Mbunge wa Kisesa mkoani Simiyu, Luhaga Mpina akitangaza nia yake ya
kugombea urais katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa
Shule ya Msingi Mwandoya, wilayani Maswa, mkoani Simuyu jana.
Idadi ya makada wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaoshiriki mbio za kuingia Ikulu imezidi
kuongezeka, baada ya Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kueleza kuwa
atachukua fomu za kuwania urais mwaka huu.
Mpina ni mtu wa 11 ndani ya CCM kutangaza nia ya
kutaka kugombea urais hadi jana, baada ya Mbunge wa Monduli, Edward
Lowassa, Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Bunda,
Stephen Wasira.
Makada wengine wa CCM waliokwishatangaza nia ya
kuwania urais ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Makongoro
Nyerere, Waziri katika Ofisi ya Rais, Kazi (Maalumu) na Mbunge wa Rungwe
Mashariki, Profesa Mark Mwandosya na Balozi Ali Karume.
Wengine waliotangaza awali ni Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis
Kigwangalla na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Mpina alitangaza nia ya kuchukua fomu za kuwania
urais alipokuwa akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mwandoya jimboni Kisesa
mkoani Simiyu.
Alisema atachukua fomu za kuomba ridhaa ya kuwania
urais kwa tiketi ya CCM ili atekeleze vipaumbele kadhaa, ikiwamo
kusimamia makusanyo ya kodi itokanayo na rasilimali za Taifa. Alisema
amefikia uamuzi huo baada ya kujipima na kuona kuwa anafaa.
Mpina ambaye amekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa
miaka 10 kupitia CCM, alisema Tanzania ina uchumi mzuri ila unaharibiwa
na mfumo wa utawala.
Vipaumbele vyake
Mpina alieleza kuwa kama atapata ridhaa ya kuwa
rais, atahakikisha makusanyo ya kodi yanaongezeka mara tatu
ikilinganishwa na hali ya makusanyo ya sasa.
“Kwa sasa Taifa linakusanya Sh12 trilioni kwa
mwaka, lakini mimi nitahakikisha makusanyo hayo yanaongezeka mara tatu
ya hapo. Sasa makusanyo yanashindikana kutokana na kuwapo kwa mianya
mingi ambayo inaruhusu wizi wa mali za umma,” alisema.
Alisema Tanzania siyo maskini ila umaskini uliopo
unasababishwa na ubadhirifu wa fedha za umma, wizi, matumizi mabaya ya
madaraka na mikataba mibovu inayofanywa na watu binafsi na serikali.
“Mambo haya nitayakomesha ndani ya muda mfupi, nikiingia madarakani kwa kutumia mfumo na kanuni mpya,” alisema.
Harakati za kisiasa
“Zaidi ya asilimia mbili ya GDP zinatoroshwa kwenda nje ya nchi
na wala wanaohusika na wizi huo hawachukuliwi hatua ingawa wanafahamika.
Sasa natuma salam kwa watu hao katika Serikali yangu wajiandae
kurejesha fedha hizo ambazo ni zaidi ya Sh2 trilioni,” alisema Mpina.
Mpina alieleza kuwashangaa makada wenzake
wanaotangaza nia na kutangulia kusema watafanya mambo fulani bila
kueleza wapi watapata fedha akihoji watatekelezaje miradi hiyo?
Alibainisha kuwa ukisema utaendeleza au kufanya
mradi fulani bila kueleza utapata wapi fedha, maana yake ni kuendelea
kuifanya nchi iwe tegemezi kwa mataifa ya nje.
“Katika Serikali yangu sitasubiri watu kutoka nje
kuwekeza, bali nchi yenyewe itakuwa mstari wa mbele kutoa fursa kwa
wazawa kuwekeza na kuendeleza uchumi,” alisema.
Mpina alisema baada ya kutengeneza msingi mzuri wa
mapato ya Serikali ataimarisha suala la huduma za afya kwa maana ya
kujenga na kuboresha vituo vya afya na hospitali.
“Pia nitaangalia mfumo mzima wa elimu na kuufanya
uweze kuleta tija kwa Watanzania wote. Nitaangalia pia suala la viwanda
kwa karibu zaidi,” alisema.
Mpina alisema atahakikisha anarudisha viwanda vyote vilivyobinafsishwa mikononi mwa umma ili viweze kutoa ajira kwa Watanzania.
Wakizungumza baada ya mkutano huo, wananchi wa
jimbo hilo walisema hawana wasiwasi na Mpina kuwa mgombea urais na
kwamba hata fedha za kuchukua fomu watamchangia kutokana na imani
waliyonayo juu yake. “Tunamruhusu achukue fomu ya kugombea,
tutamchangia fedha kwani tunaamini utendaji kazi wake,” alisema mkazi wa
Maswa, Salum Makoye.
Katibu CCM Wilaya ya Maswa, Jonathan Mabihya
aliwataka wananchi kufanya uamuzi sahihi kuchagua viongozi bora wakati
wa uchaguzi mkuu. “Uongozi siyo suala la majaribio, msikosee.
Chagueni viongozi ambao watawaletea maendeleo, vinginevyo mtajutia
uamuzi wenu kwa kipindi cha miaka mitano.
Harakati za kisiasa
Mpina alianza kujishughulisha na masuala ya siasa akiwa Chuo
Kikuu baada ya yeye na vijana wenzake kuweka mkakati wa kukiimarisha
Chama cha Mapinduzi kwa wanachuo wengine ambao hawakuwa wanachama wa
chama hicho.
Mwaka 2003 muda mfupi baada ya kurejea kutoka
masomoni, alifikia kwenye uchaguzi wa Umoja wa Vijana wa CCM ambako
aligombea na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti Wilaya ya Meatu.
Mwaka mmoja baadaye akiwa ni mwenyekiti wa vijana
wa wilaya na mfanyakazi wa halmashauri ya wilaya hiyo, alijitosa kwenye
uchaguzi wa ubunge na kushinda nafasi ambayo bado anaishikilia hadi
sasa.
Ndani ya Bunge, Mpina anashikilia nafasi ya
kamishina wa vyuo vikuu, mbunge wa Bunge la Afrika na Mwenyekiti wa
Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge.
Wakati wote amekuwa na ajenda ya kuwashughulikia
watu wanaoficha fedha nje ya nchi akilia zaidi kuhusu mabilioni ya
Uswisi ambako anataka walioficha huko watangazwe hadharani.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment