Makongoro Nyerere akitangaza nia ya kugombea urais wakati wa mkutano
ulifanyika katika Kijiji cha Mwitongo, Butiama mkoani Mara jana.
Mtoto wa Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Charles Makongoro, ametangaza nia ya
kuwania urais, akisema anaomba kibali kuisaidia CCM iache rushwa,
kuparaganyika na atakapoingia madarakani, ili asiwaangushe Watanzania,
anahitaji chama imara kisicho na shaka kama ilivyo sasa.
Akitangaza nia hiyo nyumbani kwao Mwitongo,
Butiama jana, Makongoro alisema kutokana na CCM “kubakwa na vibaka,”
inawavunja moyo wanachama na inawakatisha tamaa Watanzania, hivyo
inahitaji kiongozi anayewarudishia matumaini.
“Sisi ndiyo wazalendo tunasema mnapotaka kutupora
hiki chama sisi tupo, turudishieni na mnapoturudishia kipitishie kwa
Makongoro Nyerere mna uhakika chama hiki hakipotei siyo kumkabidhi
kibaka,” alisema Makongoro. Kabla ya kutangaza nia hiyo alisema, “nitangaze
nisitangaze?, Nitangaze nisitangaze,” akajibiwa na watu waliohudhuria
hafla hiyo ‘tangazaaa...’.
Makongoro aliyesema Sh1 milioni za kuchukulia fomu
anazo hivyo haitaji kuchangiwa, alikataa kusoma hotuba iliyoandaliwa
kwa ajili ya kutaja vipaumbele vyake atakapoingia madarakani na
kuwashangaa wenzake waliotangaza nia kwa kutaja vipaumbele, kuwa
wanafanya faulo kwa sababu ilani ya chama haijatoka.
Alisema wametangaziwa na chama kuwa ilani itakuwa
tayari Julai na kwamba hawezi kutoa kipaumbele vyake halafu baadaye
vitofautiane na vitakavyobainishwa na chama ili asije kulaumiwa.
“Nipo hapa kukiri kwamba sehemu kubwa ya tatizo la
CCM ni kutofuata utaratibu, ukiona kuna kazi inaombwa kwa kufuata
utaratibu na wanaoomba hawafuati utaratibu hawa washtukie mapema,
hawafai,” alisema Makongoro na kuongeza: “Ukiona mtu anayeomba kazi na hafuati utaratibu
huo ilhali akiujua, ujue siku ukimpa kazi biashara ya kwanza akifika
pale ni kufuta utaratibu huo na kuweka wa kwake ili akae mpaka awe
mfalme wa nchi hii, usimpe!”
Makongoro alisema kibaya zaidi viongozi wa CCM
ambao wameshiriki kuweka utaratibu huo ndiyo wanahusika na kwamba,
ingawa kikao chake hakikuwa cha kuwataja kwa majina walioshiriki kuvunja
utaratibu huo lakini hana jinsi lazima awataje.
Aliwataja baadhi ya wagombea waliokwishatangaza
nia ndani ya chama hicho akisema wamekiuka utaratibu kwa kutoa ahadi
wakati ilani ya chama hao haijapitishwa na mkutano mkuu.
“Wewe (anamtaja mgombea) ni mjumbe wa NEC
umeshiriki na unajua kuwa rasimu ya ilani itapitishwa na Mkutano Mkuu wa
CCM, wewe unatangulia kimbelembele, nakuuliza wewe nani?”
Makongoro alimpiga kijembe mgombea mwingine
akisema hana wasiwasi na uadilifu wala uwezo wa kiongozi huyo lakini
hazingatii msamiati wa kung’atuka kwa kuwa amekuwapo ndani ya Serikali
kwa muda mrefu.
Kijembe kwa Rais Kikwete
Kuhamia upinzani 1995
Kijembe kwa Rais Kikwete
Kuhusu mtifuano miongoni mwa wanaCCM na tuhuma za
ufisadi dhidi a viongozi wa chama na Serikali, Makongoro alisema yote
hayo yanatokana na kosa la Rais Kikwete kuwapenda isivyo kifani marafiki
zake ambao huishia kumvunjia heshima.
“Kosa la Rais Kikwete ni kuwapenda sana marafiki
zake. Kwa bahati mbaya baadhi ya marafiki zake hao ni vibaka. Kibaka ni
kibaka tu hata akipewa gari la Serikali na kupeperusha bendera ya
Tanzania, bado ataendelea kuwa kibaka tu,” alisema Makongoro bila kutaja
majina.
Alisema haoni haya kukiri kuwa wamo vibaka ndani ya CCM kwa sababu hata vyama vya upinzani navyo vina vibaka wao. “Ni kujidanganya kusema hakuna vibaka ndani ya CCM
wakati wapo na wanatumia fedha zao, nyingine walizopata kwa wizi
kukivuruga chama,” alisisitiza Makongoro.
Kuhamia upinzani 1995
Akizungumzia uamuzi wake wa kuhamia upinzani mwaka
1995 alikogombea ubunge Jimbo la Arusha Mjini na kushinda kupitia Chama
cha NCCR – Mageuzi, Makongoro alisema mizengwe, rushwa na chama
kugeuzwa kuwa cha matajiri na wenye fedha ndicho kilichomkimbiza na
alipata baraka zote kutoka kwa baba yake Mwalimu Nyerere.
“Watu wataanza kusema kuhusu mimi kuhamia upinzani
na baadhi eti wanadai nina laana ya kukihama chama alichoasisi baba
yangu. Hivi kweli mie naonekana kama mtu mwenye laana? Hivi naonekana
kama mtu mlevi mimi?” alisema na kuhoji Makongoro na kuongeza:
“Mizengwe kwenye kura za maoni ndani ya CCM na
matumizi ya fedha kununua uongozi ndivyo vilinifanya kuhamia upinzani
baada ya wazee waadilifu ndani ya CCM kunishauri nihame ili wanipe fursa
ya kutumikia wananchi wa Arusha kupitia nafasi ya ubunge,” alisema
Makongoro.
Alisema baada ya kutangaza nia kugombea ubunge wa
Arusha Mjini mwaka 1995, huku akitiwa moyo na wazee na wanachama wengi,
alijikuta akikimbiwa na viongozi wote wa chama kila alipofanya ziara ya
kujinadi katika kata zote 17 za jimbo hilo wakati huo.
“Walionishauri kutoka CCM kwenda NCCR-Mageuzi ni
wazee na waasisi wa CCM. Kabla ya kuhamia upinzani, nilimwarifu Mwalimu
Nyerere na kupata baraka zake zote,” alisisitiza Makongoro.
Alisema ingawa alipanga kuhamia upinzani bila
kumweleza Mwalimu Nyerere, mke wake, Jaji Aisha Nyerere ndiye
aliyeshurutisha kupata kwanza baraka za mwasisi huyo wa Taifa ikabidi
yeye na mkewe wafunge safari hadi Dodoma kumtaarifu Mwalimu Nyerere
uamuzi huo huku akiwa na hofu ya kutopokewa wazo lake, ingawa matokeo
yalikuwa kinyume na hofu yake. “Nilihama CCM kwenda upinzani siyo kwa kupenda, bali nililazimishwa,” alisema.
Maradhi ya CCM
Kununua nyumba Ulaya, Dubai
Makundi ndani ya CCM
Maradhi ya CCM
Alisema: “CCM kinaugua maradhi ya kukaa madarakani
kwa muda mrefu na dalili za maradhi hayo ni kuteua wagombea bila kujali
matakwa ya wananchi.”
Alitaja dalili nyingine kuwa ni viongozi wa CCM kuzungumza maneno yasiyolingana na matendo yao. “CCM iongoze kwa matendo badala ya maneno. Chama
kinanuka rushwa. Taifa linanuka rushwa. CCM ichukue hatua na kutokomeza
rushwa na ufisadi unaotishia kuangamiza taifa letu. “Nikipata ruhusa ya chama changu na kibali cha
wananchi, nitaanza safari ya kuwaambia vibaka turudishieni chama chetu.
CCM ni chama cha wakulima na wafanyakazi, waturudishie chama chetu.”
Kununua nyumba Ulaya, Dubai
“Wapo waliotangaza nia ambao wanajinasibu kununua
nyuma Dubai na sehemu kadhaa huko Ulaya na kwingineko. Wasijidanganye
kwa sababu wakiharibu huku na kukimbilia huko watambue watakuwa
wakimbizi tu. Hapa ndipo petu sote,” alisema.
Alisema hata utajiri wanatuambia hivi sasa
wameupata wakiwa ndani ya CCM kwa sababu baadhi yao walikuwa maskini
walipojiunga na utumishi wa chama cha Serikali. “Fedha zote, nyingine halali na nyingine haramu
wamezipata ndani ya CCM. Sasa hawa waliotajirika kwa kuwamo ndani ya CCM
wanataka kukipore chama hiki kutoka mikononi mwa wananchi walio wengi.
Haiwezekani waturejeshee chama chetu,” alisema Makongoro.
Makundi ndani ya CCM
Akizungumzia makundi ndani ya CCM, hasa nyakati za
uchaguzi, Makongoro alisema anayachukia makundi ya siku hizi kwa sababu
yanakivunja chama kutokana na wahusika kutoyavunja uchaguzi
unapomalizika.
Mkono yuko na Makongoro
“CCM hivi sasa ina makundi. Kila mgombea ana timu yake na msingi
mkuu wa timu hizi ni fedha na wanaojiunga nayo wanafuata fedha. Leo hii
nikiwa na hela hata walioko kwa wagombea wengine wananifuata. “Binafsi sina kundi na ninayachukia sana haya
makundi kwa sababu yanakivuruga chama chetu. Wenye fedha wageuka
wafugaji wa watu badala ya mifugo. Yaani wenye fedha siku hizi
wanamiliki watu wakiwamo wajumbe wa halmashauri kuu. Haiwezekani,”
alisema Makongoro
Mkono yuko na Makongoro
Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ni Mbunge wa
Musoma Vijijini, Nimrod Mkono ambaye alisema watia nia waliokuwa
wanamfuata ili awaunge mkono kuanzia sasa “bye bye”, watambue yupo na
Makongoro Nyerere.
Mkono alisema wapo wengi waliokuwa wakitaka kujua
aliopo kati ya watia nia ya urais, “Mmesikia mengi, Simba wa Butiama
amekohoa hakuna mwingine. Makongoro ndiye aliyenifanya mimi kuwa mbunge,
amenitembeza kijiji kwa kijiji mngenishangaa kusikia niko kundi
jingine,” alisema Mkono na kuongeza: “Nitajitolea kwa hali na mali, nitamtembeza Makongoro nchi nzima, wale waliokuja kwangu bye bye niko kwa Makongoro.”
Alisema Makongoro ni miongoni mwa vijana
waliolelewa katika maadili ya itikadi za uongozi na pia ametoka katika
jiko la viongozi wa ngazi kubwa tangu ukoloni.
Mkono alisema Makongoro akiongoza nchi, kuna
uhakika wa kuwa katika mstari mmoja mnyoofu kwani hana hofu yoyote kwa
Watanzania katika kuendesha gurudumu la maendeleo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya, Samwel Kiboye
alisema Watanzania kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuadhimisha sikukuu
haitoshi, bali wafanye hivyo kwa kumkabidhi kijana wake Makongoro fimbo
ya kuwaongoza.
“Tukimkabidhi kijana wa Baba wa Taifa viatu vya
baba yake tutakuwa tumemuenzi kiuhakika Baba wa Taifa hili, kwanza
kijana huyu ni mwadilifu na pia ni kiongozi shupavu kwani mifano yake
tunayo na tulishaionja wakati akiwa mwenyekiti wa mkoa huu,” alisema
Kiboye.
Kiboye alisema Makongoro ni kati ya viongozi ambao
hawana harufu ya ufisadi, ubadhilifu wa aina yoyote wala si mla rushwa
hivyo endapo atapewa nafasi ataongoza katika misingi ya kuleta mafanikio
na kuondokana na kero zinazochangia kuondoa uzalendo wa nchi.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Shy – Rose
Bhanji alisema anaamini Makongoro ndiye kiongozi anayetakiwa kuvaa viatu
vya Baba wa Taifa kulingana na sifa alizonazo katika utendaji wake wa
kazi katika nafasi alizowahi kushika na aliyopo hivi sasa ya ubunge wa
Afrika Mashariki.
Apewa kifimbo
CHANZO: MWANANCHI
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Butiama, Yohana Mirumbe alisema
wanachama wa wilaya hiyo kwa pamoja wako tayari kumuunga mkono Makongoro
katika kugombea nafasi ya kuwa mgombea wa CCM katika nafasi ya urais.
Mirumbe alisema lengo ni kutaka kiongozi
atakayeweza kumalizia kazi itakayoachwa na rais aliyepo madarakani ya
kuongoza nchi na kuiweka katika hali ya kusaidia wananchi kuondokana na
hali ngumu ya maisha.
Apewa kifimbo
Mwenyekiti wa ukoo wa Burito ambaye pia ni Chifu
wa Kabila la Wazanaki, Japhet Wanzagi alisema Makongoro kutangaza nia
hakukosea, bali ni historia ya ukoo aliotoka kuwa na karama za kuongoza
tangu enzi za ukoloni kabla ya uongozi wa kisiasa.
Chifu Wanzagi alimkabidhi kifimbo Makongoro akitaka Watanzania kumsikiliza na kumwelewa. “Ukoo huu umekuwa ukitoa viongozi na kuaminiwa na
jamii. Makongoro anatoka ukoo wa kichifu, ukoo huu hata siku moja
haufanyi kitu kwa kubahatisha au kujaribu,” alisema Chifu Wanzagi na
kuongeza: “Kama tungekuwa na shaka na Makongoro,
tusingekubali asimame, kwa sababu angetushushia heshima kwa jamii,
Watanzania, Afrika na Dunia.”
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment