu watimize ahadi yao kuipa mamlaka 
ya ndani ya Palestina euro milioni 100 kufidia pengo lililosababisha na 
hatua ya Israel kuzuia malipo ya kila mwezi ya kiasi cha dola milioni 
120 kama kodi inayotozwa na Israel kwa niaba ya Wapalestina, kwa hatua 
yake ya kujiunga na ICC. Mataifa ya kiarabu yameshawahi kuzivunja ahadi 
za aina hiyo katika siku za nyuma. Iwapo mamlaka ya ndani ya Wapalestina itasambaratika kutokana na 
matatizo ya kifedha yaliyosababishwa na vikwazo vilivyowekwa na Israel, 
Israel kama nchi inayoyakalia maeneo ya Wapalestina itakuwa na dhamana 
ya kutoa huduma kwa Wapalestina, kibarua ambacho kina gharama kubwa. 
Israel pia itapoteza ushirikiano na Abbas katika masuala ya usalama, 
ambao umesaidia sana kuepusha mashambulizi ya wanamgambo. Nathan Thrall mchambuzi wa shirika la kimataifa la kukabiliana na 
mizozo, ICG, amesema anaamini Israel inataka mamlaka ya ndani ya 
Palestina kuendelea na shughuli zake na haitamchukulia Abbas hatua kali 
mno. Kwa kujiunga na mahakama ya ICC, Abbas pia alilitilia maanani suala
 hilo. Abbas hajatangaza nia ya kuondoka madarakani. Waziri mkuu wa Israel 
Benjamin Netanyahu naye kwa upande wake anatafuta kuchaguliwa tena kwa 
awamu ya tatu katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Machi 17 mwaka huu. 
Iwapo Netanyahu atashinda, rais Abbas ataimarisha kampeni ya kutaka 
utambulisho zaidi wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi, Ukanda wa 
Gaza na Jerusalem Mashariki, maeneo yaliyotekwa na Israel mwaka 1967.
CHANZO: DW KISWAHILI 
 

No comments:
Post a Comment