Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk Willibrod Slaa amedai kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, huenda
usiwe huru na haki kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo uamuzi wa Serikali
kununua magari ya polisi zaidi ya 700 kwa lengo la kukabiliana na
wapinzani.
Dk Slaa alitoa kauli hiyo juzi wakati akihutubia wananchi wa Mji wa Vwawa, mkoani Mbeya. Alisema badala ya kutengeneza na kuboresha mazingira mazuri ya uchaguzi, Serikali inaonekana kujiandaa kupambana na wapinzani.
“Serikali imetumia dola 29 milioni kununua magari
700 ya polisi, yakiwamo yale maarufu kwa jina la ‘washawasha’. Haya yote
wanataka yatumike wakati wa uchaguzi,” alisema Dk Slaa.
Kuhusu vituo vya kuandikisha wapigakura wilayani
hapa, Dk Slaa aliwataka mawakala kuwapa ushirikiano wananchi ili waweze
kujiandikisha kwa wingi. “Mawakala na viongozi wa Serikali, acheni kuwabagua wananchi kwa misingi ya ushabiki wa vyama vya siasa,” alisema.
Alisema ubaguzi wa aina yoyote kwa misingi ya vyama haukubaliki na kwamba kila mmoja ana haki ya kujiandikisha. Aliongeza: “Ubaguzi katika uandikishaji kwa kuwataja wananchi kwa majina ya vyama CCM, Chadema au CUF hautavumilika.”
Akizungumzia wanafunzi wa vyuo vikuu na sekondari
kupata haki ya kupiga kura, Dk Slaa alimtaka Mwenyekiti wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva kuwaruhusu vijana hao kupiga kura
mahali popote kutokana na ukweli kwamba siku hiyo watakuwa maeneo
tofauti na walikojiandikisha.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu
Kusini, Mchungaji Stephen Kimondo alisema hivi sasa kuna mpasuko kati ya
Serikali na wananchi wake ndiyo maana kila kukicha migomo na maandamano
inazidi kutikisa.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment