Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga.
Idadi ya wakimbizi waliopo katika kambi ya
Nyarugusu, Kigoma imezidi kuongezeka na kufikia 51,095 huku 32 wakilazwa
kutokana na kuugua ugonjwa wa kipindupindu.
Wagonjwa hao ni waliolazwa katika kambi hiyo pamoja na wale waliopo uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga,
alisema vifo vya wagonjwa wa kipindupindu havijatokea tena katika siku
tatu za hivi karibuni baada ya ugonjwa huo kudhibitiwa.
“Kutokana na ushirikiano kati ya mashirika ya kimataifa pamoja na
madaktari wasio na mipaka, Wizara ya Afya tumedhibiti ugonjwa na idadi
ya vifo kupungua,” alisema.
Alisema katika eneo la kituo cha uhamiaji cha Manyovu kuna raia 208
ambao wameingia nchini kupitia barabara kuu ya Burundi-Tanzania
wakisubiri kupelekwa katika kambi ya Nyarugusu kwa ajili ya usajili.
Idadi ya raia wanaoingia nchini wakitokea Burundi imezidi
kuongezeka kutokana na raia hao kukimbia machafuko na vurugu kupinga
msimamo wa Rais Pierre Nkurunziza kutaka kugombea nafasi ya urais kwa
muhula wa tatu.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment