Mchungaji Christopher Mtikila akichangia hoja wakati wa Bunge Maalumu la Katiba
Historia yake
Mchungaji Christopher Mtikila ni Mwenyekiti wa
Chama cha Democratic (DP) ambacho kina usajili wa kudumu hapa Tanzania.
Alizaliwa mwaka 1950 (ana umri wa miaka 65) mkoani Njombe, Kusini mwa
nchi yetu.
Kwa bahati mbaya, hadi nachapisha uchambuzi huu
sikupata taarifa za elimu ya Mtikila kwani hakuwa mwepesi kutoa
ushirikiano mwezi mmoja uliopita na baadaye alisafiri kwenda nje ya
nchi na kurejea wakati nikiwa katika hatua za mwisho za uhariri.
Pamoja na shughuli za siasa, Mchungaji Mtikila ni
mwanzilishi na mkuu wa Kanisa la Kipentekoste la Full Salvation. Lakini
pia kwa muda mkubwa wa maisha yake amekuwa anajihusisha na harakati za
haki za binadamu kwa kupitia kitengo cha haki za binadamu cha kanisa
hilo kiitwacho “Liberty Desk”. Kanisa lake ni moja ya makanisa machache
hapa Tanzania yenye vitengo vya namna hiyo.
Umaarufu wa Mtikila ulikua sana mwanzoni mwa miaka
ya 1990 kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuongea, upinzani wake dhidi
ya muundo wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, madai yake kuhusu
kile anachokiita “uhujumu wa uchumi unaofanywa na watu ambao anawaita
magabacholi” na kesi mbalimbali za kikatiba alizokuwa akifungua katika
Mahakama za Tanzania, ni kati ya mambo machache yaliyomfanya asikike
kila kona ya nchi.
Kwa muda mrefu, chama chake cha DP hakikuweza
kupata usajili wa kudumu kutokana na kukataa kwake kuitambua Zanzibar.
Alikuwa akisisitiza kuwa chama chake ni cha Tanganyika na siyo Tanzania.
Hata hivyo, ilimpasa abadili msimamo wake katika miaka ya hivi karibuni
kwa kukubali kutafuta wanachama kutoka Zanzibar (kama sheria ya
uchaguzi inavyotaka) ndipo kikapata usajili wa kudumu.
Mtikila alifungwa kwa mwaka mmoja mwaka 1999 baada
ya kupatikana na hatia ya kutoa maneno ya kashfa dhidi ya aliyekuwa
Katibu Mkuu wa CCM, marehemu Horace Kolimba. Mwaka 2004 pia alihukumiwa
kifungo kilichosimamishwa cha miezi sita kwa kutoa maneno ya kashfa
dhidi ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Ilala. Kwa ujumla maisha yake
yamekuwa ni ya harakati muda wote, akipambana awezavyo, akisimama kidete
inavyowekana na akijikuta matatani kila uchwao.
Mchungaji Mtikila amemuoa Georgia na wana watoto.
Mbio za ubunge
Mwaka 1997, Mbunge wa Ludewa kwa tiketi ya CCM
wakati huo, Horace Kolimba aliitwa na Kamati Kuu ya chama chake mjini
Dodoma kwenda kujibu mashtaka ya ndani ya chama juu ya kauli ambazo
alikuwa akizitoa kwamba “CCM imepoteza mwelekeo”, baadhi ya viongozi wa
chama chake walimchukulia kama msaliti na wengine wakimuona kama mtu
aliyethubutu kusema ukweli bila kumhofia Nyerere. Hata hivyo, Kolimba
alifariki hukohuko Dodoma katika siku ambazo alikuwa akihojiwa.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipotangaza
uchaguzi mdogo, ndipo Mtikila alikihama chama chake cha DP akajiunga na
Chadema na kuomba ridhaa ya kugombea. Mtikila ni mzaliwa wa Ludewa na
alifanya hivyo kwa sababu chama chake cha DP kilikuwa kimenyimwa
usajili.
Uchaguzi ulifanyika Mei 25, 1997 na kumpa ushindi
mgombea wa CCM Profesa Chrispin Haule Che Mponda ambaye alipata kura
20,111 dhidi ya 8,386 za Mtikila. Mgombea wa NCCR ambayo haikuwa
imejijenga vilivyo Ludewa, Barnabas Kidulile, alipata kura 1,271.
Mbio za urais
Nguvu yake
Baada ya kushindwa uchaguzi huo, Mtikila alisikika
akihitilafiana na Chadema hadharani huku akitoa shutuma nzitonzito,
akafukuzwa kwenye chama hicho na ndipo akaendelea kuwekeza nguvu kwenye
mipango ya kukamilisha usajili wa chama chake.
Mbio za urais
Mtikila alianza harakati za kugombea urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 kwa tiketi ya DP. Alikuwa
kati ya wagombea 10 katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo. Katika uchaguzi
huo, alipata asilimia 0.27 ya kura zote, akiwa nyuma ya Jakaya Kikwete
wa CCM (asilimia 80.28), Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF (asilimia
11.68), Freeman Mbowe wa Chadema (asilimia 5.88), Augustine Mrema wa TLP
(asilimia 0.75) na Dk Sengondo Mvungi wa NCCR (asilimia 0.49).
Hakugombea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2010 na chama
chake hakikuweka mgombea. Hata mwaka huu, hajaweka msimamo wake wazi
japokuwa taarifa za ndani ya chama hicho zinaonyesha kuwa kinaweza
kusimamisha mgombea na huenda mtu huyo akawa Mtikila.
Nimemuweka katika orodha hii kwa sababu tayari
anatajwa kuwa na sifa, vigezo na hata historia ya mapambano inayompa
nafasi ya kuweza kusimama mbele ya Watanzania kuomba uongozi wa juu.
Nguvu yake
Jambo la kwanza ambalo bila shaka linampa nguvu
ikiwa ataingia kwenye kinyang’anyiro cha urais ni umaarufu wake. Mtikila
ni maarufu, si kwa watu wenye umri wa zamani tu, lakini pia hata kwa
vijana wadogo wa sasa. Ni vigumu ikiwa Mtanzania yeyote anayefuatilia
masuala ya siasa katika nchi au habari mara kwa mara na asimjue. Ni
kiongozi anayejishughulisha na mambo mengi mno na harakati
zilizopitiliza na kwa mwanasiasa anayetaka nafasi ya juu, umaarufu
unaweza kuwa karata muhimu, la msingi tu umaarufu huo vichwani mwa watu
uwe na maana ya kumuona kama “mtu muhimu” katika hatua zake.
Lakini jambo la pili linalompa nguvu na sifa
zaidi, ni kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya mara kwa mara, ya kufungua
kesi za masuala ambayo Serikali inakuwa imewanyima raia kwa muda mrefu.
Mara nyingi katika siasa za Afrika, kesi za kuishtaki Serikali kwa
masuala ambayo yanaonekana kuwa makubwa huwa linaonekana kama jambo
hatari hata kwa usalama wa mhusika.
Kesi za kikatiba ambazo amewahi kufungua ni pamoja
ya kutaka wagombea binafsi kuruhusiwa katika uchaguzi Tanzania,
wananchi wa Tanzania Bara kuruhusiwa kwenda Zanzibar bila pasipoti na
vyama vya siasa kuruhusiwa kufanya mikutano bila kuomba kibali kutoka
kwa mkuu wa wilaya na polisi na nyinginezo. Hebu tujiulize, ni vyama
vingapi vya siasa vimewahi kuwa na “uthubutu” huo?
Mtikila alishinda kesi ya mgombea binafsi na
aliiweka Serikali kwenye njia panda kwa asilimia 100. Katika suala hili
yeye ni mtu wa kujivunia na kama upiganaji wa kiwango hiki peke yake
ndiyo ungekuwa tiketi ya urais, basi tayari angestahili tuzo hiyo bila
mjadala.
Hakuna mwanasiasa mwingine yeyote hapa Tanzania aliyewahi kupambana na Serikali mahakamani kila kukicha kama Mtikila, hayupo!
Lakini jambo la tatu linalompa nguvu na sifa ni
misimamo ya kipekee. Mtikila hajali anapokuwa ana ajenda zake na
misimamo yake na mara nyingi misimamo hiyo huwa ni ya kipekee hata kama
ni mibaya kiasi gani, yeye huisimamia na kubakia nayo hata kama wenzake
wote watamkimbia. Nakumbuka tulipokuwa Bunge Maalumu la Katiba, alikuwa
na ajenda ya kusimamisha Bunge lile lisifanye kazi kwa sababu limeanza
kinyume cha sheria na halina hadhi ya kutunga katiba ya nchi. Pamoja na
wanasheria wakongwe kuwa na mawazo tofauti naye, bado alishikilia
msimamo wake na aliondoka kwenda Dar es Salaam kwa minajili ya kufungua
kesi husika (sina taarifa jambo hili lilipoishia).
Udhaifu wake
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Nini kinaweza kumwangusha?
Asipochaguliwa (Mpango B)
Hitimisho
Hata baadaye, vyama vinavyounda Ukawa vilipoamua kutoka bungeni,
Mtikila aliunga mkono uamuzi huo na alisisitiza kuwa yeye anafanya kazi
na umoja huo kwa suala la katiba, sijapata taarifa za hatima yake
katika kuendelea kuwa ndani ya Ukawa, lakini ninachojua ni kwamba
misimamo hii ya Mtikila kuna wakati imekuwa na tija kubwa, si kwake tu,
bali kwa Taifa zima.
Udhaifu wake
Udhaifu wa kwanza wa Mtikila ni utoaji wa “kauli
tata” ambazo kuna nyakati zinaudhi na kuamsha hasira ya upande
uliotuhumiwa. Mtikila ana tabia ya kuzungumza mambo magumu na
mkishindana anaweza akakudharau na hata kukupa jina baya ambalo hukuwahi
kufikiri kuwa unaweza kuitwa au kupewa. Mara kadhaa amewahi kusikika
akitoa shutuma kali kwa viongozi wa nchi na hata vyama vya upinzani.
Sifa hii si nzuri kwa mtu ambaye ana ndoto au anaotewa kushika uongozi
wa juu wa nchi siku moja.
Lakini jambo la pili ambalo naliona ni udhaifu
pia, hupenda kushughulikia mambo ya hatari peke yake na wakati mwingine
bila kufanya kazi ya kutosha kuwaelimisha wananchi na vyombo vya habari
na kutafuta hali ya kupewa uzito na mioyo ya wananchi na wadau. Tabia
hii ya kuamka na ajenda nzito mkononi na kulazimisha ajenda anayotoa
iungwe mkono ghafla bila kuwaandaa wananchi, siyo jambo zuri kisiasa.
Kuna masuala ya msingi anayapigania na
yanapotoshwa na vyombo vya habari na wanasiasa wa vyama vingine kwa
sababu tu hakufanya kazi ya siasa ya kuyatangaza, kuomba ushirikiano wa
wenzake. Ili uwe kiongozi mzuri una wajibu wa kuwashirikisha watu
waliokuzunguka ili uamuzi mkubwa unaotaka kufanya uungwe mkono.
Kujifanyia peke yako kunakuwa hakuna tija kubwa kwa masilahi mapana ya
wote.
Mwisho, Mtikila amekuwa akitoa kauli zinazodhaniwa
kuwa ni za kibaguzi na hili haliko “uvunguni”, amefanya hivyo mara
nyingi mno katika mikutano yake na hata mbele ya vyombo vya habari. Kuna
wakati amekuwa akisikika hadharani akiwatuhumu Wahindi kwa lugha za
kibaguzi, anawaita “magabacholi”, lakini pia kuna wakati amewahi
kulalamikiwa hata na nchi jirani ya Rwanda kwa namna alivyowahi
kuyashutumu makabila makubwa ya nchi hiyo kwa kauli za kibaguzi.
Kiongozi mmoja wa juu wa Serikali nimewahi
kumsikia akisema kuwa alipokutana na kiongozi mmoja wa juu wa Rwanda,
baada ya salamu akamuuliza kiongozi huyo “who is Reverend Mtikila”?
(Mchungaji Mtikila ni nani?). Mtikila siyo tu kuwa anaipa chemsha bongo
Serikali nchini, hata huko nje wanaumiza vichwa juu yake na hili siyo
suala la kujivunia kama kweli nchi inatafuta viongozi watakaoimarisha
uhusiano na nchi za jirani.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Mambo mawili yanaweza kukifanya chama cha DP kimpitishe:
Jambo la kwanza ni ikiwa hakina mtu mwenye sifa za
kumfikia. Jambo hili lina uwezekano mkubwa wa kutokea kwa sababu ndani
ya DP, mwanasiasa pekee maarufu na anayefahamika ni Mtikila. Kuna
wanasiasa wengine kadhaa vijana lakini hawajafanikiwa kufahamika na kwa
sababu mgombea urais huuzwa kwa wananchi, kumuuza mtu mgeni katika siasa
za ushindani ni vigumu, ndiyo maana anaweza kupitishwa yeye mwenyewe
ili kukiweka chama chake kwenye nafasi ya kipekee.
Lakini jambo la pili linaloweza kumvusha ni kwa
sababu tayari ana uzoefu na kuihitaji nafasi hii mwaka 2005. Hili liko
wazi, kwamba DP inajua umuhimu wake kama Mtanzania aliyewahi kuzunguka
huku na kule na akapigiwa zaidi ya kura 30,000. Kwa mtu asiyejua siasa
anaweza kuzidharau kura hizo lakini wanaojua mambo ya siasa wanafahamu
ilivyo kazi kubwa hata kupata kura chache tu kwenye kinyang’anyiro
hicho. DP inaweza kumpitisha ili akaongeze wigo wa kura nyingine zaidi.
Nini kinaweza kumwangusha?
Jambo la kwanza linaloweza kumwangusha ni ikiwa chama chake
kitamtazama kama mtu mwenye misimamo mikali na anayeweza kukikosesha
chama hicho nafasi katika uchaguzi wa kisasa ambao unahitaji zaidi
kuzungumzia “masuala” na siyo watu au shutuma. Kama nilivyoeleza, kwa
kiasi kikubwa majukwaa ya Mtikila hutumika kushutumu watu, Serikali na
vitu kama hivyo. Ni mara chache mesikika akihutubia kuhusu ajenda za
kuzisimamia kwa mapana. DP inaweza kuhitaji kuondokana na staili hizo na
ikatafuta mwanzo mpya kwa kumweka mtu mwingine.
Lakini pili, matokeo ya mwaka 2005 ambayo yanaweza
kutafsiriwa kama hayakuwa mazuri, yanaweza kuchukuliwa kama sababu ya
kutompa nafasi, ili apatikane mwanachama mwingine ambaye ataweza kukipa
zaidi nafasi chama hicho.
Asipochaguliwa (Mpango B)
Asipochaguliwa atakuwa na masuala kama matatu:
Kwanza ni kuendelea na uchungaji katika kanisa
lake ambalo linaendelea kukua na hivyo linahitaji usimamizi. Nadhani
kazi hii ya uchungaji ni moja ya mambo muhimu kwake na ameshaizoea
vilivyo huku akichanganya na kudai haki za wananchi. Nauona uchungaji
kama karata muhimu pia ya kuendeleza karama yake ya siasa na nina hakika
ataendelea na kazi hii.
Lakini mpango wa pili nadhani ni kuendelea
kuongoza DP. Hadi sasa sijamsikia akitamka kuwa atastaafu muda mfupi
ujao, nadhani bado atakuwamo katika chama alichokiasisi na kwa sababu
siasa za Kiafrika ziko namna hii kwa kiasi kikubwa, naona ataendelea
kugombea na kuwa mwenyekiti kama jukumu jingine.
Mpango wa tatu utaendelea kuwa harakati za
ufunguzi wa kesi za kutetea wananchi na masuala makubwa ambayo yanakiuka
kikatiba. Kazi hii imo moyoni na kwenye damu yake na nina hakika kwamba
ataifanya kufa au kupona, hii ndiyo imejenga sifa yake na lazima
atakwenda nayo mbele zaidi kama moja ya mipango yake.
Hitimisho
Mtikila, ni mwanasiasa mtata, anayethubutu, mwenye
misimamo. Si rahisi kumfafanua hivihivi. Maisha yake ni harakati tokea
asubuhi hadi jioni, ukipishana naye anavyopenda kupanda bajaji au
pikipiki akiwahi mahakamani (siyo wakili) na ukimuona anavyosimamia
masuala makubwa katika nchi, huwezi kuamini kuwa mtu wa aina yake ndiye
hasa mwenye uwezo huo.
Kuongoza kanisa (uchungaji), kuongoza chama cha
siasa na kushinda mahakamani kupambana na Serikali kwenye kesi kubwa
kabisa ni mambo mchanganyiko mno na yanathibitisha kuwa mwanasiasa huyu
angepata chama chenye mtandao mkubwa katika nchi na akatumia uwezo wake
vizuri kwa masilahi mapana ya Taifa, angekuwa na mchango mkubwa kwa
jamii kuliko ilivyo sasa. Namtakia kila la heri kwenye safari yake
ambayo naamini ina maana kubwa na walau ina mchango wa kipekee katika
mapambano ya kidemokrasia hapa Tanzania.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment