Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu) Profesa Mark Mwandosya
akiwahutubia wanaCCM katika Uwanja wa Mkapa, Mbeya jana.
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya jana alitangaza nia ya
kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kusema kesho
atachukua fomu za kuwania nafasi hiyo.
Profesa Mwandosya alisema atachukua fomu katika Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kesho saa nne asubuhi mjini Dodoma.
Akitangaza nia hiyo jijini Mbeya, Profesa
Mwandosya alianza kwa vijembe, akisema alikuwa kimya kutangaza nia hiyo
kama neema tu ya Mungu. Alisema katika maisha ni afadhali kuwa kimya
kuliko kuwa mpayukaji na mwenye uamuzi wa papo kwa papo yenye hasara kwa
Taifa.
“Mara nyingi katika maisha mjenga hoja na mtendaji
makini ni bora kuliko mpayukaji mwenye maamuzi ya papo kwa papo na
kusababisha hasara kwa Taifa,’’ alisema.
Alisema kipindi cha mpito katika Serikali nyingi
ni kigumu, hivyo misingi ya waasisi wa Taifa inachangia Watanzania
kuendelea kuwa na furaha.
CCM haiyumbi, bali wanachama
“Wapo wanaosema CCM inayumba, lakini mimi nasema
CCM haiyumbi isipokuwa baadhi ya wanachama wake ndiyo wanaoyumba mno
baada ya kukiuka kiapo cha ahadi za CCM ikiwamo inayokataza rushwa,’’
alisema na kuzisoma ahadi zote za CCM:
“Ahadi ya kwanza inasema; ‘binadamu wote ni ndugu
zangu na Afrika ni moja. Ahadi ya pili; ‘nitaitumikia nchi yangu na watu
wake wote, ya tatu; ‘nitajitolea nafsi yangu kuondosha umaskini,
ujinga, magonjwa na dhuluma’ ya nne; ‘rushwa ni adui wa haki, sitapokea
wala kutoa rushwa’.” Alisema na kueleza kwamba mbali ya ahadi hiyo,
wengi wameikiuka na hivyo wanayumba.
Alitaja ahadi nyingine kuwa ni ya tano isemayo;
‘cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida
yangu,’ ya sita; ‘nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia
elimu yangu kwa faida ya wote,’ ya saba inasema; ‘nitashirikiana na
wenzangu wote kujenga nchi yetu, ya nane; ‘nitasema kweli daima, fitina
kwangu mwiko na ya tisa inasema; ‘nitakuwa mwanachama mwaminifu wa CCM
na raia mwema wa Tanzania na Afrika.’
Profesa Mwandosya aliwaambia mamia ya wanannchi
waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Mkapa kwamba wana CCM wengi
wamekiuka ahadi hizo ambazo waliapa mbele ya Watanzania na Mungu na
kwamba ndiyo maana wanayumba wao, lakini CCM ipo imara.
Sababu za kugombea
Alisema ameamua kuingia kwenye kinyang’anyiro
hicho ili kuhakikisha Dira ya Maendeleo ya 2025 ambayo alishiriki
kuiandaa mwaka 2000, inatekelezwa na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya
uchumi wa kati na hatimaye mwaka 2050 iwe nchi ya dunia ya kwanza. “Sasa tutafikaje huko, wengi wanaweza kuuliza,” alisema na
kueleza kuwa ameandaa mambo 10 ya kutekeleza ili kufikia malengo hayo.
Profesa Mwandosya aliyataja mambo hayo kuwa ni
pamoja na kuanzisha kilimo cha kisasa na kisayansi kinachozingatia sifa
zote za kilimo cha kisasa kwa kuboresha pembejeo na miundombinu yote ya
shughuli za kilimo.
Alitaja suala la pili kuwa ni kupambana na rushwa
kwa kuondoa vikwazo vinavyozuia mapapa wa rushwa wasishughulikiwe na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Upo utaratibu kwamba kabla ya kuhojiwa, vigogo
wala rushwa, lazima Takukuru wapate kibali, lakini kwa wala rushwa
wadogowadogo wao wanakamatwa na kufikishwa mahakamani bila kizuizi
hicho, sasa hilo ni kero,’’ alisema.
Alisema akifanikiwa kupita na kuingia Ikulu,
ataboresha sheria ili vigogo wa rushwa kubwa washughulikiwe kuliko
wadogo ambao wataacha wenyewe.
Pia alisema akifanikiwa katika safari yake hiyo,
atahakikisha vyombo vya kiuchumi kama Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
mifuko ya hifadhi inapewa uhuru zaidi wa kujisimamia na kwamba Serikali
itakuwa mhimili wa uchumi ili kuwafanya Watanzania waone matunda ya
kukua kwa uchumi.
“Serikali itakuwa injini ya kukua kwa uchumi kwa
kuboresha mazingira ili sekta binafsi zifanye kazi kwa ufanisi na kulipa
kodi nzuri kwa Serikali,’’ alisema.
Profesa Mwandosya alisema uchumi ukizorota
Serikali, haiwezi kutekeleza majukumu na kwamba zilizotangulia zilifanya
kazi nzuri kwa kujenga misingi ya uchumi.
Alisema mambo mengine ya kutekeleza ni kuanzisha
na kuendeleza viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na
kuhimiza zaidi kilimo cha umwagiliaji ili nchi ijitosheleze kwa chakula
na kuuza mazao yaliyosindikwa nje ya nchi.
Hatua nyingine ni kuondoa vizuizi vya uwekezaji
kwa Watanzania na hata wa nje, kuimarisha sekta ya utalii wa ndani na
nje kwa vile una fursa nyingi na pia kuhakikisha sekta ya utumishi
inaboreshwa ili wafanyakazi waongeze bidii, uadilifu na kujituma kazini.
Profesa Mwandosya alisifia Serikali ya Rais Jakaya
Kikwete kwamba imefanya mengi mazuri, lakini Watanzania wengi
hawathamini wakati viongozi na watu mbalimbali wa nje ya nchi
wanashangaa kwa ufanisi wa kazi hiyo.
Alisema Tanzania inaendelea vizuri katika kukua
uchumi wake na kwamba yeye atasimamia kwa nguvu zote kuhakikisha uchumi
unazidi kupanda chati hadi kuwafikia Watanzania wote.
“Baada ya uchumi kukua nitahakikisha elimu inaboreshwa kwa
kuangalia sera na mitalaa na ikiwezekana elimu ya msingi itaanza darasa
la kwanza hadi la kumi, lakini baadaye litakuwa hadi la 12,’’ alisema.
Alisema katika hili, pia atasimamia kuboreshwa kwa
masilahi ya walimu na taaluma yao. Pia, baada ya uchumi kukua
atahakikisha sekta ya afya inaboreshwa kwa kusimamia zaidi kitengo cha
kinga akisema ni bora kuliko tiba. “Kwa kweli siku hizi maofisa afya hawaonekani mitaa lakini utafika wakati tutalazimika kuimarisha zaidi kinga.’’
Profesa Mwandosya aligusia pia kwamba Serikali
yake itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi na kuhakikisha
Watanzania wanakuwa wamoja.
Alisema ulinzi wa Taifa na wananchi ni suala la lazima na kwamba akifanikiwa Serikali itaendelea kuliboresha.
Kuhusu ajira kwa vijana, alisema wasomi
wanaotembea na vyeti mikononi kutafuta ajira wanapoteza muda na kuwataka
vijana wa aina hiyo wawe wabunifu na wenye mawazo ya kujiajiri.
Aliwataka vijana wenye mawazo na fikra za kutaka
kufanya kazi ya kujiajiri wafike kwake na watasaidiwa kupata fedha,
lakini siyo kuomba kazi.
“Vijana jitumeni, hata kama mnakosa kazi Tanzania,
wasomi nendeni Uarabuni, Zambia na Malawi kutafuta kazi, jifunzeni
lugha mbalimbali za kimataifa kikiwamo Kichina,’’ alisema na kuongeza
kwamba wasomi wengi wa Kenya, Uganda , Ghana na Nigeria wamejaa nchi za
mbali kufanya kazi.
Profesa Mwandosya alizungumzia pia suala la
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar akieleza kuwa ataudumisha kwa nguvu
zote ili uwe wa kuigwa Afrika.
Alisema kwa kawaida visiwa vingi duniani ni
chimbuko la maendeleo, hivyo anaamini Zanzibar inaweza kuwa kitovu cha
maendeleo ya Tanzania. “Zanzibar ikiwa na rasilimali watu, ikitumiwa vizuri itakuwa kitovu cha maendeleo ya nchi yetu,’’ alisema.
Sababu za kutangaza nia Mbeya
Kuhusu sababu za kutangaza nia ya kuchukua fomu za urais jijini
hapa Profesa Mwandosya alisema alizaliwa Mbeya miaka 68 iliyopita na
kusoma Shule ya Msingi Majengo. Aliishi eneo hilo kwa kipindi kirefu.
Profesa Mwandosya alisema mbali na yeye kuishi
jijini Mbeya pia Baba wa Taifa Marehemu Julius Nyerere alikuwa akifanya
mikutano yake eneo la viwanja hivyo wakati alipokuwa akidai uhuru wa
Tanganyika.
“Eneo hili enzi hizo lilikuwa likiitwa Welfare
Center, hivyo Waafrika walikuwa wakikusanyika hapa kumsikiliza Mwalimu
Nyerere,’’ alisema.
Awali, watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya waliwasili na kuelezea matumaini yao kwa Profesa Mwandosya.
Wazanzibari watinga Mbeya
Katika hali isiyotarajiwa Wazanzibari zaidi ya 10
walitua jijini hapa wakiwa wamevalia fulana zilizoandikwa “Matumaini ya
Zanzibar yapo kwa Profesa Mwandosya.’’
Wazanzibari hao wengi wao wakiwa wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM, walisema walifika Mbeya kwa vile wanamwamini
Profesa Mwandosya kwamba anaweza kuisaidia Tanzania Zanzibar na Tanzania
kwa ujumla.
Pia, alikuwapo Mbunge wa Kibiti, Abdul Marombwa
ambaye alisema kwamba Profesa Mwandosya anafaa kuongoza Tanzania kwa
kuwa ana uelewa na mtazamo wa maendeleo ya kweli.
Ajibu maswali
Alipoulizwa atawafanyia nini Watanzania ili
kuwaongezea imani alisema Profesa Mwandosya alisema: “Nitasimamia
utawala bora na kuishi kwa kufuata haki na amani. Siamini katika utajiri
wa kuwagawia wananchi.”
Kuhusu amelifanyia nini Taifa kwa kipindi chote
alichokuwa mtumishi wa Serikali alisema: “Nimeyafanya mengi na wenzangu,
sina nilichofanya peke yangu. Niliwahi kwenda kwenye shule moja ambayo
niliichangia fedha nyingi na wakataka shule ile iitwe jina langu lakini
nilikataa,” alisema na kuongeza: “Nilikataa kwa sababu hata kama
kiongozi anabuni miradi mbalimbali, utekelezaji ni wa watu tofauti.”
Hata hivyo, aliwataka watu wanaotaka kujua zaidi
mchango wake kwa jamii kwenda wizarani au kwenye taasisi mbalimbali
alizowahi kufanyia kazi kuzitafuta na akawataka Watanzania wajenge
desturi ya kujisomea vitabu ili kujua waliyofanya na watu tofauti.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment