Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ambaye kura
mbalimbali za maoni ambazo zimepigwa nchini ameonekana kuwa chaguo la
kwanza la Watanzania katika kinyang’anyiro cha urais kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM), amesema kwamba hana mpango wa kuhamia upinzani kwani
maisha yake tangu mwaka 1977 alipohitimu chuo kikuu yamekuwa ni ndani ya
chama hicho.
Alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano na wahariri nyumbani kwake
Dodoma na kuongeza kuwa kama kuna watu hawamtaki ndani ya CCM waondoke
wao yeye atabakia ndani ya chama hicho. Kadhalika, alisema hana mpango mbadala katika safari yake ya
kuwania urais kupitia CCM, alisisitiza kuwa mpango wake ni mmoja tu
kutafuta ridhaa ya CCM kuwatumikia wananchi ili kuwaletea maendeleo.
Pamoja na kueleza kuridhishwa kwake na mafanikio ya serikali na
CCM, alitoa hadhari kwamba upinzani umeanza kuimarika mijini na vijijini
na kuonya kwamba wakibweteka wanaweza kupoteza dola. Alikumbusha kwamba katika bara la Afrika vyama vingi vilivyoleta
uhuru (vyama vya ukombozi) vimeondolewa madarakani na ikitokea hivyo
havirejei tena madarakani.
Alisema pamoja na kazi nzuri ambayo imefanywa na Rais Kikwete
katika kutekeleza ilani ya CCM, hakuna sababu ya kubweteka ni lazima
watu waongeze bidii zaidi katika kujituma na kutekeleza wajibu wao.
KULIPIZA KISASI
Lowassa alisema madai yanayotolewa dhidi yake kwamba ni mtu wa
visasi hayana maana kwani yeye ni Mkristo na anaamini katika imani yake
kwamba “samehe saba mara sabini.” “Siamini katika kufukua makaburi yaliyopita yamepita,” alisema na
kusisitiza kuwa anatafuta uongozi wa nchi ili kuwaletea wananchi
maendeleo na siyo kuchimbana.
Alitaka watu wafufue moyo wa uzalendo kwa nchi yao kwani siku hizi
unapungua sana. Aliomba watu wawe na mapenzi na nchi yao kwani hakuna
kwingine kokote pa kwenda.
Alizungumzia kauli za “yeye na Kikwete hawakukutana barabarani” na
kuhoji kwamba ni kwa nini uhusiano wake na Rais Kikwete umekuwa hoja
kwa kuwa hakuna kokote ambako uhusiano huo umekwaza lolote katika
utekelezaji wa majukumu ya nchi. “Sisi ni marafiki. Anaendelea na kazi zake, ninaendelea na kazi zangu. Ume-influence nini?” aliuliza.
Alitumia mkutano huo pia kukanusha madai kuwa Mwalimu Julius
Nyerere alimkataa. “Ni maneno ya kutunga, hakuna ushahidi ni uongo wa
kutupa,” alisisitiza. Jumamosi ijayo Lowassa anatarajia kutangaza nia ya kuwania urais
kupitia CCM. Tayari Amina Salum Ali ametangaza nia yake, huku Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, akisema kuwa
anatarajia kutangaza nia kijijini kwako.
Mbali na Amina Salum Ali, kuna makada sita waliojitangaza kwamba
watagombea urais ambao ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari
Makamba; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi
Maalum, Profesa Mark Mwandosya; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalah.
Wanaotajwa kugombea ni Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika,
Steven Wasira; Waziri wa Ujenzi, Dk. John Maghufuli; Waziri wa Uchukuzi,
Samwel Sitta; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro; Spika
wa Bunge, Anne Makinda; Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye; Waziri
wa Mambo ya Nje, Bernard Membe; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na
Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment