Mke wa Rais, Salma Kikwete akimsalimia mjumbe mwenzake wa Halmashauri
Kuu ya CCM, Stephen Wasira mjini Dodoma jana. Wajumbe wengini ni Raphael
Chegeni (wa pili kushoto) na Profesa Mark Mwandosya.
Mbio za kuwania urais
na nafasi nyingine kupitia CCM zimetangazwa rasmi baada ya Halmashauri
Kuu ya Taifa (NEC) kutoa ratiba ikibainisha kuwa mgombea urais chama
hicho tawala atajulikana Julai 12, siku mbili baada ya yule wa Zanzibar
kufahamika.
“Sasa ni ‘ruksa’ kwa wanaotafuta uteuzi wa
kupeperusha bendera ya chama katika nafasi za urais, ubunge, udiwani na
uwakilishi kuchukua fomu kwa tarehe zilizopangwa,” Katibu wa NEC Itikadi
na Uenezi, Nape Nnauye, alisema jana mjini hapa. Wanaotaka kuwania
urais wataanza kuchukua fomu kuanzia Juni 3 hadi Julai 2. Nape alisema Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ambao
ndiyo wenye jukumu la kuchagua mgombea urais wa chama hicho, utafanyika
kwa siku mbili kuanzia Julai 11 hadi 12. Alisema mgombea urais wa
Zanzibar, atapitishwa na NEC Julai 10.
Mara baada ya kupitishwa kwa ratiba ya mchakato
huo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Mwigulu Nchemba alijizulu
wadhifa huo ili kupata fursa ya kuwania urais.
Naibu Waziri huyo wa Fedha, alimwandikia
mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kuomba kuachia ngazi,
naye akampa nafasi kueleza nia hiyo mbele ya kikao. Akizungumza mkutanoni hapo, Mwigulu alisema amefikia uamuzi huo kwa kuwa hawezi kuwa refa na mchezaji.
Kutokana na uamuzi huo, Rais Kikwete alimteua
aliyekuwa msaidizi wake kisiasa, Rajab Luhavi kuwa mjumbe wa Halmashauri
Kuu na kuchukua nafasi ya Mwigulu.
Uchukuaji fomu urais
Akizungumzia utaratibu wa uchukuaji fomu alisema
kwa wanaowania kuteuliwa kugombea urais wataanza kuchukua fomu hizo Juni
3, mwaka huu na mwisho wa kuzirejesha ni saa 10.00 jioni ya Julai 2.
Alisema muda huo wa Juni 3 hadi Julai 2, pia
utatumika kwa wagombea urais kutafuta wadhamini 450 katika mikoa 15,
kati ya hiyo mitatu ikiwa ya Zanzibar, kwa maana ya Pemba na Unguja. Utaratibu wa zamani kwa wagombea uliwataka kuwa na
wadhamini 250 katika mikoa 10, miwili iwe ya Zanzibar. Pemba mmoja na
mwingine Unguja.
Alisema hatua hiyo ya wadhamini 450 imetokana na
kuongezeka kwa idadi ya wanachama na mikoa na kwamba idadi hiyo
haitakiwi kupungua wala kuzidi.
Vikao vya mchujo
Urais Zanzibar
Ubunge, uwakilishi na udiwani
Gharama za uchaguzi
Sadifa asusa
Mikoa ya Bara imeongezeka kutoka 20 hadi 25 na Zanzibar imebaki mitano, Unguja mitatu na Pemba miwili. “Safari hii ukija na wadhamini zaidi ya 450 unarudi nao nyumbani kwako, sisi hatuwataki hao wengine,” alisema.
Akizungumzia masharti ya uchukuaji fomu, alisema
chama kimepiga marufuku mbwembwe na shamrashamra katika uchukuaji na
urudishaji wa fomu.
Nape alisema masharti mengine ni wajumbe wa NEC
kutotakiwa kuwadhamini wagombea, kwa sababu wao ni waamuzi katika vikao
vya juu. “Pia mwanachama haruhusiwi kumdhamini mgombea zaidi ya
mmoja.”
Vikao vya mchujo
Kuhusu vikao vya uchujaji wa wagombea urais, Nape
alisema Kamati ya Usalama na Maadili itafanya kikao chake Julai 8,
kuangalia utaratibu wa kanuni kama haukuvunjwa na kitafuatiwa na Kamati
Kuu Julai 9 na kisha NEC Julai 10.
Urais Zanzibar
Nape alisema tarehe za uchukuaji wa fomu kwa wagombea wa Zanzibar, zinafanana na zile za wagombea wa urais wa Muungano. Alisema Kamati ya Usalama na Maadili ya Zanzibar, itafanya kikao chake Julai 4, ikifuatiwa na Kamati Maalumu Julai 5.
Alisema kikao cha Kamati Kuu kitakachofanyika Julai 9, kitapitia majina ya wagombea watakaojitokeza kuwania nafasi hiyo. “Watatakiwa watafute wadhamini 250 kutoka mikoa mitatu ya Zanzibar, lakini angalau mkoa mmoja uwe Pemba au Unguja,” alisema.
Ubunge, uwakilishi na udiwani
Nape alisema wagombea wa nafasi hizo watachukua fomu Julai 15 na
kuzirejesha Julai 19, saa 10.00 jioni. “Kampeni zitaanza Julai 20 na
kumalizika Julai 31 mwaka huu.”
Alisema Agosti Mosi mwaka huu, itakuwa ni siku ya kupiga kura za maoni kwa wagombea wa ngazi zote.
Gharama za uchaguzi
Nape alisema gharama za kuchukua fomu zipo
kikanuni na hazijabadilishwa. Alisema fomu ya kuwania urais ni
Sh1milioni, ubunge ni Sh100,000 na udiwani ni Sh50,000.
“Sisi hatufanyi biashara. Gharama zipo kwenye kanuni,” alisema.
Akizungumzia jinsi ya kuzuia rafu katika uchaguzi,
alisema chama kimeweka mikakati ya kudhibiti kadi feki kwa kutaka kila
mwanachama kuwa na kadi nyingine (kadi ya benki, mpigakura au
kitambulisho cha kazi) kuthibitisha uhalali wake. “Daftari la wanachama tutalifunga Julai 15 ili tuweze kufanya uhakiki wa wanachama,” alisema.
Sadifa asusa
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa (UVCCM) Taifa,
Sadifa Juma Khamis jana aliondoka kabla ya muda wa kikao cha NEC
kumalizika, akieleza kukasirishwa na mabadiliko kuhusu uteuzi wa viti
maalumu kundi la vijana kuhamishiwa Jumuiya ya Wanawake wa chama hicho
(UWT).
“Itakuwaje nafasi za vijana wachaguliwe na watu
wenye umri zaidi ya miaka 40. Naondoka zangu nakwenda Zanzibar,” alisema
Sadifa na kuondoka katika viwanja vya White House ulipofanyika mkutano
wa NEC.
Akielezea uamuzi huo, Nape alisema NEC imeamua
kulipeleka jukumu la uteuzi wa mwisho wa wabunge UWT. Hata hivyo,
alisema kura za mwisho tu ndizo zitakazopigwa na UWT kwa kundi hilo.
Alisema NEC imeongeza viti maalumu viwili kutoka Baraza lake la Wazee.
Uchaguzi
Dk Shein afiwa, aondoka kikaoni
Uchaguzi
Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Juu Tanzania la CCM leo linafanya mkutano mkuu ambao utachagua viongozi wa ngazi ya Taifa.
Katibu Mtendaji Mkuu wa shirikisho hilo,
Christopher Ngubiagi alisema mkutano huo utakaofanyika katika ukumbi wa
Kilimani na utafunguliwa na Rais Kikwete.
Dk Shein afiwa, aondoka kikaoni
Wakati mkutano ukiendelea, Makamu Mwenyekiti wa
CCM (Zanzibar) na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein alilazimika
kuondoka Dodoma kutokana na msiba wa dada yake, Fatma Mohamed Shein (72)
uliotokea jana.
Fatma aliaga dunia saa 4.30 asubuhi katika
Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar alipokuwa amelazwa kwa muda kutokana
na maradhi ya saratani.
Msemaji wa familia ya marehemu, Said Mohamed
alisema mipango ya mazishi itawekwa bayana leo baada ya kuwasili Rais
Shein. Fatma aliwahi kupelekwa India kwa matibabu na kurejeshwa katika
Mnazi Mmoja alikolazwa mara mbili.
Mohamed alisema mazishi yatafanyika katika makazi
ya familia Kidongo Chekundu, Mjini Magharibi. Fatma ameacha mtoto mmoja,
Saih Mohamed Ali.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment