Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi,
akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam
jana.Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi,
ameeleza kusikitishwa dhidi ya majibu yaliyotolewa na Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais Ikulu kuhusu taarifa za kamchafua zilizochapishwa na
gazeti la Taifa Imara Machi 20, mwaka huu.
Dk. Mengi, alisema jana kuwa majibu yaliyotolewa na Mkurugenzi wa
Kurugenzi hiyo, Salva Rweyemamu, siyo ya busara kwani yanapuuza usalama
wa maisha yake. “Majibu haya ya Salva yanaongeza hofu ya usalama wa maisha yangu
jambo ambalo siyo dogo na la kupuuzwa kama anavyoona yeye,” alisema Dk.
Mengi na kuongeza:
“Ukiangalia, ukisoma kiundani majibu ya barua ya Rweyemamu, nina
kila sababu ya kuhofia usalama wa maisha yangu. Shughuli zake Ikulu ni
za kuheshimiwa, lakini awe na busara katika shughuli zake kunishauri
eti niende polisi kuhusu suala hilo ni kama kunifanya nionekane sina
busara kama yeye.”
Alisema uhai wa mtu siyo jambo dogo wala siyo la kupuuzwa na kwamba
busara ilihitajika katika kushughulikia suala hilo, lakini haikuwa
hivyo kwani majibu hayo yamesababisha tatizo hilo dhidi ya usalama wa
maisha yake kuwa pale pale.
Machi 23, mwaka huu, gazeti la Taifa Imara, lilichapisha habari
iliyoeleza kuwa, Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe,
alimchongea Dk. Mengi kwa Rais Kikwete, kwamba ndiye kinara wa kuihujumu
serikali yake na alikuwa anamshawishi Zitto kujiunga na mipango hiyo.
Habari hiyo iliendelea kudai kuwa, Dk. Mengi aliapa kumshughulikia
Rais Kikwete kwa nguvu zake zote amalizapo muda wake wa urais huku Rais
Kikwete naye akiapa kupambana na yeye (Dk. Mengi). Aprili 17 mwaka huu, katika mkutano wake na waandishi wa habari,
Dk. Mengi alisema, tuhuma hizo dhidi yake zilimshtua sana na kumpa hofu
kubwa kwa usalama wa maisha yake hivyo kuilaumu kurugenzi ya
mawasiliano Ikulu na Idara ya Habari (Maelezo) kwa kukaa kimya zaidi ya
wiki tatu bila kutoa ufafanuzi wowote kuhusu habari hiyo ambayo pia
inamhusu Rais na kuiacha kusambaa.
“Nilitoa kauli kwamba, tuhuma hizo dhidi yangu zilinishtua sana na
kwamba tamko la Mheshimiwa Rais kwamba atapambana nami lilinipa hofu
kubwa kuhusu usalama wa maisha yangu,” alisema Dk. Mengi.
Dk. Mengi alisema majibu yaliyotolewa na kurugenzi ya Mawasiliano
ya Rais Ikulu, yalieleza kuwa Rais hakuwahi kuwa na mawasiliano na Zitto
Kabwe kama ilivyoelezwa na kwamba haikufanya lolote kutokana na kubanwa
na majukumu, hivyo kupuuza habari hizo kwa kuziona ni ndogo na za
upuuzi. “Salva hakufanya lolote eti kutokana na kuwa na majukumu mengi na
alipuuza habari hizo kwa sababu aliziona ni jambo dogo na upuuzi,”
alifafanua Dk. Mengi na kuongeza:
“Bwana Rweyemamu alisema pia kwamba alinishangaa kwa kutokutoa
taarifa katika kituo chochote cha Polisi kuhusu hofu ya usalama wa
maisha yangu. Majibu haya ya Salva yanaongeza hofu ya usalama wa maisha
yangu, jambo ambalo siyo dogo na la kupuuzwa kama anavyoona yeye.”
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment