Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia ameijia
juu serikali kwa kudai inaendelea kudidimiza elimu nchini kwa kuzindua
sera ya elimu yenye upungufu mkubwa.
Akichangia katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka wa fedha 2015/2016 jana,
Mbatia alisema inashangaza kuona kuwa sera ya elimu iliyozinduliwa na
Rais Kikwete kwa mbwembwe imejaa malalamiko na changamoto kana kwamba
serikali inajilalamikia yenyewe na hivyo kunahitajika sera inayozingatia
usawa.
"Sera ya elimu iliyozinduliwa na Rais ina mapungufu na makosa mengi
na hali hii ndiyo maana hata mikataba ya kifisadi yenye utata
inasainiwa bila kuhaririwa kutokana na kukosekana kwa umakini,” alisema.
Mbatia alisema ikiwa serikali itaanza na sera mbovu, ni wazi kuwa
hata mitaala ya elimu itakuwa mibovu na hali hiyo inaonyesha kuwa
serikali ya CCM imechoka; hivyo inahitaji watu wengine wenye dhamira ya
kweli katika kuikomboa nchi.
KAMBI YA UPINZANI
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeponda sera hiyo ya elimu kwa
kudai kuwa ni dhaifu na pia mitaala ya elimu mibovu nchini
inayosababisha nchi kuendelea kushika mkia katika nchi za Afrika
Mashariki.
Kadhalika, imeitaka serikali kuiagiza Tume ya Vyuo Vikuu (TCU)
kutoa ndani ya siku sitini mwongozo mpya wa vyuo vya elimu ya juu nchini
kuhusu vigezo vya kuzingatia wakati wa kuandaa mitaala ya elimu ya juu.
Aidha, imeitaka serikali kuiagiza Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kutoa
ndani ya siku sitini mwongozo mpya wa vyuo vya elimu ya juu nchini
kuhusu vigezo vya kuzingatia wakati wa kuandaa mitaala ya elimu ya juu.
Akiwasilisha hotuba ya kambi hiyo jana bungeni kwa Wizara ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, Msemaji wa Kambi hiyo, Susan Lyimo, alisema elimu
haijawahi kuwa kipaumbele katika sera za awamu zote nne za Serikali ya
CCM ndio maana haitekelezi hata ilani yake yenyewe.
Kambi hiyo ilisema ni wazi serikali haijawekeza vya kutosha katika elimu kutokana na kudhihirika kwenye bajeti zinazotengwa. “Ikumbukwe hata hizo zinazotengwa ni asilimia kidogo zilizokwenda kwa wastani wa 50 au chini hadi Machi 2015,” alisema.
Aidha, alisema takwimu zinaonyesha kuwa katika nchi za Afrka
Mashariki Kenya imetumia asilimia 7.8 ya GDP katika elimu huku Tanzania
ikitoa asilimia 1.49 ya GDP, Uganda asilimia 5.8 na Rwanda asilimia 4.8.
Alisema ni jambo la kuchekesha pale serikali inapotamba kuwa elimu
imefanikiwa kwa asilimia 81 katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN),
huku walimu ambao ni watendaji wakuu wakiwa hawajatekelezewa maslahi
yao.
Lyimo alisema uchambuzi unaonyesha kuwa bado kiwango cha fedha za
bajeti ya sekta kinachopangwa ni asilimia kati ya 15 – 17 cha bajeti
nzima ya serikali kiwango ambacho Tanzania haijaweza kufikia
kilichokubaliwa cha Azimio la Dakar, Senegal chini ya EFA, cha kuwekeza
hadi walau asilimia 20 ya bajeti ya Taifa katika elimu.
Alisema kambi yake inaitaka serikali kuvifungia mara moja vyuo
vyote vya elimu ya juu vinavyoendeshwa kwa maslahi ya kibiashara zaidi
bila kuzingatia mitaala na ubora wa elimu mpaka hapo vitakapojirekebisha.
Kambi hiyo imehoji Tanzania inafuata falsafa gani ya elimu kwa sasa
kwa kuwa wakati wa hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, nchi ilikuwa
ikifuata falsafa ya “Elimu ya Kujitegemea” ambayo ilimwezesha
aliyenufaika kujiajiri katika sekta mbalimbali za uzalishaji mali.
Alisema Sera ya Elimu inasema serikali itahakikisha kuwa elimu ya
msingi katika mfumo wa umma inatolewa bila ada. Kambi hiyo imeitaka
serikali kulithibitishia Bunge kama elimu bila ada itaanza kutolewa kwa
mwaka wa fedha 2015/16 au tamko hilo la sera lilikuwa ni la kisiasa. “Sera ya Elimu Kwanza ni sera ya upinzani ipo katika ilani ya
uchaguzi ya Chadema 2005, na 2010 na imepewa kipaumbele cha kwanza, cha
pili na cha tatu,” alisema.
Alisema Chadema iliposema elimu itakuwa bure kama ingechaguliwa
kuunda serikali mwaka 2005 na 2010, CCM iliendesha propaganda na
kuwapotosha wananchi kwamba haiwezekani kutoa elimu bure. Akizungumzia shule binafsi, Lyimo alisema kumekuwa na malalamiko
mengi kuhusu gharama za shule hizo kuwa kubwa kiasi cha wananchi
wachache tu ndio wanaoweza kuwalipia watoto wao.
Alisema jambo hilo limeleta matabaka katika utoaji wa elimu kwani
inaonekana shule za serikali ni kwa ajili ya watu maskini na shule
binafsi ni kwa ajili ya watoto wa matajiri. “Bunge hili limefanya jitihada gani kuwianisha gharama za elimu
kati ya shule binafasi na shule za serikali ili kuondoa matabaka katika
utoaji elimu,” alisema.
MATATIZO ELIMU YA JUU
Ilisema pamoja na tafiti kuonyesha Tanzania ilivyo nyuma katika
ubora wa elimu ya juu, sasa hivi kumezuka tatizo kubwa la utofauti wa
mitaala ya vyuo vikuu hasa vya binafsi hali inayosababisha migomo na
sintofahamu miongoni mwa wanafunzi. “Mfano vyuo vya St. Joseph na Kampala International University
(KIU). Kwa muda mrefu tatizo hili limefikishwa kwa wahusika na bado
ufumbuzi wa kina haujajulikana,” alisema.
Alisema tofauti kubwa ya mitaala ya elimu ya juu kati ya vyuo vya
elimu ya juu vya serikali na binafasi imesababishwa na kuongezeka kwa
kasi kwa vyuo vya elimu ya juu nchini kutokana na ongezeko la watu
wanaohitaji elimu lakini elimu ya vyuo binafsi inatolewa kibiashara
zaidi kuliko huduma.
BODI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU
Ilisema wanafunzi wengi hawapati fedha kwa wakati hali inayoleta
adha kubwa kwani wengi wao wanatoka kwenye familia duni na kwamba hata
inapotolewa inatolewa kibaguzi.
Ilisema tangu kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo, kumekuwa na changamoto
nyingi kuhusu elimu ya juu hadi Rais alipoteua Tume chini ya Prof.
Maoko Makenya kushugulikia matatizo ya mikopo ya elimu ya juu lakini
ripoti ya tume hiyo haijawekwa hadharani na bado matatizo ya mikopo ya
wanafunzi iko pale pale.
Kambi hiyo ilitaka kujua ni kwanini serikali haitoi fedha ya mikopo
hadi wanafunzi wagome na kuandamana, ni wapi fedha hizo zinakwenda hasa
ikizingatiwa asilimia 100 ni za ndani na kwa nini ndani ya masaa 12 tu
ya mgomo wa UDSM Mei 15, mwaka huu fedha zilitoka.
BRN
Ilisema BRN ya Elimu ilibainisha wazi kutoa ruzuku ya asilimia 100
yaani Sh. 10,000 kwa kila mwanafunzi shule za msingi na Sh. 25,000 kwa
shule za sekondari, lakini utekelezaji umekuwa kwa asilimia 42 kwa shule
za msingi na asilimia 48 kwa sekondari. Wakichangia wabunge, waliibana Wizara hiyo kwa kushindwa kutatua
tatizo la mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya Elimu ya juu hali ambayo
imesababisha elimu ya Tanzania kuwa mahututi .
RACHEL MASHISHANGA
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Rachel Mashishanga, alisema suala
la mikopo kwa wanafunzi limekuwa tatizo la muda mrefu kutokana na
urasimu unaofanywa na baadhi ya vyombo vinavyohusika na mchakato wa
utoaji wa mikopo hiyo. "Mikopo wanapewa watoto wanaotoka katika familia zenye uwezo wakati
wanaotoka familia duni hawanufaiki, kuna urasimu ambao serikali lazima
itafute ufumbuzi kutatua tatizo hilo,” alisema.
Mashishanga alisema wakati umefika kwa serikali kujipanga
kuhakikisha mikopo inayotolewa na serikali kwa wanafunzi wa vyuo vya
Elimu ya juu inanufaisha hata wanafunzi wanaotoka familia duni. Alisema serikali ya CCM kimsingi imeshindwa kuboresha elimu nchini
kwa miaka 50 sasa na kwamba ni wakati sasa kwa wananchi kufanya
mabadiliko katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.
GRACE PUJA
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Grace Puja, alisema ili wanafunzi wote
wanufaike na mikopo serikali iweke utaratibu ianze kutolewa kupitia
kwenye mabenki. “Nchi za wenzetu kama vile Marekani na Canada wanafunzi huwa
wanakwepa sana mikopo kwa hiyo na sisi tungeanza utaratibu mikopo iwe
inatolewa kwenye mabenki ili mwanafunzi anapokopa atambue kuwa huo ni
mkopo analazimika kuurejesha,” alisema.
SUZAN LYIMO
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Lyimo, alisema mwaka 2005
serikali iliunda tume kuchunguza changamoto zinazoikabili sekta ya elimu
ikiwamo mikopo ya wanafunzi, lakini tume hiyo imekula pesa tu hakuna
kilichofanyika.
JAMES MBATIA
Naye Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia, alisema sera ya
elimu iliyozinduliwa na Rais kwa mbwebwe ina mapungufu makubwa sana hali
ambayo inazidi kuifanya elimu kuwa mahututi. Alisema jambo la kushangaza ni kuwa sera hiyo imejaa malalamiko na
changamoto kana kwamba serikali inajilalamikia yenyewe na kwamba
kunahitajika sera inayozingatia usawa.
"Sera ya elimu iliyozinduliwa na Rais ina mapungufu na makosa mengi
na hali hii ndiyo maana hata mikataba ya kifisadi yenye utata
inasainiwa bila kuhaririwa kutokana na kukosekana kwa umakini,” alisema.
Mbatia alisema kama tukianza na sera mbovu ni wazi kuwa hata
mitaala ya elimu itakuwa mibovu na kwamba hali hiyo inaonyesha kuwa
serikali ya CCM imechoka hivyo inahitaji watu wengine wenye dhamira ya
kweli kuikomboa nchi.
MARGARETH SITTA
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Margaret Sitta,
alisema Rais Jakaya Kikwete,aliahidi kabla ya mkutano wa 20 wa Bunge
kumalizika serikali itaanzisha chombo cha kushughulikia malalamiko ya
walimu. Alisema ili kuwa na ubora wa elimu, serikali ihakikishe inaboresha
idara ya ukaguzi ambayo kwa sasa imetelekezwa kwa kutokuwa na vitendea
kazi.
Sitta alisema hivi sasa usajili wa shule mpya uzingatie zaidi ubora
na miundombinu mizuri kwani hivi sasa kuna shule nyingi zimesajiliwa,
lakini baadhi hazina ubora unaotakiwa.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment