Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya.
Kinyang'anyiro cha urais kupitia tiketi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM), jana kiliendelea kupamba moto baada ya wana-CCM
watatu kutangaza kwa nyakati na mahali tofauti nia ya kushika nafasi
hiyo ya uongozi wa juu kabisa nchini.
Waliotangaza nia hiyo jana ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi
Maalum), Prof. Mark Mwandosya, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki,
Makongoro Nyerere na Balozi Ali Karume.
Makada hao wa CCM walitangaza nia hiyo baada ya kutanguliwa na
makada wenzao watatuambao ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
aliyetangaza nia kama hiyo Jumamosi iliyopita, Waziri wa Kilimo, Chakula
na Ushirika, Steven Wasira na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba,
ambao walitangaza nia yao ya kuwania urais juzi kwa nyakati na maeneo
tofauti.
Hadi kufikia jana, jumla ya wana-CCM sita tayari wametangaza hadharani nia ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
PROFESA MWANDOSYA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya,
ametangaza nia yake ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kugombea nafasi ya urais kupitia chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Prof. Mwandosya alitangaza nia yake jijini Mbeya jana, huku akisema
kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa ni kujenga uchumi imara wa Taifa na
Watanzania kwa ujumla.
“Kwa muda mrefu watu wamekuwa wakiniuliza kuhusu mwaka 2015, ingawa
walikuwa hawasemi mwaka huo una nini, lakini niliwaelewa ingawa
niliendelea kukaa kimya kwa sababu ukimya ni moja ya haiba yangu…lakini
leo nimeamua kuvunja ukimya kwa kutangaza rasmi nia yangu kwamba
nakusudia kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama changu cha
Mapinduzi kuwa mgombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu,” alisema
Prof. Mwandosya.
UCHUMI IMARA
“Ikiwa nitateuliwa na chama changu na hatimaye kupata ridhaa ya
Watanzania kuwa rais wao, kipaumbele changu cha kwanza kitakuwa ni
kujenga uchumi imara kuanzia ngazi ya Taifa na kwa Watanzania wote kwa
ujumla, naamini kuwa uchumi ukiwa imara, mambo mengine yote yatafuata na
yatakwenda barabara,” alisema Prof. Mwandosya.
Alisema kuwa ingawa kazi ya kujenga uchumi iliyoanza kufanywa na
Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, na kuendelezwa kwa mafanikio na
Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, imekuwa na mafanikio makubwa,
lakini ukuaji wa uchumi wa Taifa bado haujamnufaisha mwananchi wa
kawaida, hasa wale wenye kipato cha chini.
Alisema kuwa endapo atafanikiwa kuwa rais wa nchi, kazi ya kwanza
itakuwa ni kujenga uchumi imara utakaokuwa na mfumo mzuri wa
kuwanufaisha wananchi wote.
KUBORESHA ELIMU
Aidha, Prof. Mwandosya alisema kuwa pamoja na kuimarisha uchumi,
pia anakusudia kuboresha sekta ya elimu ili kuhakikisha kuwa Taifa
linapambana kwa dhati na adui ujinga. Alisema kuwa akiingia madarakani, kwa kuanzia elimu ya msingi
itaanzia darasa la kwanza hadi kidato cha pili ingawa dhamira yake ni
kuona elimu ya msingi inaanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
“Tutaanza taratibu kuboresha sekta ya elimu na katika hatua ya
awali, tutaifanya elimu ya msingi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato
cha pili na baadaye tutahakikisha kuwa elimu hiyo ya msingi inafikia
kuwa ya kidato cha nne,” alisema Prof. Mwandosya.
Alisema kuwa lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha kuwa kila mtoto wa
Kitanzania anayefanikiwa kwenda shuleni, kiwango cha chini cha elimu
anayoipata kinakuwa ni ile ya kiwango cha kidato cha nne. Alisema kuwa uboreshaji wa sekta hiyo ya elimu utakwenda sambamba
na kuboresha mazingira ya watumishi wa sekta ya elimu kama vile
kuwajengea walimu nyumba za kuishi pamoja na kuboresha maslahi yao.
SEKTA YA AFYA
Prof. Mwandosya alisema kuwa Serikali atakayoiunda ikiwa
atachaguliwa kuwa Rais, itamulika katika sekta ya afya kwa kuhakikisha
inapunguza mazoea ya sasa ambayo yamejikita zaidi kwenye utoaji wa tiba
na kujielekeza zaidi katika kuwakinga Watanzania na maradhi.
Alisema kuwa nguvu zikiekelezwa kwenye kinga, itasaidia kupunguza
maambukizi ya magonjwa, hali ambayo pia itapunguza kwa kiwango kikubwa
gharama zinazoelekezwa kwenye tiba ya magonjwa hayo.
Alisema katika kufanikisha hilo, ni lazima jitihada zaidi
zielekezwe kwenye uwekaji wa mazingira katika hali ya usafi na pia
kuwajengea Watanzania tabia ya kujikinga na maradhi.
RUSHWA NA UFISADI
Prof. Mwandosya alisema serikali atakayoiunda ikiwa atachaguliwa
kuwa Rais wa Tanzania, itajenga mfumo imara wa kupambana na kuichukia
rushwa na ufisadi ambao anaamini kuwa ndiyo kiini cha kudumaza
maendeleo.
“Ni lazima tutajenga mfumo imara wa kuchukia na kupambana na rushwa
kwa sababu tusipochukua hatua madhubuti za kukabiliana na rushwa na
ufisadi, hata mambo mazuri tunayokusudia kuyafanya hayatapata
mafanikio,” alisema Prof. Mwandosya.
Katika hotuba yake, Prof. Mwandosya aliwaomba wana-CCM na
Watanzania wote kumuunga mkono ili achaguliwe kuliongoza taifa kwa kuwa
anaamini anao uwezo, nia na sababu ya kuwatumikia Watanzania.
Aidha, alisema kuwa anakusudia kwenda Dodoma kesho kwa ajili ya kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais.
ACHANGIWA FEDHA ZA FOMU
Baada ya tangazo hilo, wananchi walianza kumchangia fedha za kwenda kuchukulia fomu ambapo zaidi ya Sh. milioni 10 zilipatikana. Kabla ya kutoa hotuba yake, viongozi mbalimbali wa kimila, dini na
wanasiasa, walimzungumzia Prof. Mwandosya wengi wao wakimwelezea kuwa ni
mtu ambaye amelitumikia Taifa kwa muda mrefu, lakini hajawahi kupatwa
na kashfa ya aina yoyote.
MAKONGORO NYERERE
Mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere, ametangaza nia ya
kuwania urais wa awamu ya tano kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), huku akielezea sababu za kugombea ubunge wa Arusha Mjini na
kushinda mwaka 1995 kupitia chama cha NCCR-Mageuzi.
Akizungumza mbele ya umati wa watu waliokusanyika nyumbani kwa Baba
wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye pia ni baba yake,
Makongoro alisema kuhamia NCCR-Mageuzi kulitokana na kupewa baraka na
baba yake, hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
“Niliamua kugombea ubunge kupitia NCCR kutokana na kuambiwa sina
pesa za kuwahonga wana-CCM katika kura za maoni….nikaitwa na wazee wa
Tanu, (Mzee Mollel na Laizer) wa kule Arusha, wakaniambia nimwambie
Mwalimu Nyerere nigombee ubunge kupitia chama hicho cha upinzani
kutokana na kutokuwa na pesa,” alisema Nyerere.
Alisema licha ya Mwalimu kumpa baraka za kuhamia NCCR-Mageuzi,
lakini Katibu Mkuu wa zamani wa chama hicho, marehemu Dk. Lawrence Gama
na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ali Ameir Mohamed, walitoa baraka zao za
kuondoka CCM na kuhamia upinzani.
Alisema nia yake ya kuamua kutangaza nia ya kuutaka urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao ili apate
nafasi ya kuwakomesha mafisadi ndani ya CCM. Makongoro alisema nchi ina wanasiasa ‘uchwara’ ambao hukimbilia
kujiunga na CCM wakiwa maskini, lakini wanapokuwa ndani ya Chama
hutajirika bila kuelewa utajiri huo wanaupata toka wapi.
“Nikiingia madarakani, lazima CCM irejee katika mstari, kwani
nitawanyoosha mafisadi ambao lengo lao ni kujilimbikizia mali
wakiwa ndani ya chama,” alisema. Aidha, alisema makundi yaliyopo ndani ya chama hicho atahakikisha
yanamalizwa, kwani mara nyingi makundi yanatakiwa kuwapo wakati wa
kukaribia uchaguzi, lakini baada ya hapo Chama kinatakiwa kiwe kimoja na
kauli moja.
Alisema hata wakati wa utawala wa Marais Nyerere, Ali Hassan Mwinyi
na Benjamin Mkapa, makundi yalikuwapo na kuvunjwa baada ya Rais
kutangazwa, lakini awamu ya nne bado makundi yapo kwa miaka 10 sasa. Alisema hivi sasa wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmashauri
wamekuwa wakishurutishwa na viongozi wa CCM kutoa fedha za kufanyia
kampeni na baadhi ya mafisadi, lakini wanaposhindwa kufanya hivyo
huhamishwa kituo cha kazi.
“Hawa wakurugenzi hivi sasa wamekuwa sehemu ya timu za wagombea
uongozi, wanalazimishwa kutoa pesa kiasi wanachotakiwa, lakini pale
wanaposhindwa kufanya hivyo, huhamishwa kituo cha kazi,” alisema
Makongoro.
Hata hivyo, Makongoro hakutaka kueleza zaidi mambo atakayoyafanya akiwa madarakani zaidi ya kusema anasubiri ilani ya CCM. Awali, viongozi mbalimbali wa chama hicho, viongozi wa dini na
wazee wa kimila, walitoa baraka zao kwa mgombea huyo na kumhakikishia
atashinda uchaguzi mkuu ujao kwa nafasi anayoitaka.
CHIFU WANZAGI
Chifu wa kabila la Wazanaki, Japhet Wanzagi, alimkabidhi ‘kifimbo’
Makongoro kama ishara ya mafanikio ya nafasi aliyoiomba katika uchaguzi
ujao, kama mtu aliyetumwa na na ukoo wa Burito. “Mtu anayekabidhiwa kifimbo hiki ni yule anayeaminiwa na ukoo na
kukubalika ukoo huu haubahatishi na wala haufanyi majaribio kwani
tutajiondolea heshima,” alisema Chifu Wanzagi.
Alisema ukoo wa Burito hauna shaka na Makongoro ndiyo maana umeamua
kumsimamisha ili achukue nafasi hiyo kama alivyowahi kuongoza hayati
Mwalimu Nyerere, hivyo lazima (Makongoro) naye afuate nyayo hizo.
M/KITI WA WAZEE BUTIAMA
Mwenyekiti wa Wazee Butiama ambaye pia anawakilisha wazee wengine
nchini, Jack Nyamwaga, alisema wana imani na Makongoro kutangaza nia ya
kuwania nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kutokana na uwezo wake wa
utendaji. “Tunaamini Mungu atamfanikishia kupata nafasi hiyo kama ilivyokuwa kwa hayati Mwalimu Nyerere,” alisema Nyamwaga.
VIONGOZI WA DINI
Awali, Padre Daniel Hinc wa Shirika la Ufufuo Butiama, alimuombea
Makongoro kufanikiwa kupata nafasi hiyo kutokana na haja ya moyo wake. Naye Mchungaji wa Kanisa la Anglikana, Jacob Nyaganya, alisema ni
wakati wa Makongoro kuchukua uongozi wa nchi huku akimfananisha na Daud
aliyefanikiwa kumuua Goliath akiwa na umri mdogo.
Naye Sheikh Salum Isuko, aliyemwakilisha Sheikh wa mkoa, alitoa
baraka zake kwa Makongoro ili apate nafasi ya kuongoza nchi katika awamu
ijayo.
M/KITI CCM WILAYA
Yohana Mirumbe, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Butiama, alisema
wananchi wa wilaya hiyo wana imani na Makongoro kuwania nafasi hiyo. “Ameamua kufanya hivyo baada ya kuona shida za wananchi zinazidi
kushamiri na viongozi wengine wakinufaika kupitia mgongo wa Chama
chetu,” alisema Mirumbe.
MBUNGE NIMROD MKONO
Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, alisema Makongoro ni mtoto
anayetakiwa na wananchi wa wilaya hiyo na Tanzania kwa ujumla kutokana
na kufuata nyayo za hayati Baba wa Taifa. “Familia imemlea vizuri, si muoga wa vita kwani alishawahi kuingia
katika mapambano ya silaha 1979 katika Vita vya Kagera akiwa na cheo cha
Luteni…sasa vita hii ataiweza tu na kuingia madarakani,” alisema Mkono.
Alisema uwezo wa Makongoro ni mpaka sasa amekuwa Mbunge wa Afrika
Mashariki na kutokana na kukubalika kwake amechaguliwa kuwa Mwenyekiti
wa Bunge hilo.
SHY-ROSE BHANJI
Shy-Rose Bhanji, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, akiwa
anafanya kazi pamoja na Makongoro, alisema utendaji wa kazi wamtia nia
huyo unamshawishi kumuunga mkono wa kuwania urais wa Tanzania. “Katika Bunge la Afrika Mashariki, ameiletea nchi heshima kubwa
kutokana na michango yake anayoitoa ikiwa na uhakika zaidi,” alisema.
BALOZI ALI KARUME
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Balozi Ali Abeid Karume, jana alitangaza nia ya kugombea urais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akitaja kilimo kuwa kitakuwa
kipaumbele chake.
UHURU
Wakati akitangaza nia hiyo huko Dunga, katika ukumbi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Kati, Unguja, Balozi Karume alisema ikiwa atapata ridhaa
ya CCM na ya wananchi ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
atahakikisha raia wake wanakuwa na uhuru wa kuchagua chama na dini bila
ya kuvunja sheria za nchi. Karume ambaye ni mwanadiplomasia wa siku nyingi, alisema pia kila
raia wa Tanzania atakuwa na uhuru wa kujituma na kufanya biashara ili
kujitafutia riziki.
“Sitaki kuona serikali nitakayoiongoza kuwa kikwazo cha kuwazuia
watu kufanya biashara, mfano; mtu anataka kuuza njugu mpaka awe na
leseni, kwani anataka kuendesha gari?” alihoji Balozi Karume.
Balozi Karume ambaye pia ni mtoto wa pili wa Rais wa kwanza wa
Zanzibar, alisema atahakikisha kila mtu atakuwa na uhuru wa kuepukana na
njaa na kuhakikisha serikali ndio itakayofidia bei ya mazao ya
wakulima.
RUSHWA, UFISADI
Pia alisema kuwa atahakikisha anatafuta misingi na vichocheo
vinavyosababisha rushwa ili kuitokomeza ikiwamo kuondoa vikwazo ambavyo
havina maana akiamini kuwa ndivyo vinavyosababisha rushwa pamoja na
kukemea ufisadi.
Alisema atahakikisha anayaendeleza yale yote aliyoacha Rais Jakaya
Kikwete na kamwe hatambeza kwa yale yote aliyowafanyia Watanzania wakati
akiiongoza nchi. Balozi Karume alitumia nafasi hiyo kuwapiga vijembe wagombea
waliotangulia kutangaza nia na kusema kuwa wapo baadhi ya wagombea ambao
wametangaza wanataka kuunda Tanzania mpya, jambo ambalo haliwezekani
kwani Tanzania ni hiyo hiyo na haiwezi kuwa nyingine.
Hata hivyo, alisema wapo watu waliosema hawatakubali Kilimo Kwanza na watawekeza kwenye elimu. Alisema hata yeye atawekeza kwenye elimu, lakini na suala la
kilimo ni muhimu sana katika nchi kwani historia ya nchi inatokana na
kilimo. “Kama hujawa na kilimo ukapata chakula, kweli hutaweza kusoma na njaa, haiwezekani, lazima ushibe ndiyo usome,” alisema.
Alitaja sifa za rais ajaye kuwa anatakiwa awe nazo huku akieleza
kuwa kwa upande wake sifa hizo anazo na anaweza kuongoza nchi. Miongoni
mwa sifa hizo ni rais ajaye awe muadilifu, awe na elimu, awe na
uzalendo, awe mwanasiasa mkongwe wa CCM, aijue dunia na kuwa kiungo
kizuri kati ya Tanzania na nchi nyingine duniani na awe balozi ambaye
ameshaiwakilisha Tanzania katika nchi za Ulaya.
“Hatutaki rais ambaye hata dunia haijui wala hawezi kuzungumza na
viongozi wengine wa nchi za nje na wala hatutaki rais kila anachoambiwa
anasema yes, sir au ok, tunataka rais atakayeweza kuzungumza kwa
ufasaha,” alisema Balozi Karume, ambaye aliiwakilisha Tanzania kwa miaka
mingi akiwa Balozi katika nchi kadhaa za Ulaya.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment