Dk Shukuru Kawambwa
Kambi ya Upinzani
Bungeni imeilipua Serikali ikihoji vigezo ilivyotumia kutoa taarifa ya
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), inayoonyesha kuwa sekta ya elimu
imefanikiwa kwa asilimia 81 na kushika nafasi ya kwanza ya utekelezaji
wa awamu ya kwanza ya mkakati huo.
Imesema wakati takwimu hizo zinatolewa, wanafunzi
bado wanakaa chini kwa kukosa madawati, uhaba wa walimu, madarasa na
vifaa vya kufundishia, ada juu kwa shule za binafsi, michango lukuki,
elimu ya walimu isiyoeleweka, wanafunzi kukosa mikopo, maslahi ya walimu
pamoja na kutotekelezeka kwa Sera ya Walimu.
Wakati kambi hiyo ikieleza hayo, Kamati ya Bunge
ya Huduma za Jamii, imesema hadi kufikia Machi mwaka huu, baadhi ya
taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo zilikuwa hazijapata hata senti
moja ya fedha ya maendeleo, kikiwemo Chuo Kikuu cha Mzumbe ambacho
kilitakiwa kupatiwa Sh850milioni.
Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo alihoji; “Ni uwekezaji gani umefanyika
hadi tukapata matokeo haya ya BRN? Matatizo yote yanayoikabili sekta ya
elimu yameboreshwa vipi? Kuna miujiza gani kama siyo mbinu chafu na
ujanja ujanja tu?”
Akifafanua matatizo yanayoikabili sekta ya elimu,
Lyimo alisema, “Mwaka 2010 katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, mliwaahidi
Watanzania kuwa kila shule ya msingi itakuwa na darasa la elimu ya awali
lenye madawati. Mpaka sasa ahadi hiyo haijatekelezwa hata kwa asilimia
50 tu, watoto bado wanakaa chini na kumeongezeka tatizo la kukosa
matundu ya vyoo.”
Alisema mpaka sasa walimu wanaendelea na kilio
chao cha malimbikizo ya mishahara na stahili zao nyingine, huku
akisisitiza kuwa walimu walioajiriwa Mei Mosi, mwaka huu, mpaka sasa
hawajalipwa fedha za kujikimu.
“Tunaitaka Serikali kuonyesha fedha zilizotengwa
kwa ajili ya nyongeza ya mishahara ya walimu katika bajeti ya 2015/16.
Tunataka kujua walimu zaidi ya 37,000 waliopandishwa madaraja lakini
hawajarekebishiwa mishahara yao watalipwa lini?” alisema Lyimo.
Aliiponda sera mpya ya elimu iliyozinduliwa na Serikali hivi karibuni kuwa haiwezi kufanikiwa.
Alisema kuna mambo matatu yanayoweza kuifanya
ifanikiwe ambayo ni kuwa na walimu bora, zana bora za kufundishia na
walimu wenye motisha, huku akiitaka Serikali kueleza imetenga fedha
kiasi gani ili kufanikisha mambo hayo matatu.
“Tunataka kujua ni lini elimu ya msingi katika mfumo wa umma itatolewa bure kama inavyoeleza sera ya elimu,” alisema.
Katika hotuba hiyo, kambi ya upinzani ilihoji
baadhi ya vyuo kuanza kujitengenezea mitalaa yake kwa lengo la kuwavutia
wanafunzi, jambo linalosababisha kukosekana kwa ubora linganifu wa
elimu ya juu katika ngazi mbalimbali.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii,
Mwenyekiti wake Margaret Sitta alieleza changamoto lukuki zinazoikabili
Wizara ya Elimu.
Wabunge
Kuhusu upanuzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, alisema
makandarasi wametishia kukipeleka mahakamani kutokana na kushindwa
kuwalipa Sh1.2 bilioni za ujenzi wa mabweni ya wanafunzi ambao
ulikamilika toka 2009.
Kamati hiyo pia iliishauri Serikali kuhakikisha
inawaandaa wataalamu kwa ajili ya kutoa elimu bora kwa wanafunzi,
kuboresha mazingira ya walimu na kuondoa kero za utolewaji wa mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, waziri wake Dk Shukuru Kawambwa aliomba kuidhinishiwa Sh989.5
bilioni kwa mwaka 2015/16.
Wabunge
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Diana Chilolo
alichafua hali ya hewa baada ya kuwapiga vijembe Chadema kuwa ni
afadhali nyumba yake kuliko jengo la makao makuu ya chama chao.
Chilolo aliwapiga vijembe hivyo wakati akichangia hotuba ya bajeti ya wizara hiyo ya elimu.
“Mmeshindwa hata kujenga barabara ya kwenda
ofisini kwenu kwa kiwango cha lami yaani mita 100 tu zinawashinda,”
alisema na kuamsha hasira za wabunge wa Chadema waliosimama wakitaka
Mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mngo’ngo awape nafasi wampe taarifa.
Hali hiyo iliwafanya Halima Mdee (Kawe-Chadema) na
Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini-Chadema) kusimama lakini
hawakupewa nafasi.
Hata hivyo, alipopewa nafasi Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo alimtaka mbunge huyo kutosema jambo bila ya kuwa na uhakika.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu (CCM),
Felister Bura alisema ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha kuwa walimu
wanalipwa madai mbalimbali wanayoyadai.
Felister alisema walimu wanafanya kazi katika
mazingira magumu, wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la kipekee. Mbunge wa
Viti Maalumu (Chadema), Rachel Mashishanga alisema kuna tatizo katika
utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Alisema baadhi ya wanafunzi hususan wasio na uwezo, hukosa mikopo huku wale wenye uwezo wakipata.
Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alisema zinahitajika juhudi za makusudi katika kuhakikisha kuwa elimu inapewa kipaumbele. Alisema elimu nchini bado iko chini kunahitajika juhudi za kutosha kuiokoa.
CHANZO: MWANANCHI
Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alisema zinahitajika juhudi za makusudi katika kuhakikisha kuwa elimu inapewa kipaumbele. Alisema elimu nchini bado iko chini kunahitajika juhudi za kutosha kuiokoa.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment