Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Valentino Mokiwa.
Wakati mchakato wa watangaza nia ya kuwania urais
ukiendelea nchini, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es
Salaam, Dk. Valentino Mokiwa, ametaja sifa anazopaswa kuwa nazo rais
ajaye.Dk. Mokiwa ambaye aliwahi kuwa mkuu wa kanisa hilo, alitaja sifa
hizo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari
juu ya maadhimisho ya miaka 50 ya dayosisi hiyo yanayotarajia kufanyika
Julai 5, mwaka huu pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana
ikiwamo elimu, afya na huduma za jamii.
Askofu Mokiwa alisema kiongozi anayetaka kuiongoza nchi anapaswa
kufahamu changamoto kubwa ambazo zinalikabili taifa na namna ya
kupambana nazo. “Wote waliotangaza nia na wengine wanaotarajia kutangaza wana sifa
hizo, nawapongeza na kuwatakia heri, hata mimi ningeweza kutangaza nia
kama urais usingekuwa ni majukumu makubwa, lakini kiongozi anayetaka
kuliongoza Taifa hili anapaswa kuweka vipaumbele muhimu kuwa suala la
kwanza kwa Watanzania kuliko sura yake,” alisema Askofu Mokiwa.
UMASKINI
Alitaja changamoto ya kwanza ambayo Rais ajaye anapaswa aifanye kuwa kipaumbele chake ni tatizo la umaskini uliokithiri.
Alisema umasikini umesababisha kuenea kwa magonjwa makubwa kama
virusi vya ukumwi na kuua watu wengi, watu kuchomwa moto pamoja na
kugombanisha majirani. “Umaskini unaumiza watu, unaniumiza mimi, unasababisha maradhi,
hatutaki rais atakayekuja na kipaumbele chake na kuacha kipambele hiki
ambacho kinawaumiza watu wengi,” alisema.
RASILIMALI
Changomoto nyingine aliitaja kuwa ni rasilimali za taifa kama gesi
na madini ambayo rais ajaye anapaswa kuitatua na kuifanya kipaumbele
chake. Askofu Mokiwa alisema rais ajaye anapaswa kutumia rasilimali za
nchi kushusha ukali wa maisha na siyo kugawa rasilimali za taifa kwa
nchi nyingine au watu wachache.
KUBORESHA MAISHA YA WATUMISHI
“Changamoto ya kukimbiwa na wataalamu wetu kutokana na kutolipwa
vizuri kukimbilia mataifa mengine kutoa huduma, lakini kumbe tunaweza
kuboresha maisha yao na kusababisha kubaki nchini na wengine kuja,”
alisema.
Alifafanua kuwa rais ajaye anatakiwa kutambua changamoto hiyo
ambayo kama ikimalizika uwezekano wa wataalamu kutoka mataifa mengine
kuja nchini upo. “Natamani siku moja nione shule za kata zinafundishwa na walimu
kutoka mataifa mbalimbali, kama tunavyoshuhudia wataalamu wetu wakiwa
katika mataifa mengine,” alisema Askofu Mokiwa.
Aliseman rais ajaye anapaswa afahamu na kuona kuwa bajeti ya serikali inaboresha masuala ya elimu kwa kulipa vyema watumishi.
SAYANSI, TEKNOLOJIA
Alisema Rais ajaye anapaswa kufahamu kuwa ukuaji wa sayansi na
teknolojia ambayo Watanzania ni wanufaikaji, inahitaji kuwa na
wataalumu na wabunifu wa mambo mbalimbali kutoka nchini. Askofu Mokiwa alieleza kuwa rais anapaswa kufahamu kuwa kupata
wazalishaji na wabunifu ni kuongeza idadi kubwa ya wageni kuja nchini
kuchukua ujuzi badala ya kutegemea wabunifu kutoka nje.
ULINZI WA TAIFA NA MIPAKA
Askofu Mokiwa alibainisha kuwa rais ajaye anatakiwa kulinda mipaka ya taifa ili kuboresha usalama wa nchi na Watanzania. “Mtanzania anapaswa kuwa huru, tofauti na sasa unahofia kusafiri
kutokana na kushamiri kwa wimbi la majambazi wanaoingia nchini kwa njia
ya makontena, hivyo rais ajaye atambue kulinda na kuimarisha mipaka ya
nchi,” alisema.
MIGOGORO YA KISASA
Kuhusu migogoro ya kisiasa, Askofu Mokiwa alisema ni chanzo cha
uvunjifu wa amani kutokana na tamaa za madaraka miongoni mwa wanasiasa
ndani ya vyama ambayo inatokana na nguvu ya fedha walizonazo. “Kwa sasa tuko kwenye kipindi ambacho vyama vya siasa vitaanza
kutumia vijana kupambana badala ya kutumia ajenda ya ajira kwa vijana,”
alisema.
UBORA WA MATIBABU
Askofu Mokiwa alisema anasikitishwa na kitendo cha mawaziri na
viongozi wakubwa wa nchi kwenda kupata matibabu nje ya nchi kwa magonjwa
ambayo yanaweza kutibika nchini. Alisema ni vyema rais ajaye akatambua kuwa Watanzania wanahitaji usawa katika matibabu.
Alisema changamoto kwake iwe ni kuleta madaktari kutoka mataifa mengine ili watoe matibabu nchini kwa usawa. “Kiongozi ajaye aondokane na suala hilo la kukosekana kwa madaktari
wenye sifa kwani viongozi wakubwa kutibiwa nje ya nchi ni kuwatukana
madakari wetu,” alisema.
HAKI ZA WATANZANIA
Askofu Mokiwa alisema masuala ya elimu, afya, maji na mahitaji
muhimu ni mambo ambayo ni haki ya Watanzania hivyo hayapaswi kuwa
vipaumbele vya wagombea. “Wagombea waje na vitu ambavyo ni vya maana na siyo mambo ambayo ni
haki ya Watanzania, kuyafanya kuwa hoja ya kutaka kuwa rais wa nchi,”
alisema.
KATIBA MPYA
Askofu Mokiwa alisema suala la Katiba mpya kiongozi ajaye anapaswa
kuangalia hasa vipengele ambayo vimeingizwa visivyo na maslahi kwa
Watanzania na nchi ili viondolewe kwa ajili ya usalama wa Taifa.
“Nitapenda kila anayetaka kuchukua fomu awe na mzingo wa Watanzania
kichwani kwake na furaha ya Watanzania ndio iwe furaha yake na siyo
vinginevyo,” alisema Askofu Mokiwa.
Alisema pia anatamani kukaa na wagombea wote ili kuwapa maswali magumu ambayo yataleta mstakabali wa Taifa.
UANDIKISHAJI DAFTARI LA WAPIGA KURA
Akizungumzia uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura,
alisema mashine za kuandikisha ziongezwe pamoja na siku za kuandikisha
zisiwe na kikomo.
Alisema ni vyema Watanzania wakaendelea kujiandisha kutokana na
watu kuongezeka pamoja na kufikia sifa za kujiandikisha kila mara. “Tukiweka kikomo cha kuandikisha Watanzania kwenye daftari la
wapiga kura ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kupiga kura. Kila mwezi,
siku watu wanatimiza vigezo hivyo daftari liachwe ili kila mara watu
wajiandikishe,” alisema.
MIAKA 50 YA DAYOSISI
Askofu Mokiwa alisema Dayosisi hiyo inatimiza miaka 50 ya tangu kuanzishwa kwake Julai 10, mwaka 1965. Alisema kanisa hilo linajivunia mafaniko makubwa ya huduma za
jamii, kama elimu, afya, maji na mahitaji muhimu kwa majirani
wanaowazunguka, yatima na wasio na uwezo.
“Kwa kuazimisha miaka hii 50 tutafanya sherehe Julai 5, tukiwa na
malengo yale yale ya kuboresha, kudumisha na kujali jamii inayotuzunguka
katika kutoa huduma muhimu kwa kutumia wahisani wengi na makanisa ya
Anglikana ndani na nje ya nchi,” alisema Askofu Mokiwa.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment