"Tunataka wote tujiandikishe na baada ya hapo, tutakwenda kuhakiki kama
majina yetu yapo ili siku ya uchaguzi tuweze kutekeleza lengo letu" Johnson.
Minja.
Jumuiya ya
Wafanyabiashara Tanzania, imejiandaa kuwabana wagombea wa urais kupitia
mdahalo maalumu kwa lengo la kuwachuja ili kupata mtu atakayeweza
kushughulikia kero zao na kukuza uchumi. Uamuzi huo unaelezwa kuchochewa na migogoro ya kimaslahi iliyoibuka baina ya wafanyabiashara na Serikali.
Katika siku za hivi karibuni kumeibuka mgogoro
baina ya pande hizo mbili uliotokana na mfumo mpya wa ulipaji kodi ambao
wafanyabiashara hao waliupinga kwa migomo na kufunga maduka.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Johnson Minja
aliliambia gazeti hili kuwa katika kuhakikisha dhamira yao hiyo ya
kuchuja wagombea inafanikiwa, wameanzia na hatua ya kuhamasishana
kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la
Wapigakura.
“ Ukweli ni kwamba tumebaini kuwa sisi siyo chama
cha siasa lakini kazi zetu zinaathiriwa na masuala ya kisiasa, kwa hiyo
tumejadiliana na kuona kuna umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika
kuhakikisha viongozi wenye maamuzi ambao hupatikana kwa njia ya uchaguzi
wanapatikana wenye uelewa na wenye nia ya dhati ya kukuza uchumi wetu,”
alisema.
Minja alisisitiza kuwa, “Tutashiriki kikamilifu
kuwasikiliza kwa makini wagombea wa nafasi ya udiwani na ubunge
watakapokuwa wanajinadi na kuchunguza kama kweli ahadi wanazozitoa
kuhusu kuondoa umasikini na kukuza uchumi zinatekelezeka au wanazitoa
ili kutulaghai wapate kura zetu,” alisema.
Alisema kwa nafasi ya urais wana mpango wa
kuhakikisha kwamba wanaandaa mdahalo mkubwa utakaowakutanisha wagombea
wa vyama vyote na watapata nafasi ya kujieleza na kuulizwa maswali, ili
kuwapima pia uelewa na uwezo wao katika masuala ya uchumi.
“Hii ni nafasi nyeti sana, tutapenda kuwasikiliza
kwa nafasi kwenye mdahalo huo ambao tunatarajia kufanya hapa Dar es
Salaam. Tunaamini kwamba tukipata rais mwenye uelewa mzuri na mwenye nia
ya dhati ya kukuza uchumi, atakuwa mstari wa mbele katika kutoa
vipaumbele vya kuwezesha fursa kwa wafanyabiashara kuwa rafiki na
kuondoa vikwazo,” alisema.
Minja, alisema rais mwenye uelewa katika masuala
ya uchumi, atakuwa na moyo wa kuhakikisha kwamba fursa za kuanzisha
viwanda vidogo vidogo nchini inapatikana.
“Jumuiya yetu hadi sasa ina wanachama 2,650,000 na
bado tunaendelea kuhamasisha wafanyabiashara ambao bado hawajajiunga
waingie. Sisi tunajitambua kwamba ni kiunganishi katika sekta zote iwe
wafanyakazi au wakulima kwa hiyo, tunatakiwa kufanya jitihada hizi ili
kuleta mabadiliko ya kiuchumi bila kuathiri siasa,” alisema Minja.
Alisema kuwa mwitikio wa kutimiza lengo hilo ni
mkubwa na tayari wameanzisha mtandao wa mawasiliano baina yao kuhusu
namna ya kutekeleza azima hiyo. “Tunataka wote tujiandikishe na baada ya hapo,
tutakwenda kuhakiki kama majina yetu yapo ili baada ya mdahalo siku ya
uchaguzi tuweze kuwa na nia moja ya kuwachagua viongozi watakaoweza
kutushawishi kwa hoja zao,” alisema Minja.
Minja alieleza pia kuwa wafanyabiashara hao wanaamini kuwa Tanzania ya leo inahitaji kiongozi bora na siyo bora kiongozi.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment