Waziri wa Elimu ya Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shakuru Kawambwa.
Serikali katika mwaka wa fedha 2015/16 imeweka
vipaumbele katika sekta ya elimu kwa kuongeza upatikanaji wa fursa ya
elimu kwa usawa katika ngazi zote za elimu na mafunzo.
Vile vile kuinua ubora wa elimu na kujenga stadi stahiki katika
ngazi zote na mafunzo na kuimarisha taasisi za usimamizi wa ubora wa
elimu pamoja na ufuatiliaji na tathmini ili zitekeleze majukumu ya
kuhakikisha elimu bora inatolewa katika ngazi zote za elimu na mafunzo.
Waziri wa Elimu ya Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shakuru Kawambwa, alisema hayo jana wakati akiwasilisha hotuba ya wizara yake
ya Makadirio ya Matumizi ya fedha kwa mwaka 2015/16. Alisema katika eneo la utungaji na utekelezaji wa Sera za Elimu,
wizara hiyo inaanza kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014,
kupitia na kurekebisha sheria na miongozo mbalimbali ya elimu ili
kuendana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014.
Aidha, pamoja na mambo mengine, wizara hiyo itahuisha mitaala na
kuimarisha mfumo wa utoaji wa elimu ya juu, ufundi na mafunzo ya ufundi
stadi ili kutoa elimu kulingana na mahitaji halisi ya soko la ajira na
maendeleo ya Taifa.
Alisema katika ithibati ya shule, wizara hiyo itasajili shule za
msingi na sekondari kwa kutilia mkazo zaidi shule za ufundi na sayansi
pamoja na vituo vya elimu ya watu wazima na vituo vinavyotoa elimu ya
sekondari nje ya mfumo rasmi.
Kuhusu ukaguzi wa shule na vyuo vya ualimu, wizara hiyo itafuatilia
ubora wa elimu katika asasi 17,242, zikiwemo asasi 8,225 za elimu ya
Msingi na 313 za sekondari zilizokuwa katika utepe mwekundu, asasi 6,672
za elimu ya msingi na 1,722 za sekondari zilizokuwa katika utepe wa
njano, na nyingine 181 za sekondari kwenye mpango wa asasi kwa madaraja
wa mwaka 2014/15.
Dk. Kawambwa, alisema pia wizara yake katika kusimamia Taasisi na
Wakala, itajenga uwezo wa taasisi za usimamizi wa ubora wa elimu katika
ngazi ya elimu ya juu na ufundi na Mafunzo ya Ufundi ili kuhakikisha
kuwa elimu bora inatolewa katika ngazi zote za elimu na mafunzo.
Wizara hiyo inatarajia kutumia jumla ya Sh. 989,552,542,000.00 kati
ya hizo Sh. 510,877,383,000.00 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh.
478,675,159,000.00 kwa miradi ya maendeleo. Awali Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kuhusu
utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo, ilisema bado upatikanaji wa
fedha za maendeleo kwa taasisi zilizo chini ya wizara ni tatizo kwani
hadi mwezi Machi kuna taasisi zilikuwa hazijapokea hata senti moja kwa
ajili ya maendeleo.
Akisoma taarifa ya kamati hiyo, Mwenyekiti wake, Margerth Sitta,
alisema katika kutekeleza majukumu yake wizara iyo inakabiliwa na
changamoto ya utendaji kazi usioridhishwa wa idara ya ukaguzi wa elimu
nchini kutokana na ufinyu wa bajeti.
Changamoto nyingine alisema ni upungufu katika Sheria ya Baraza la
Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) inayolenga kudhibiti utoaji holela wa
mafunzo ya elimu ya ufundi stadi nchini. Kamati hiyo ilishauri iruhusu Idara ya Ukaguzi wa Elimu nchini kuwa
wakala unaojitegemea ili uweze kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na
ufanisi zaidi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment