Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
imefanya marekebisho ya matangazo mawili Gazeti la Serikali, kwa
kupunguza kata za mradi wa uendelezaji wa mji wa Kigamboni, Dar es
Salaam kutoka tisa hadi sita na eneo la mradi kutoka hekta 50,934 hadi
6,494.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa pamoja
baina ya wananchi wa Kigamboni, kamati ya ufuatiliaji malalamiko ya
wananchi wa eneo hilo, Mbunge, Waziri wa Tamisemi, Mkuu wa wilaya na
wadau wengine.
Alisema ili kuondoa malalamiko ya wananchi wa eneo hilo kwa muda
mrefu, amerekebisha Tangazo la Serikali Na. 229 la mwaka 2008 lililotaja
maeneo ya mpango kuwa ni Kigamboni, Vijibweni, Mjimwema na Kibada kwa
kuongeza Kata ya Tungi na sehemu ya Kata ya Somangila katika mitaa
miwili ya Kizani na Mbwamaji ambazo hazikuwamo kwenye tangazo la awali.
Alisema pia amerekebisha Tangazo la Serikali Na. 6 la mwaka 2013
lililotaja eneo la Mpango kuwa na kata tisa kwa kupunguza ukubwa wa eneo
la Mpango kutoka hekta 50,934 hadi 6,494 na kupunguza idadi ya kata
kutoka tisa hadi sita kwa kuondoa Kata za Kisarawe II, Kimbiji na
Pembamnazi kwenye eneo la mpango.
Lukuvi alisema pia amerekebisha Tangazo la Serikali Na. 7 la mwaka
2013, lililoanzisha Mamlaka ya Uendelezaji mji Mpya wa Kigamboni (KDA)
na kutaja majukumu yake kwa kuondoa jukumu la KDA la kuwa mwendelezaji
Mkuu wa eneo la Kigamboni.
Waziri Lukuvu alifafanua kuwa katika marekebisho hayo, pia
ameridhia marekebisho ya vipengele mbalimbali, lengo likiwa ni
kukamilisha mpango wa uendelezaji Mji mpya wa Kigamboni kwa kushirikiana
na wananchi na wadau wengine na kuondoa dhana iliyokuwa imejengeka
awali kuwa Serikali ingetwaa maeneo ya wananchi, kuwahamishia mahali na
kuuza maeneo yao kwa wawekezaji kwa gharama kubwa na bila ridhaa ya
wananchi.
“Kwa mujibu wa dhana mpya, wananchi wa Kigamboni wana fursa ya
kushiriki katika uendelezaji kwa mwananchi mwenyewe kuwa mwendelezaji
katika eneo lake kwa kuzingatia mpango; mwananchi kulipwa fidia au kuuza
eneo lake kwa mwekezaji kwa hiari yake kwa kuzingatia bei ya soko na
kuingia ubia na mwekezaji kwa kutumia ardhi yake kama mtaji,”
alifafanua.
Alibainisha kuwa katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huo,
jukumu la Serikali litakuwa ni kuandaa mazingira wezeshi katika kila
hatua ya utekelezaji, na kwamba KDA itakuwa na jukumu la kuratibu wadau
mbalimbali na kusimamia utekelezaji wa mpango kwa ujumla.
Waziri huyo alisema kwa sasa serikali itaanza kutengeneza barabara
za mji huo, na kwamba kila mwananchi atakayekutwa katikati ya barabara
atalipwa fidia kwa wakati kwa kuwa zaidi ya Sh. bilioni tatu zimetegwa
kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hiyo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment