Balozi Ali Karume akizungumza na wanachama wa CCM katika Ofisi za
Halmashauri ya Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja jana.
Mwanadiplomasia
mashuhuri visiwani Zanzibar, Balozi Ali Karume ametangaza nia ya
kuchukua fomu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kuwania
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Balozi Karume alitangaza nia yake hiyo jana katika
Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kati Unguja na kuahidi kuwa iwapo
chama chake kitampitisha na kupata ridhaa ya kuingia Ikulu, atatoa uhuru
wa kujieleza kwa wananchi wake na uhuru wa kuikosoa Serikali bila ya
kuvunja sheria na katiba ya nchi.
Alitumia muda mwingi kuelezea historia na uzoefu
wake wa uongozi ndani ya chama na Serikali na kuwataka Watanzania
kutokurupuka kumchagua rais kama watataka maendeleo endelevu.
Balozi Karume alisema ameamua kugombea nafasi hiyo
ya urais, baada ya kujipima na kuona ana sifa na uwezo wa kuliongoza
Taifa la Tanzania na akawakumbusha wagombea wenzake umuhimu wa kuwa na
kiongozi atakayeweza kujenga umoja na kudumisha amani miongoni mwa
Watanzania.
“Ni wakati wa kufikiria na kutukuza utaifa wetu,
badala ya Utanganyika na Uzanzibari,” alisema Balozi Karume katika
mkutano wake huo uliochukua takriban saa moja na nusu.
Kwa mujibu wa Balozi Karume, urais unahitaji
kiongozi mwenye sifa na uadilifu atakayepiga vita vitendo vya ubadhirifu
na kukemea rushwa ili kujenga Taifa lenye kufuata misingi ya sheria na
utawala bora.
“Uongozi si suala la majaribio, hivyo ni wajibu wa
kila Mtanzania kuwa makini na watu ambao walishawahi kupewa uongozi na
kushindwa kutokana na kukosa uadilifu,” alisema Balozi Karume.
Hata hivyo, alisema kwamba atahakikisha
anaendeleza mipango yote ya maendeleo iliyoanzishwa na Rais Jakaya
Kikwete na kukabiliana na kero mbalimbali zinazowakabili Watanzania hasa
suala la umaskini, maradhi na elimu.
Vipaumbele vyake
Akizungumza katika shamrashamra za kutangaza nia
hiyo, Balozi Karume alisema lengo lake ni kuwania nafasi hiyo ya juu
serikalini ili kupokezana kijiti na kuendeleza mambo yote mazuri
yaliyoanzishwa na mtangulizi wake, Rais Jakaya Kikwete.
Balozi Karume alitaja kipaumbele chake cha kwanza
kuwa ni uhuru wa watu wote. “Kila mtu ana haki ya kuwa na uhuru wa
kujiamulia mambo yake kuwa muumini wa dini au chama chochote cha siasa
tena bila kubughudhiwa na mtu mwingine.
“Mkombozi wa mwananchi ni kuimarisha kilimo kwanza, elimu baadaye, huwezi kusoma huku ukiwa na njaa na hilo ndilo lengo nikipata ridhaa ya kuwa Rais wa Muungano” alisema Balozi Karume.
“Mkombozi wa mwananchi ni kuimarisha kilimo kwanza, elimu baadaye, huwezi kusoma huku ukiwa na njaa na hilo ndilo lengo nikipata ridhaa ya kuwa Rais wa Muungano” alisema Balozi Karume.
Alisema Tanzania ili iweze kujenga uchumi imara, inahitaji
kiongozi mwenye mbinu na uwezo wa kupambana na rushwa na ufisadi kwa
vile ndiyo adui wakubwa wa maendeleo yake.
Alisema kuwa atahakikisha Watanzania wanapata
uhuru wa kuchagua chama wanachotaka, uhuru wa kuabudu dini wanayotaka na
kufanya biashara katika mazingira bora pamoja na kufungua milango ya
uwekezaji yenye masilahi kwa Serikali na wananchi wake.
Alisema uhuru atakaousimamia pia utahusu uhuru wa
kujituma na kufanya biashara bila kuwekewa vikwazo, kwani nayo ni haki
ya msingi ya wananchi wa Tanzania.
“Uhuru wa kujituma ni muhimu sana kwa kila mtu
siyo mtu anataka kuuza njugu wewe unamwambia huna leseni… leseni kwani
anataka kuendesha gari? Mtu akitaka kuendesha gari ndiyo mdai leseni,
lakini siyo kuuza njugu lazima watu wapewe uhuru wa kujituma,” alisema
Balozi Karume.
Balozi alieleza kuwa atasimamia uhuru wa kuepukana
na njaa kwa kusimamia uanzishwaji wa viwanda ili kusindika mazao na
bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuziongezea thamani.
Karume alitumia muda mwingi kuelezea historia ya
nchi na CCM akieleza kuwa ni muhimu kwa wanachama hao kuwachagua
viongozi wenye uelewa mzuri wa kimataifa na siyo watu ambao
wanasindikiza na kutia aibu mbele ya mabalozi wa nchi za nje.
“Hatutaki mtu wa okay, sir au yes sir! Tunataka
mgombea urais ambaye anaelewa mambo ya kidiplomasia na anajua kuzungumza
na mataifa mbalimbali siyo anakwenda Ulaya anashindwa kuongea badala
yake anaitikia tu yes sir,” alisema.
Balozi Karume amewataka wanachama wa CCM
kuwachagua viongozi kwa vigezo vya uwezo na uadilifu na siyo kwa sababu
wamekaa muda fulani katika matawi na mashina ya chama hicho tawala, huku
akielezea jinsi gani wao walivyopikwa katika chama hicho.
Aidha, aliwapiga vijembe wenzake waliotangulia
akisema wapo baadhi ya wagombea ambao wametangaza anataka kuunda
Tanzania mpya jambo ambalo alisema haliwezekani kwani Tanzania ni
hiyohiyo na haiwezi kuwa nyingine.
Alisema watu waliosema hawatakubali kilimo kwanza
na badala yake watawekeza kwenye elimu wamekosea, kwani ingawa elimu ni
muhimu, kilimo nacho bado ni muhimu pia.
Ilivyokuwa ukumbini
Balozi Karume aliwasili katika Ukumbi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kati mkoani Unguja saa 9:45 jioni akiwa
ameambatana na Zainabu Shamori ambaye amewahi kuwa Katibu wa CCM Mkoa wa
Kusini Pemba na Kusini Unguja.
Pia, Zainabu amewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya, Zanzibar wakati
wa uongozi wa Rais Amani Abeid Karume na aliwahi kuwa Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).
Baada ya Balozi Karume kuwasili katika ukumbi huo
alipokewa na wapambe wake ambao ni wanachama wa CCM na baadhi ya
wafanyabiashara waliokuwa wakiimba na kushangilia kwa kupiga makofi muda
wote.
Balozi huyo alipopanda jukwaani, kundi la watu
waliokuwapo ukumbini ambao idadi yao haikufika 100, waliendelea kuimba
na kushangilia kwa kupiga makofi. Hata hivyo, hapakuwapo na shamrashamra
za ngoma.
Licha ya uchache wao, watu hao walionekana wenye
furaha na kumshangilia Balozi Karume kwa kila neno alilokuwa akisema
hasa pale alipoelezea namna atakavyopambana kuondoka rushwa na ufisadi
unaoitafuta Serikali na kudhoofisha uchumi.
Huku akiendelea kushangiliwa, Balozi Karume
alisema kwamba Rais mstaafu Karume, ambaye ni kaka yake, alisema kuwa
katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu ni vizuri apatikane rais mwenye uzoefu wa
kimataifa.
“Rais alisema ni vizuri apatikane rais ambaye
atakuwa ametembea nchi mbalimbali ili ajue uzoefu wa mataifa mengine
yanayofanya kazi,” alisema Balozi Karume.
Balozi huyo aliongeza kuwa uzoefu wa kimataifa ni
sifa muhimu kutokana na kasi ya maendeleo ya kiuchumi inayoendelea
duniani hivi sasa.
Katika mkutano huo wa Balozi Karume, hakuna
viongozi maarufu waliopo madarakani au wastaafu waliomsindikiza kama
ambavyo imekuwa kwa baadhi ya wanasiasa wanaotangaza nia ya kuwania
nafasi ya kuteuliwa na vyama vyao kugombea urais.
Siyo mara ya kwanza
Balozi Karume aliwahi kugombea urais wa Zanzibar
mwaka 2000, lakini alijitoa katika hatua za awali na kumwachia Rais
Karume, pia mwaka 2005 na mwaka 2010, aligombea urais wa Tanzania Bara.
Wakati akiondoka ukumbini baada ya kutangaza nia
jana, Balozi Karume alitumia muda mwingi kusalimia wanachama waliokuwapo
ukumbini kwa kuwapa mikono.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment