Kansela Angela Merkel na Rais Joachim Gauck wa Ujerumani Jumanne wanashiriki katika maandamano ya kutetea uvumilivu katika
jamii na kupinga vuguvugu la maandamano linalozidi kukua dhidi ya
Uislamu nchini Ujerumani.
Mbali na Rais Gauck ambaye atayahutubia maandamano hayo yatakayofanyika
jioni ya leo katika eneo la kihistoria la Lango la Brandeburg katika mji
mkuu wa Ujerumani Berlin mawaziri wengi wa serikali ya Merkel pia
wanatarajiwa kuhuhudhuria.
Hapo jana Merkel alisisitiza kwamba Uislamu ni sehemu ya Ujerumani yeye
pamoja na Rais Gauck wamelishutumu kundi la Wazalendo wa Ulaya dhidi ya
Kusilimishwa kwa Ulaya PEGIDA kwa kutaka kuigawa jamii ya Ujerumani na
kufanya hivyo kwa kutumia vibaya kwa faida yao hufo walio nayo wananchi
katika suala la uhamiaji,ugaidi na Waislamu wa itikadi kali.
Maandamano hayo ya leo yanakusudia kujibu yale yanayofanyika kila wiki
katika mji wa mashariki wa Ujerumani wa Dresden yanayoandaliwa na kundi
la PEGIDA ambapo Jumatatu yalihudhuriwa na watu 25,000 huku maandamano
dhidi ya kundi hilo nayo yakifanyika nchi nzima na kuhudhuriwa na watu
zaidi ya 100,000.
Ujumbe wa amani na uvumilivu
Wakiyatangaza maandamano hayo ya Jumanne Baraza la Waislamu
nchini Ujerumani na Jumuiya ya Waturuki mjini Berlin zimesema Waislamu
nchini Ujerumani wanalaani kwa nguvu zote mashambulizi ya kigaidi ya
kuchukiza yaliotokea nchini Ufaransa na kwamba wanataka kuonyesha
mshikamano wao na wahanga wa Ufaransa.
Zimesema kwa kutumia maandamano hayo wanataka kutuma ujumbe wa amani na
uvumilivu,ujumbe dhidi ya chuki na matumizi ya nguvu kwa ajili ya
Ujerumani yenye mchanganyiko wa watu ambayo inaheshimu na kulinda uhuru
wa kujieleza na dini.
Katika maoni ya mtandaoni ya gazeti mashuhuri la Spiegel nchini
Ujerumani Kansela Merkel amepongezwa kwa kutocheza mchezo wa ghilba
ambapo katika hotuba yake ya mwaka mpya alikuwa mstari wa mbele wa
kupinga vuguvugu la PEGIDA kwa kuwalaani viongozi wa kundi hilo kwa kuwa
watu wasiopenda maangiliano na hata waliojaa chuki nyoyoni.Ameonyesha
msimamo wa wazi wa unaostahiki kutukuzwa wa kupinga chuki dhidi ya
Uislamu.
Vuguvugu la PEGIDA
Maandamano ya PEGIDA na mengine madogo kama hayo yamechochewa
na kile kinachoelezwa kuwa ongezeko kubwa la idadi ya wakimbizi
nwanaotafuta hifadhi ya kisiasa nchini jambo lililoifanya serikali
kuhangaika kuwatafutia makaazi katika majengo ya shule,maofisi na
kuwaweka pia katika makontena vijijini.
Mwaka jana Ujerumani ilipokea zaidi ya maombi 180,000 ya watu wanaotaka
hifadhi likiwa ni ongezeko la asilimia 57 kutoka mwaka 2013 na wengi wao
walikuwa wanatokea Syria,Afghanistan, Iraq,Eritrea na Somalia na pia
kutoka nchi kadhaa za Balkan. Ujerumani ina takriban wakaazi milioni nne wa Kiislamu sawa na kama asilimia tano ya wananchi wake milioni themanini.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment