Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB), imesema ilichelewa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu
nchini kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo kuchelewa kwa fedha
kutoka serikalini, marejesho madogo ya mikopo na uchache wa fedha
zilizokusanywa.
Akizungumza na NIPASHE, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na
Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, alisema HESLB ilishindwa
kupeleka fedha kwa wakati kutokana na vyanzo vilivyotegemewa kutoa fedha
kuchelewesha huku akisisitiza kuwa fedha iliyokwisha kusanywa haikuweza
kutosheleza idadi ya wanafunzi wenye mahitaji.
“Siyo kama inavyoelezwa na vyombo vya habari, mikopo katika mihula
yote ya kwanza ilitolewa kwa wakati, katika kipindi hiki cha muhula wa
mwisho wa masomo mikopo imechelewa kwa sababu ya fedha zinazotengwa kwa
ajili ya mikopo kuchelewa na urudishaji wa mikopo usioridhisha, alisema
Mwaisobwa.
Aidha, alisema mikopo haikuchelewa kupelekwa katika vyuo vyote
vyenye wanafunzi wenye mahitaji na kuongeza kuwa hata vyuo vilivyofanya
migomo, baadhi ya vitivo vilikuwa vimepatiwa mikopo. Alisisitiza kuwa HESLB imeshapeleka fedha za mikopo kwenye vyuo
vyote na kuwa vyuo ambavyo wanafunzi hawajapokea, vina utaratibu wake wa
kuwapatia fedha hizo.
Hivi karibuni, wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini vikiwamo Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Chuo Kikuu cha
Mtakatifu Joseph, Chuo Kikuu cha Iringa na Chuo Kikuu Kishiriki cha
Ualimu cha Dar es Salaam (DUCE) waligomea masomo kuishinikiza serikali
kupitia HESLB kuwapatia fedha za kujikimu.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment