Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana
na Kliniki ya Lotus, imeanzisha kampeni mpya inayolenga kuelimisha umma
kuhusu ugonjwa wa usonji (autism), ambao Watanzania wengi hawaufahamu.
Ugonjwa huu kwa sasa unatishia familia nyingi kwani dalili zake huanza utotoni na huendelea hadi ukubwani. Mwenyekiti wa Chama cha Kuhudumia watu wenye Usonji Tanzania, Dk.
Stella Rwezaula, kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, aliishukuru
Kliniki ya Lotus kwa kuwa mstari wa mbele kuanzisha kampeni hiyo ili
kuwaelimisha Watanzania kuhusu ugonjwa huo.
“Ni vyema ugonjwa huu ukigundulika mapema na kutibiwa ili
aliyeathirika apone na kuishi maisha ya kawaida hapo baadaye kulingana
na athari aliyoipata. Mtoto kuanzia miaka 0-6, anaweza kutibiwa vizuri
na kusaidia kubadilisha maisha yake,” alisema.
Alisema watoto wenye hali hii wana shida katika kuwasiliana na
tabia zao ni kurudia rudia mambo anayofanya mara kwa mara na pia watu
wengi wenye ugonjwa huu wana namna yao ya kujifunza, kusikiliza na
kuitika.
“Mfano ni kwamba katika hali ya kawaida, mtoto wa mwaka mmoja
hutabasamu au kuwa na furaha kila wakati, huiga mambo mbalimbali
anayoona na kufuatilia vitu anavyoviona vikisogea, lakini mtoto mwenye
ugonjwa huu hafanyi vitu hivi,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kliniki ya Lotus, Dialla Kassam,
alisema uelewa bado ni mdogo nchini Tanzania na watoto wengi hujulikana
wakati hali imekuwa mbaya zaidi.
“Kukosa uelewa wa hali hii ya watoto wenye mahitaji huwafanya
walimu na wazazi kudhani watoto ni watundu, wavivu au wanakera na wakati
mwingine huadhibiwa kwa sababu hiyo wakati watoto hawa wanahitaji
uangalizi wa karibu, kupendwa na kupata msaada kutoka kwa walimu na
wenzao,” alisema.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment