Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akizungumza na wahariri wa vyombo vya
habari, nyumbani kwake, Dodoma jana.
Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa hana mpango wa kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na iwapo
kuna mtu anamchukia ndani ya chama hicho, ni vyema akahama kwa sababu
yeye hana mpango huo.
Lowassa alitoa kauli hiyo alipozungumza na
wahariri wa vyombo vya habari nyumbani kwake mjini Dodoma jana ambako
alieleza mambo mbalimbali kuhusu afya yake, suala la Richmond, elimu,
ajira, utajiri wake na hali ya kisiasa kwa ujumla.
Hata hivyo, Mbunge huyo wa Monduli hakutaka kujibu
maswali mengi kwa madai kuwa atazungumza Jumamosi mjini Arusha
atakapotangaza nia yake ya kugombea urais.
Kuhama CCM
Alipoulizwa iwapo yupo tayari kuhama CCM na kwenda
upinzani asipopitishwa na chama hicho kuwania urais alisema: “Sina
mpango wa kuhama chama changu, sina plan B, mimi ni plan A tu, tangu
nimemaliza Chuo Kikuu mwaka 1977 nimekuwa mwana-CCM, sijafanya kazi nje
ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa
Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC). Maisha yangu yote yapo CCM. “Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi,” alisema.
Kimya miaka saba
Lowassa aliyejiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008
kutokana na kashfa ya mtambo wa kufua umeme wa Richmond, alisema kimya
chake baada ya tukio hilo kilitokana na siasa nyingi za uhasama na
kutishiana.
“Kwa miaka saba, niliona ni hekima kunyamaza,
askofu mmoja alinifundisha kuwa ukimya ni hekima kutoka kwa Mungu.
Nilichagua kuwa kimya. Nilinyamaza kwa sababu ilikuwa salama kunyamaza,
ningezungumza ningeweza kutibua mambo kwenye nchi na kusababisha mambo
ambayo hayapo.
“Nilinyamaza ili kuipa muda Serikali ifanye kazi
yake.... sikupenda kuzungumza kwa sababu ya siasa nyingi za uhasama na
kutishiana kwingi, kuna kusingiziana kwingi, kufitiniana kwingi. Kukaa
kimya ni jambo gumu sana kwa mwanasiasa, lakini nashukuru Mungu niliweza
hilo,” alisema Lowassa ambaye Jumamosi atatangaza nia ya kuwania urais
mjini Arusha.
Wagombea wapime afya
Wagombea wapime afya
Alipoulizwa kuhusu madai kuwa afya yake inaterereka, alisema anaamini yupo fiti na akashauri wagombea urais wote wakapimwe. “Hata nikikimbia kilomita 100 watasema mimi
mgonjwa. Hivi karibuni nilitembea kilomita tano na albino jijini Dar es
Salaam, kuna watu wakasema nimechoka sana, nimepata ‘stroke’ na
nimekimbizwa Ujerumani kutibiwa, huo ni upuuzi mtupu. Kuna chuki
imeingia katika siasa zetu na kutakiana mabaya. Afya ni neema kutoka kwa
Mungu tu. Napenda kuwahakikishia kuwa nipo fiti na nipo fiti na kwa
lolote. Nadhani ni wakati sasa kwa chama chetu waweke utaratibu
wanaogombea nafasi hii ambayo nitaitangaza Jumamosi, tukapime wote afya
na mimi nitakuwa wa kwanza kujitokeza kwenda kupima.
“Twendeni tukapime tuone nani mgonjwa. Tuonane kwenye uwanja wa
mapambano katika mchakamchaka wa maendeleo, ninajua nitawashinda kwa
mbali,” alisema.
Sakata la Richmond
Kuhusu sakata la Richmond, ambalo lilimfanya
ajiuzulu uwaziri mkuu, Lowassa alisema tatizo kubwa halikuwa kuhusu
mitambo hiyo ya umeme ila uwaziri mkuu. “Ajenda haikuwa kuhusu Richmond, ila uwaziri mkuu
ndiyo maana niliwaachia. Tunajifunza nini katika hilo, wakubwa wawili
wa Marekani, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje (Hillary) Clinton na Rais
wake (Barack) Obama, wote wamekuja Tanzania na wamethibitisha kuwa ile
mitambo ni mizuri. Lakini jingine tulilojifunza katika ubishi ule
umeisababisha nchi hasara ya Dola 120 milioni,” alisema Lowassa.
“Moja ya ushauri wangu wakati ule ilikuwa ni
kutaka kuvunja mkataba wa Richmond nikaita wataalamu, nikawaelezea
kuhusu habari za magazeti kuwa zinasema hawa jamaa (Richmond) hawana
fedha, hebu angalieni, nikaita wataalamu na mwanasheria mkuu,
nikawaambia kuna hii habari kuweni makini, pamoja na hayo nikaweka kwa
maandishi kwa mwanasheria mkuu, pia kulikuwa na timu ya mashauriano ya
Serikali iliyokuwa chini ya makatibu wakuu nao walikuwa na vikao vyao,
ilikuwa inaongozwa na (Katibu Mkuu Wizara ya Fedha (Gray Mgonja) nao
wakakutana chini ya Katibu Mkuu Kiongozi na baada ya kukutana wakatoa
uamuzi ambao sina haja ya kuujadili. Lakini ubishi ule umetugharimu Dola
120 milioni. “Nilipotaka mkataba uvunjwe nilikuwa nimetoa
uzoefu wangu kwani kabla ya kuwa waziri mkuu nilikuwa nimekuwa waziri wa
maji na mifugo ambako nilivunja mkataba wa kampuni ya Kiingereza
iliyokuwa imewekeza katika mradi wa maji Dar es Salaam ya City Water.
“Chini ya uongozi wa Rais (Benjamin) Mkapa
tukagundua hawa jamaa (City Water) ni matapeli…tulifanya kikao saa tisa
alasiri, tukachukua kibali cha kumkamata yule Mzungu wa City Water na
tukamfukuza akaondoka siku hiyohiyo kwa ndege kurudi kwao, tulifanya saa
tisa alasiri ili asiende mahakamani kupata zuio, kwa hiyo tulivizia
muda huo ili asije kwenda kupata zuio.
Nini tofauti ya Lowassa nje ya Serikali na ambaye angeendelea kuwa waziri mkuu na kisha kugombea urais? “…Naamini kuwa kama tungeanza kwa kasi ile tuliyoanza nayo nikiwa waziri mkuu, sasa ningepita napunga mkono ningepata kura zote… lakini kinachonisikitisha tumekuwa hatufanyi maamuzi magumu au rahisi, kila kitu kinakwenda legelege. Rais amefanya jitihada kubwa, lakini kuna mambo katika nchi hayaendi, matokeo yake Uganda, Kenya na Rwanda zinatupita sasa, haifai, lakini nawaachia uhondo nitaelezea vizuri Jumamosi, Arusha.”
Nini tofauti ya Lowassa nje ya Serikali na ambaye angeendelea kuwa waziri mkuu na kisha kugombea urais? “…Naamini kuwa kama tungeanza kwa kasi ile tuliyoanza nayo nikiwa waziri mkuu, sasa ningepita napunga mkono ningepata kura zote… lakini kinachonisikitisha tumekuwa hatufanyi maamuzi magumu au rahisi, kila kitu kinakwenda legelege. Rais amefanya jitihada kubwa, lakini kuna mambo katika nchi hayaendi, matokeo yake Uganda, Kenya na Rwanda zinatupita sasa, haifai, lakini nawaachia uhondo nitaelezea vizuri Jumamosi, Arusha.”
Elimu au kilimo kwanza?
Akizungumzia kuhusu kupingana na kaulimbiu ya
Serikali ya ‘Kilimo Kwanza’, Lowassa alisema ataendelea kushikilia
msimamo huo kwa sababu elimu ndiyo kila kitu katika maisha ya mwanadamu.
“Mimi sikubaliani na wenzangu wanajua, sikubaliani
na kilimo kwanza, naamini ‘elimu kabla, kilimo kwanza baadaye’.
Tukitaka nchi yetu ipige hatua ni lazima tuwekeze katika elimu... Nchi
zote za mashariki ya mbali waliwekeza katika elimu, kuna shule za kata
hazina walimu, lazima tuwekeze kwenye elimu ili tujikomboe,”
alisisitiza.
Ajira kwa vijana
Kuhusu ajira kwa vijana, Lowassa alisema bado anaamini kuwa hilo
ni bomu ambalo lisipopatiwa majibu litapasuka. “Wakati ule nilisema
hilo, waziri mmoja akanishambulia akinipinga akisema takwimu zangu si
sahihi na hakuna tatizo, lakini bado mimi naamini kuna tatizo kubwa.
“Machafuko ya Afrika Kaskazini yalitokana na
vijana kukosa kazi, haiwezekani vijana wamalize chuo kikuu, kidato cha
sita na vyuo vingine wakarudi mitaani kwa sababu hakuna kazi, hilo ni
jambo gumu. “Duniani kote wakati wa uchaguzi lazima wagombea
waseme watatengeneza ajira ngapi, hata Obama alipogombea kwa mara ya
pili alishinda kwa sababu alitengeneza ajira kwa vijana.
“Tunaweza kutumia gesi tuliyonayo kukopa fedha na
kuanzisha ajira kwa vijana kwa kuwapa mashamba wakalima michikichi.
Tuwekeze maeneo ambayo yataleta ajira kwa vijana. Ukiniamsha usingizini
uniulize kipaumbele changu nitakwambia ajira, ajira, ajira,” alisema.
Urafiki na JK
Alipotakiwa kuzungumzia uhusiano wake na Rais
Jakaya Kikwete, Lowassa alisema hadhani kama hiyo ni ajenda. “Sidhani
kama hiyo ni ajenda, acheni maneno yasiyokuwa na maana, kila mtu ana
marafiki, mbona hatuwaulizi, sidhani kama kuna tatizo.” alisema kwa
kifupi.
Utajiri wake
Alipoulizwa ana utajiri kiasi gani na fedha
anazochangia kwenye harambee makanisani na misikitini zinatoka wapi,
Lowassa alisema anatamani angekuwa tajiri, lakini anachukia umaskini.
“Tatizo siku hizi kuna maneno mengi, kila nyumba
nzuri wanasema ya Lowassa. Mimi nina nyumba chache na ng’ombe kati ya
800 na 1,000. Kwetu Umasaini unapokuwa kiongozi unapewa ng’ombe ili
usipate taabu kwa ajili ya kuwakarimu wageni wanapokuja wala usiwe
ombaomba au usichukue rushwa. Lakini kama kuna mtu mwenye shaka na
utajiri wangu aende Sekretarieti ya Maadili kule ataona kila kitu,”
alisema.
“Nachukia umaskini, napenda utajiri, natafuta
uongozi wa nchi hii ili kuwasaidia Watanzania kuwa matajiri na si
kukumbatia umaskini. Hii kudanganya watu kwamba nikiwa maskini ndiyo
nafaa kuwa kiongozi ni ujinga ambao inabidi tuuache. Nataka watu wawe
matajiri, tuache kuwabeza matajiri, matajiri wawe ni mfano kwa wengine,
watu kama (Reginald) Mengi, (Said) Bakhressa na (Nazir) Karamagi
wanatakiwa kuwa mfano kwa wengine, tungekuwa na watu kama hawa 20,000,
nchi hii ingekuwa haikopi nje. Naukataa umaskini na nauchukia umaskini.
Nakataa umaskini na ninataka watu wanihukumu kwa hilo,” alisema.
Kuhusu kushiriki harambee nyingi na anakopata
fedha alisema: “Sina fedha ila nina marafiki wengi, nikipata mwaliko wa
kuchangia nawatafuta marafiki zangu wanachanga. Mfano ‘juzi’
nilipomwakilisha Makamu wa Rais mjini Arusha, marafiki zangu walichangia
Sh100 milioni, Makamu wa Rais alichangia Sh10 milioni na watu wa Arusha
wakatoa Sh100 milioni. Hizo hazikuwa fedha zangu, ila ni watu
walichangia. Nafurahia kufanya harambee, harambee zangu zinasaidia
misikiti, makanisa na shule, hivi ni vitu vya maendeleo ya watu,
nawashauri na wabunge wafanye hivyo kwenye majimbo yao. Hata shule za
kata zilichangiwa kwa harambee, tusionee aibu ni jambo jema,”
alisisitiza.
Tahadhari kwa CCM
Akijibu swali kuhusu tahadhari inayotakiwa kuchukuliwa na CCM
mwaka huu, Lowassa alisema upinzani umeanza kupata nguvu, nguvu kubwa
mijini na vijijini. “Sisi ni chama dola tumefanya mambo mazuri, lakini
tusibweteke wenzetu wanajiandaa vizuri na sisi tunapaswa kujiandaa
vizuri. Vyama vingi vilivyoleta ukombozi sehemu nyingi vimeshaondolewa
mfano UNIP, Kanu na mkishaondolewa hamrudi madarakani, meseji yangu
kubwa kwa chama changu tusifanye mchezo, tusibweteke badala yake tufanye
kazi kubwa zaidi.”
Kulipa kisasi
Alipoulizwa kama atalipa kisasi akishinda urais, Lowassa alisema hana mpango wa kulipa kisasi kwa sababu hana kisasi. “Siamini katika kufukua makaburi, tufanye kazi.
Mimi ni Mkristo naamini katika maandiko ya Bwana Yesu, alisema samehe
saba mara sabini. Tuchape kazi.”
Kukataliwa na Nyerere
Alipoulizwa kama kweli Mwalimu Julius Nyerere
amewahi kumkataa alisema jambo hilo si la kweli. “Jambo hili si la
kweli, sijawahi kukataliwa.”
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment