Mwigulu Nchemba.
Idadi ya makada wa CCM wanaotangaza nia kuwania
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho imezidi
kuongezeka, baada ya Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Stephen
Wasira na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kutagaza nia hiyo kwa
nyakati na maeneo tofauti jana.Wakati Wasira akitangaza nia hiyo mkoani Mwanza, Nchemba yeye alitangaza akiwa mkoani Dodoma.
MWINGULU KUWAINUA WALIMU
Mwigulu Nchemba, ametangaza nia ya kuwaniwa urais kwa kutaja mambo
sita ambayo serikali ya awamu ya tano inatakiwa kuyatekeleza ili kuleta
maendeleo ya nchi.
Alitangaza nia hiyo jana mjini hapa katika ukumbi wa Chuo cha
Mipango na kutaja mambo hayo kuwa ni kuipeleka nchi kuwa ya kipato cha
kati na kuwajengea wananchi uwezo wa kujenga uchumi wa kujitegemea. “Kazi ya serikali ya awamu ya tano ndiyo jambo la msingi la mkataba
wa Rais ajaye, kila awamu ilikuwa na kazi yake, awamu ya kwanza ilikuwa
ni kutafuta uhuru na umoja wa kitaifa, ya pili ni kubadili mfumo wa
uchumi na ya tatu ni kujenga taasisi na mifumo ya uchumi na ya nne ni
kujenga miundombinu, rasilimali watu na kujenga misingi ya uchumi.
Alisema kwa zaidi ya miaka 50 Taifa limekuwa tegemezi na hivyo
katika awamu ya tano mambo ya msingi yanayotakiwa kuzingatiwa ni kujenga
nidhamu ya matumzi ya fedha kwa kuziba mianya ya rushwa na kukomesha
kufanyakazi kwa mazoea. “Kiongozi akipatikana kwa mazoea atafanyakazi kwa mazoea, watu
wanaondelea kuchaguliwa kwa mazoea wanaongoza kwa mazoea, vita ya kwanza
nitakayoanza nayo ni kukomesha kufanyakazi kwa mazoea,” alisema.
Alisema jambo kubwa la kiongozi anayehitajika ni yule anayefahamu
mahitaji ya Watanzania wa sasa na kwamba Watanzania watambeba mtu
anayejua mahitaji yao. Alisema baadhi ya watu wanaongelea suala la uzoefu wa uongozi bila
kutambua kwamba uzoefu ni suala la kistarehe ambalo linaweza kufanywa na
kiongozi asiyefahamu shida za Watanzania.
Alisema yeye binafsi umaskini wa Watanzania anaufahamu hajausoma
wala kujifunza kutoka vitabuni bali anaujua kwani ameuishi tangu
alipozaliwa, hivyo kama chama chake na wananchi watampa ridhaa ya
kuongoza nchi, atakuwa na uwezo wa kupambana na tatizo hilo kwa kuwa
nalijua vizuri.
Alisema baadhi ya watu wanataka kuwayumbisha Watanzania katika
kumtafuta kiongozi wa nchi kwa kuzungumzia masuala ya ujana na uzee bila
kutambua kuwa mambo ya msingi yanayohitajika kwa kiongozi ni yule
ambaye ana uwezo, uadilifu, uzalendo na dhamira ya kweli ya kuwatoa
wananchi kwenye umaskini.
“Yameanza kuzungumzwa masuala ya kukaa muda mrefu serikalini,
lakini haiwezi ikawa sifa ya kutosha ya kuliongoza Taifa, unaweza ukawa
umekaa sana serikalini, lakini ukawa umelisabishia hasara kubwa taifa,”
alisema na kushangiliwa na hadhira iliyohudhuria mkutano huo.
Alitoa mfano wa Waziri Mkuu wa zamani, marehemu Edward Sokoine,
ambaye anakumbukwa kwa matendo yake na si kwa uzoefu wake kwani hakukaa
muda mrefu serikalini.
RUSHWA
Akizungumzia namna anatakavyokabiliana na rushwa, Nchemba alisema
katika serikali yake mtu yeyote atayakepatikana na hatia ya kashfa ya
rushwa atafukuzwa, atafilisiwa na atafungwa jela na hakutakuwa na
dhamana yoyote.
Alisema atabadilisha Sheria ya Takukuru Na. 11, 2007 na kutangaza rushwa kuwa ni janga la kitaifa. “Hii habari ya mtu anayekula rushwa anahamishwa kutoka sehemu moja
kwenda nyingine na matokeo yake kwenda kufanya ‘send off’ wakati kala
kodi za wananchi halitakuwapo katika serikali yangu na suala la rushwa
litashughulikiwa haraka sana,” alisema.
AJIRA
Alisema lazima kufanyike sensa ili kujua vijana ambao hawana kazi wakafanye kazi. Alisema kuna watu ambao wamemaliza mikataba yao ya kazi na
waendelea wakati kuna vijana mitaani waliosoma kwa kodi za Watanzania
hawana ajira.
MASHIRIKA YA UMMA
Alisema kuna watu wamegeuza fedha za mashirika ya umma kama zao kwa kula faida na familia zao. Alisema haiwezekani sungura akawa mdogo kwa wengine, lakini kwa wengine akawa mkubwa kama tembo. Aliongeza kuwa zaidi ya Sh. trilioni nane zinaenda nje ya bajeti,
jambo ambalo aliahidi atalisimamia ili kuondoa matatizo katika sekta ya
afya, elimu na miundombinu.
MIKOPO YA WANAFUNZI
Alisema atahakikisha kunakuwapo chanzo maalum cha mikopo ya elimu
ya juu ili kila mtoto anayepata nafasi ya kwenda chuo kikuu atimize
ndoto yake ya kwenda chuo kikuu.
ZANZIBAR
Mwigulu alisema serikali yake atasimamia Muungano na kuhakikisha
uchumi wa Zanzibar unapewa kipaumbele maana kuna nchi ambazo ni visiwa
zimefanikiwa na kuahidi kuiweka Zanzibar kwenye uangalizi maalumu. “Muungano huu umejengwa katika misingi ya kindugu hivyo unapaswa
kulindwa na kuenziwa kwa manufaa ya watu wetu” aliongeza kusema Nchemba.
Mashaka Mgeta na Daniel Mkate, Mwanza
WAZIRI wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Stephen Wasira, ametangaza
rasmi nia ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, huku
akionya kuwa Ikulu si mahali pa kumuweka kiongozi mwenye ‘harufu’ ya
rushwa na ufisadi.
Wasira amesema Tanzania ina tatizo kubwa la rushwa linalokwamisha
jitihada, mikakati na mipango ya maendeleo na ustawi wa wananchi. Kutokana na hali hiyo, Wasira alisema vita dhidi ya rushwa na
ufisadi havipaswi kutajwa kama maigizo, bali kuwa na dhamira na utashi
wa rais wa nchi na umma.
Aliyasema hayo jana jijini Mwanza wakati akizindua rasmi nia ya kutaka kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alisema hali ilivyo sasa, Tanzania imekithiri kwa rushwa kuanzia
ngazi za chini kwenye jamii hadi taifa, hivyo akiteuliwa na CCM na
hatimaye kushinda katika uchaguzi huo, miongoni mwa vipaumbele vyake
vitakuwa kuwashughulikia watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na
ufisadi.
Wasira alisema pamoja na nchi kuwa na sheria zinazopaswa kutumika
katika kudhibiti vitendo hivyo, inapaswa kuwa na rais asiyekuwa na
‘harufu’ ya rushwa. Alisema Ikulu siyo sehemu ya biashara na kwamba hakuna biashara inayofanyika mahali hapo.
Alisema amekaa Ikulu kwa miaka minne ya uongozi wa Rais Kikwete,
lakini hakuona biashara yoyote ikifanyika kwa kuwa hata simu za wageni
wote wanaofika pale huachwa mlangoni. “Ninaliongea hili si kwa sababu tu ninataka kuwa Rais, bali ni kwa
dhati ya moyo wangu na maslahi ya nchi yetu. Hivyo mnipime. Kumbukeni
katika maisha yangu yote ya kuwa kiongozi sijatajwa katika kashfa kama
za Escrow, EPA na nyingine,” alisema.
WASIRA KUPELEKA JEMBE LA MKONO MAKUMBUSHO
Wasira alisema uadilifu wake umejengwa katika maelekezo na
mafundisho aliyoyapata kuanzia utawala wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu
Julius Nyerere na `warithi’ wake, marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na
Benjamin Mkapa na Rais wa sasa, Jakaya Kikwete.
VIPAUMBELE
Wasira alitaja vipaumbele kadhaa atakavyovisimamia ikiwa atafanikiwa kushinda mchakato na hatimaye kuwa Rais.
UMOJA
Alisema ikiwa atachaguliwa kuwa Rais, serikali yake itaendeleza
umoja imara wa Watanzania wa imani, itikadi, rangi na tofauti za aina
yoyote, kwa vile ni msingi wa kuleta maendeleo na ustawi wa watu. Kwa hali hiyo alisema serikali yake itatetea na kulinda Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar na kuwaleta pamoja raia wote ili washiriki
kujenga uchumi wa nchi na kunufaika na rasilimali zilizopo.
Wasira alisema jamii inakabiliwa na matatizo mengi yanayohitaji mfumo na sera thabiti za jumla katika kufikia utatuzi wake.
ELIMU
Wasira alisema serikali ya CCM imefanikiwa kutekeleza mikakati
yenye lengo la kukuza kiwango cha elimu, hivyo jukumu la serikali yake
kama akichaguliwa kuwa rais, itakuwa ni kuiboresha sekta hiyo. Alisema ingawa sekta hiyo inapata kiasi kikubwa cha bajeti ya
serikali kuliko nyingine, serikali yake (akichaguliwa) itawekeza katika
matumizi ya sayansi ili wahitimu wamudu ushindani wa ajira na
mabadiliko ya teknolojia duniani.
UMASKINI
Wasira alisema pamoja takwimu za kuwapo ukuaji wa uchumi, lakini
Tanzania inakabiliwa na idadi kubwa ya masikini wanaofikia asilimia 28.2
ya raia zaidi ya milioni 43. Alisema sehemu kubwa ya watu maskini inapatikana vijijini ambapo
shughuli kubwa za uchumi wao ni kilimo cha mazao, uvuvi na ufugaji.
Kwa mujibu wa Wasira, uhalisia huo unasababisha umuhimu wa pekee
katika kuwekeza zaidi kwenye sekta za kilimo kwa kutumia teknolojia ya
kisasa kuanzia mkulima mmojamoja hadi wakulima wakuba na kuachana na
jembe la mkono ambalo linafaa kuwekwa jumba la makumbusho, ufugaji na
uvuvi ili ziendeshwe kwa mfumo wa kibiashara na kuchochea uboreshaji wa
maisha ya Watanzania walio wengi.
Wasira alisema umaskini hasa uliobobea maeneo ya vijijini
unasababisha watu kuhamia mijini pasipokuwa na ujuzi na taaluma, hivyo
kuibua tatizo la ongezeko la watu wa mijini wanaokabiliana na hali kama
hiyo (umaskini).
UBORESHAJI KILIMO
Alisema ikiwa atachaguliwa kuwa Rais, serikali yake itawekeza zaidi
katika kukifanya kilimo kuwa cha kibiashara kwa kuleta mapinduzi
yatakayowezesha wakulima kutumia nyenzo, teknolojia na mbinu za
kisayansi. Alisema hakuna jawabu lenye tija kwa kupambana na umasikini nchini
ikiwa kilimo kitaachwa kuwa miongoni mwa vipaumbele vya serikali.
“Haiwezekani tukazungumzia kuboresha kilimo kwa kutumia jembe la
mkono. Wakulima lazima watumie nyenzo za kisasa kama trekta hivyo
majembe ya mkono yatapelekwa kwenye majumba ya makumbusho,” alisema. Alisema pamoja na kutumia trekta, kutakuwa na uwezeshwaji wa
wakulima katika kutumia sayansi ya kilimo, utafiti kwa huduma za ugani
na uboreshaji wa miundombinu.
“Kwa ujumla unapokipuuzia kilimo ni sawa na kusema unawapuuzia watu wa hali ya chini walio wengi nchini,” alisema.
VIWANDA NA MASOKO
Wasira alisema ujenzi na kufufua viwanja vya ndani ni miongoni mwa
vipambele vyake ikiwa atachaguliwa kuwa Rais, kwa vile sekta hiyo
inaongeza thamani ya bidhaa na ajira kwa wananchi. Alisema kuendelea kuuza nje ya mazao ghafi kunachangia kuimarisha
viwanda na kukuza ajira za nje huku Watanzania wakiwamo wakulima
wakiendelea kubaki katika dimbwi la umaskini.
MIFUGO
Wasira alisema wafugaji ni sehemu ya jamii muhimu katika kukuza
uchumi wa nchi, hivyo ‘serikali yake’ itajielekeza katika kuwawezesha
wazalishe mazao yenye thamani yatakayohimili ushindani wa biashara na
masoko. Alisema ili kufanikisha hali hiyo, serikali yake itaibua mfumo bora
wa kuwapo mikopo kwa wafugaji na vifaa bora vya kisasa kwa wavuvi.
Wasira alisema kiwango cha uvuvi kinapaswa kukidhi wingi wa
rasilimali zake kama bahari, maziwa na mito hivyo kuifanya sekta hiyo
ichangia ukuaji uchumi na kuboresha maisha ya watu.
AJIRA KWA VIJANA
Wasira alisema ukosefu wa ajira kwa vijana ni tatizo lisilohitaji
kutajwa pasipo kuibua namna bora ya kuendeleza jitihada za serikali
katika kukabiliana nalo. Alisema vijana 200,000 wanaoajiriwa miongoni mwa milioni moja
wanaohitimu vyuo vikuu kila mwaka, ni wengi wanaohitaji namna bora ya
kuwawezesha wanufaike na mifumo tofauti ya biashara na uchumi.
Alitoa mfano kuwa uboreshaji wa mbinu, pembejeo za kilimo na
uanzishwaji wa viwanda vya kuongeza thamani za mazao ni moja ya maeneo
yatakayoongeza kwa vijana. Pia alisema vijana wanaojihusisha na ufundi kama wa vyuma, makenika
na bomba watawekea utaratibu bora wa kukuza kipato na kuongeza ajira.
“Tuna vijana wa ufundi kule Tabata Dampo na Gerezani, Dar es Salaam
na hapa Mwanza wapo Makoroboi ambao ni miongoni mwa wengi ambao kama
nikiwa Rais, nitaelekeza jitihada mahususi za kuwashirikisha katika
uchumi na biashara,” alisema.
AFYA
Wasira alisema sekta ya afya inakabiliwa na kero zikiwamo
zinazosababisha ukosefu wa dawa na kuathiri mipango kama ya bima za afya
kwa raia. Alisema kwa hali hiyo, serikali yake itaendeleza na kubuni mbinu
mpya za uboreshaji wa sekta ya afya iliyo kiini cha nguvukazi katika
uzalishaji.
MIUNDOMBINU
Wasira alisema ikiwa atakuwa Rais, uboreshaji wa miundombinu
utaelekezwa katika ujenzi na ukarabati wa njia za treni (reli) ili
pamoja na mambo mengine, kupunguza usafirishaji wa mizigo mikubwa
inayoharibu barabara.
WIZI SERIKALI
Wasira alithibitisha kuwapo kwa watumishi wasiokuwa waadilifu, wanaoendeleza vitendo vya wizi na ubadhirifu serikalini. Alisema ikiwa atakuwa Rais, atahakikisha ofisi ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anaongezewa nguvu za kisheria,
ikiwamo kuwafikisha mahakamani washukiwa wa vitendo hivyo.
“Haifai sana kwa CAG kuwabaini wezi wa fedha za umma halafu ampelekee Rais majina badala ya kuwafikisha mahakamani,” alisema. Kwa mujibu wa Wasira, kiasi kikubwa cha fedha za umma zinapotea serikalini kwa njia ya manunuzi.
AKEMEA KUMPONDA KIKWETE
Wasira alisema si sahihi kwa baadhi ya wanasiasa hasa waliomo ndani
ya CCM kuiponda serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kwa vile imefanikisha
utekelezaji wa ilani ya chama hicho kwa ufanisi mkubwa. “Nyerere alikuja na namna yake ya utawala, Mwinyi akaja na sera za
ruksa, Mkapa akaleta ukweli na uwazi na Rais Kikwete ni ari mpya, kasi
mpya na nguvu mpya. Sasa mimi ninakuja na hoja ya uadilifu kwa utumishi
wa umma,” alisema.
Mwisho
AINGIA MWANZA KIMYA, AONDOKA KWA SHANGWE
Wasira aliingia jijini Mwanza kimya-kimya bila kuwapo shamra shamra za hafla ya kutangaza nia ya kutaka kuwania urais. Juzi Wasira alifika jijini hapa saa 11 jioni na kwenda moja kwa
moja kwenye hoteli moja iliyopo maeneo ya katikati ya jiji, akiwa na
mke, watoto na watu wengine wa familia yake.
Saa 5:00 jana aliingia kwenye ukumbi wa Benki Kuu (BoT) eneo hilo halikuwa na watu wengi isipokuwa waliokuwa ndani. Lakini baada ya kuanza kuhutubia saa 5:09, idadi kubwa ya watu
iliongezeka nje ya ukumbi huo na wengine kusimama kandoni mwa barabara
ya Capri Point.
Walifuatilia hotuba ya Wasira kupitia runinga zilizowekwa nje ya
ukumbi huo, huku wengine wakiwa wanatumia redio na simu kumsikiliza
waziri huyo katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete. Baada ya hotuba yake, watu wengi walimfuata na kumpongeza, wengine
wakitaka kumbeba, lakini alikataa akisema: “Nashukuru, sipendi
niwasumbue, twendeni pamoja ndugu zangu.”
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment