Fahmi Dovutwa akichangia mada wakati wa semina ya wajumbe wa bunge maalum la katiba kupitia vifungu vya rasimu ya kanuni.
Historia yake
Fahmi Nasoro Dovutwa ni Mwenyekiti wa kitaifa wa
Chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP). Alizaliwa Februari 27,
1957 mjini Kisarawe mkoani Pwani (Amefikisha miaka 58 Februari mwaka
huu).
Dovutwa alianza elimu yake ya msingi mwaka 1967
katika shule ya msingi Zanaki hadi alipohitimu mwaka 1974 alipoendelea
na masomo ya sekondari katika shule ya sekondari Azania ambako alihitimu
mwaka 1977.
Rekodi za elimu za Dovutwa zimekuwa “kizungumkuti”
kupatikana. Hata taarifa zake binafsi alizotoa kwa ajili ya rekodi za
Bunge Maalum la Katiba zinasisitiza kuwa ameishia kidato cha nne.
Juhudi za kumpata yeye mwenyewe ili akamilishe
rekodi zake hazikufua dafu na ni yeye peke yake tangu nianze kufanya
uchambuzi wa watu wanaotajwa kuwania urais, ambaye hakutoa ushirikiano
kabisa ili kunifanya nipate rekodi zake sahihi. Hata hivyo hilo haliwezi
kunizuia kumchambua.
Watu wa karibu yake wamenijulisha kuwa kwa muda
mrefu amekuwa akijishughulisha na kazi za ujasiriamali katika soko la
Magereza jijini Dar es Salaam hadi baadaye alipochaguliwa kuongoza chama
cha UPDP ambacho yeye ni mwenyekiti hadi sasa.
Mwaka 2014, alikuwa ni miongoni mwa Watanzania
waliopata fursa ya kuteuliwa na Rais wa Tanzania kupitia kundi la vyama
vya siasa, na kuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba lililofanya kazi
yake mjini Dodoma na kukamilisha Katiba Inayopendekezwa ambayo hata
hivyo imeligawa taifa katika vipande viwili. Dovutwa ameoa na ana
watoto.
Mbio za ubunge
Katika historia ya kisiasa ya Dovutwa, hakutoa pia
rekodi zinazoonyesha kama aliwahi kugombea ubunge katika jimbo lolote
na hata nilipozitafuta sikufanikiwa kuzipata.
Mbio za urais
Kiongozi huyu alijitosa katika mbio za urais mwaka
2010 akitumia tiketi ya chama chake cha UPDP. Katika uchaguzi ule ambao
Jakaya Mrisho Kikwete aliongoza kwa ushindi wa asilimia 62.83,
akifuatiwa na Willibroad Slaa aliyekuwa na ushindi wa asilimia 27.5, na
Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF akiwa na asilimia 8.28, Dovutwa aliibuka
katika nafasi ya mwisho akiwa na asilimia 0.16 ya kura zote kwa kupitwa
na Peter Mziray wa APPT (asilimia 1.15), Hashim Rungwe wa NCCR (asilimia
0.31), na Mutamwega Bhatt wa TLP aliyekuwa na asilimia 0.21 ya kura
zote.
Katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, Dovutwa
hajatangaza popote kuwa atagombea tena nafasi ya urais lakini duru za
kisiasa ndani ya chama hicho ikiwamo kutoka kwa baadhi ya viongozi
waandamizi, zimenieleza kuwa anapewa nafasi kubwa ya kugombea tena.
Nguvu yake
Udhaifu wake
Nguvu yake
Jambo la kwanza ninalolitazama kama nguvu ya
Dovutwa ni “umaarufu”. Nathubutu kusema kuwa huyu ni mmoja wa viongozi
maarufu wa wa vyama visivyo na wabunge. Mikogo yake ya kuvutia katika
kampeni za mwaka 2010. Uvaaji wake kuanzia chini hadi “kofia nyekundu”,
vilimtofautisha na mgombea yeyote yule kwenye uchaguzi ule. Mimi binafsi
nilijikuta navutiwa sana na staili za kiongozi huyu hata kama sikuwa
najua sera za chama chake kwa mwaka 2010. Nguvu hii ya kuvutia macho
nayo ni muhimu sana kwa mwanasiasa yeyote, hata kama ukiwa na elimu
kubwa, mipango mingi bado suala la unavaaje, unavutiaje na ukoje
(mtazamo wa nje), halikwepeki katika siasa.
Lakini pia, Dovutwa ni mjasiriamali mzoefu na sifa
hii pia inamuongezea nguvu mtu yeyote yule ambaye anataka uongozi wa
juu wa nchi. Tena nimeambiwa kuwa amekuwa mjasiriamali mdogo kwa kipindi
kirefu na hasa akifanya kazi na vijana wa chini. Natambua kuwa fursa
hiyo ilimpa nafasi kubwa ya kuendelea kuyaishi maisha ya vijana wa chini
na hata kujua masuluhisho ya haraka, ya muda mfupi na muda mrefu, kwa
sababu pia ukishaingia ikulu kazi yako kubwa ni kutafuta majawabu ya
masuala ya watu. Majawabu ya muda mrefu na muda mfupi.
Udhaifu wake
Udhaifu wa kwanza wa Dovutwa uko katika elimu
(hadi hapo atakapowajulisha Watanzania elimu yake rasmi tofauti na
iliyoko kwenye vyanzo sahihi vya taarifa kama tovuti ya Bunge Maalum la
Katiba), udhaifu huu unasimama kama ulivyo kwa sababu taifa letu
linakwenda mbele sasa na elimu ni jambo la msingi katika uongozi, hata
kama siyo kila kitu. Kukosekana kwa taarifa za elimu yake tofauti na
ilivyo kwa viongozi wengi wa vyama vya siasa ni jambo linaloleta shaka
juu ya weledi wa kiongozi huyu. Kwa karne ya sasa na hapa Tanzania
kulikojaa wasomi, ni nadra sana ikatokea kwamba Mtanzania mwenye elimu
ya kidato cha nne tu “akawa na ndoto za kuingia Ikulu na jambo hilo
likatekelezeka”.
Lakini jambo la pili, Dovutwa mara nyingi amekuwa
ni mtu wa kukosa ajenda na matokeo yake hupenda kurukia ajenda za
masuala ambayo hayana tija. Mara kadhaa ameonekana katika vyombo kadhaa
vya habari akivishambulia sana vyama vya upinzani lakini akiwa hafanyi
hivyo kwa CCM. Hali hii inamuweka katika sahani ya wanasiasa ambao
wanashangaza kidogo na nadhani huu ni udhaifu mkubwa sana kama kweli
bado ana ndoto za kugombea urais, achilia mbali kuingia Ikulu.
Uhusiano wenye mashaka baina yake na CCM ni suala
jingine linalosisitiza juu ya udhaifu wake. Dovutwa, akiwa mgombea urais
kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka 2010, aliwashangaza Watanzania katikati
ya kampeni huku Chama Cha Mapinduzi kikionekana kuzidiwa sana na
upinzani, hususani Chadema na CUF, Dovutwa alijitokeza hadharani (akiwa
mgombea) na kutangaza kuwa chama chake na vyama vingine kadhaa visivyo
na wabunge na mitandao mikubwa “ati” vinamuunga mkono mgombea wa CCM,
Jakaya Mrisho Kikwete.
Hata hivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi
haikukubaliana na kujitoa huko kwa baadhi ya vyama na kusisitiza kuwa
kisheria muda wa kujitoa umekwisha. Tamko na msimamo ule ambao sina
uhakika kama kweli ulitokana na vikao vya chama chake, vina maana kuwa
huenda anafanya “kazi maalumu” katika siasa za ndani ya nchi. Kwa
sababu, katika mantiki ya kawaida, si jambo rahisi chama cha upinzani
kufanya maamuzi ya kuunga mkono chama kinachoongoza, katika nchi
inayosaka demokrasia kama yetu.
Katika Bunge Maalum la Katiba, Dovutwa ni mmoja wa
viongozi ambao pia walishangaza sana Watanzania. Yeye ni mmoja wa
wabunge wa bunge lile ambao walisimama hadharani mara kadhaa na
“kuponda” msimamo wa vyama vya Ukawa lakini bila kueleza kuwa anaunga
mkono upande upi.
Ni jambo la hatari sana chama cha siasa au
viongozi wa vyama vya siasa wanapokwenda katika kazi kubwa ya kitaifa
bila kuwa na ajenda ya msingi ya kuisimamia. Ndiyo maana kulikuwa na
sintofahamu hiyo ambayo iliegemea upande mmoja bila kutafakari kuwa
vyama vilivyoondoka katika mchakato ule navyo vilikuwa na hoja zao.
Viongozi kama Dovutwa walipaswa kufanya kazi ya
kujenga hoja kuliko kuendelea “kuponda” Ukawa, jambo lililowapotezea
muda na kushindwa hata kujenga taswira za vyama vyao.
Lakini udhaifu mwingine wa Dovutwa ni kushindwa
kukihuisha chama chake. Chama cha UPDP hakijapata ushindi wa kujivunia
katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba 2014. Chama
hiki kilizidiwa na vyama vipya kama ACT na ADC ambavyo viliambulia viti
kadhaa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Nini kinaweza kumwangusha?
Asipochaguliwa (Mpango B)
Kama Dovutwa ameshindwa kukihuisha chama chake kisimamie ajenda
muhimu za kitaifa hapa nchini lakini pia kufanya vibaya sana hata katika
uwakilishi chini wa wananchi, hizo siyo dalili nzuri kwa kiongozi
ambaye anatarajia kuwa kiongozi wa nchi.
Baadhi ya viongozi waandamizi wa UPDP walioongea
nami, wameniambia kuwa chama chao kimekuwa na matatizo makubwa sana
katika kufanya uchaguzi wa kikatiba wa kila baada ya awamu. Baadhi yao
wameeleza kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho mara kadhaa
wamekuwa na uoga kuwa chaguzi zikifanyika kwa uwazi na haki, huenda
wakaangushwa. Tuhuma hizi pia zinamgusa Dovutwa mwenyewe ambaye amewahi
pia kuonekana kwenye kipindi kimoja che televisheni akijitetea kuwa
chama chake kitajitahidi kukamilisha chaguzi zake za ndani. Kama Dovutwa
anashindwa kusimamia chaguzi za chama chake kwa uhakika na kwa wakati
hadi anasuasua sana, ni dalili tosha kuwa kazi ya urais wa nchi inaweza
kumuwia ngumu kupita kiasi.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Jambo moja ambalo naona linaweza kumvusha Dovutwa
katika harakati za ndani ya chama chake za kupewa ridhaa ya kugombea
urais ni uongozi wake ndani Chama. Dovutwa ndiye kiongozi mkuu wa UPDP
na jambo hilo kwa siasa za Afrika lina maana kuwa mara nyingi yeye ndiye
mwenye nafasi kubwa ya kupewa ridhaa muhimu kama hizi, mara
zinapotokea. Sitashangaa kuona chama chake kikimpitisha kwa sababu yeye
ni mwenyekiti wa chama.
Lakini jambo la pili linaloweza kumfanya apitishwe
ni kwa sababu aligombea urais mwaka 2010. Mipango na mbinu alizotumia
mwaka 2010 pamoja na kwamba zilimpa nafasi ya mwisho lakini tunakubali
kuwa kuna baadhi ya Watanzania walimpigia kura. Ndiyo kusema kuwa UPDP
kama inahitaji kura zaidi katika uchaguzi wa mwaka huu huenda yeye
Dovutwa akapaswa kutumia uzoefu wake wa mwaka 2010 ili kufanikisha jambo
hilo.
Nini kinaweza kumwangusha?
Jambo la kwanza linaloweza kukifanya chama chake
(UPDP) kisimpitishe kugombea urais, nadhani ni itakapotokea kuwa chama
hicho kina mgombea urais mwingine mwenye sifa na uwezo mkubwa kumshinda.
Kama nilivyoeleza awali, elimu tu ya Dovutwa haieleweki na inawezekana
kabisa kuwa hata yeye mwenyewe hapendi kuiweka wazi. Ikiwa chama chake
mathalani kikapata mtu mwingine mwenye elimu kubwa sana na uwezo
kumshinda, nadhani Dovutwa anaweza kupumzishwa katika nafasi hiyo.
Lakini jambo la pili linaloweza kumfanya
asipitishwe ni ikiwa hoja ya mwaka 2010 ya kumuunga mkono Kikwete
itatiliwa mashaka katika vikao vya maamuzi vya chama chake.
Baadhi ya viongozi waandamizi wa UPDP waliokubali
kuongea nami wamesisitiza kuwa hatua ile ya Dovutwa ya mwaka 2010
haikupita katika vikao vya maamuzi. Ikiwa atatiliwa mashaka kuwa anaweza
tena kufanya yale ya mwaka 2010, huenda sababu hii pia ikamuweka nje ya
mbio hizi.
Asipochaguliwa (Mpango B)
Ikiwa Dovutwa hatapitishwa kugombea urais wa Tanzania, huenda akawa na mipango kama mitatu mezani:
Mpango wa kwanza unaweza kuwa kutafuta jimbo na
kugombea nafasi hiyo. Lakini nadhani kwa nguvu dhaifu ya chama chake ni
vigumu pia kushinda jimbo lolote, maana kama chama hakina wenyeviti wa
serikali za mitaa wa kutosha, madiwani ni vigumu kudhani kuwa kitapata
“mbunge” kutoka mbinguni.
Hitimisho
Mpango wa pili unaweza kuwa ni kuendelea na uongozi wa ndani ya
chama chake. Mpango huu ndio anaendelea nao hadi sasa na nimeambiwa kuwa
kunaweza kufanyika uchaguzi mwingine katika chama hicho na kwamba bado
atatetea nafasi yake ya uenyekiti, jambo ambalo halina shida
kidemokrasia.
Na mpango wa tatu unaweza kuwa kuunganisha nguvu
za vyama vya upinzani visivyo na wabunge ili kuunda umoja wao. Tayari
nina taarifa za kina kuwa baadhi ya vyama visivyo na wabunge vinaendelea
na vikao vya chini kwa chini ili vione kama na vyenyewe vinaweza kuunda
“Ukawa” yao. Mpango huu utakuwa unamhusu sana Dovutwa kwa sababu
natambua ushawishi alionao juu ya vyama visivyo na wabunge.
Hitimisho
Dovutwa ana changamoto kubwa sana katika siasa za
Tanzania. Ukiachilia mbali kwamba yupo katika chama kisicho hata na
diwani lakini nisisitize kuwa taswira kadhaa za chama hicho
zinamsababishia yeye na wenzake hukumu ambazo wakati mwingine
zingeepukika kama zingefanyiwa kazi.
Kama nilivyoeleza pale juu, huyu ni mmoja wa
viongozi wa vyama visivyo na wabunge ambaye ana mvuto wa pekee
unaotokana na staili zake za kufanya mambo na ubunifu wa mavazi n.k.
Hayo peke yake hayatoshi. Ana jukumu kubwa sana la kusimamia uhuishaji
wa chama chake na kufuta makosa ya nyuma kuliko kusonga mbele.
Nafasi ya Dovutwa kisiasa ndani ya nchi natumaini
kuwa itaendelea kuwa palepale (bila kukua) kwa sababu Watanzania wa sasa
wanazidi kupata weledi mkubwa unaowasaidia katika ufanyaji wa maamuzi
mbalimbali.
Siasa za sasa zinataka viongozi wepesi sana ambao
sioni kama Dovutwa ni mmoja wao. Ikiwa mwenyekiti wa chama cha siasa
kilichosajiliwa unaombwa wasifu wako na hauutoi kwa wiki kadhaa ina
maana kuwa hata wanaokupigia chapuo kuwa una uwezo wa kugombea nafasi
fulani ya juu wanakuwa wanakosea sana.
Pamoja na mapungufu lukuki ambayo nimeyabainisha
kutokana na hali halisi inayomkabili kiongozi huyu, namtakia kila lililo
jema katika mipango yake ya mbele kisiasa huku nikimpa nafasi finyu ya
kuwa mgombea mwenye mafanikio ikiwa atafanya hivyo Oktoba mwaka huu.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment